Rais waameutaka uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuendelea kufanyakazi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwani Wizara hiyo imepata mafanikio makubwa.Hayo aliyasema leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wakati ilipowasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2019/2020 na Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021.

Rais Dk. Shein alieleza Imani yake kwamba zoezi hilo limesaidia kwa kiasi kikubwa katika kutathmini shughuli za Wizara za Serikali.Alisema kuwa Serikali imeweka mkazo katika kufanya tafiti hatua ambayo imepelelekea kuanzisha Taasisi mbali mbali hapa nchini na kueleza kuwa kituo cha Utafiti cha Kizimbami ndio cha mwanzo katika nchi za Afika Mashariki hiyo ni kuonesha wazi kuwa Zanzibar imepiga hatua muda mrefu.

Aidha, alieleza kuwa Taasisi za utafiti zilizopo zikiwemo za Mifugo pia, ipo hapa Zanzibar hivi sasa ambayo imekuwa ikienda kwa kasi sambamba na Taasisi ya utafiti ya uvuvi na rasilimali za bahari.Alisema kuwa taasisi hizo zimeundwa kwa ajili ya kuendeleza kilimo, uvuvi na afya kwa lengo la kuleta tija.Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi zake za kudhibiti mali zisizorejesheka ukiwemo mchanga hali ambayo imepelekea kuongezeka kwa mapato ya Serikali kwa kiasi kikubwa.Alieleza matumaini yake makubwa kuwa Zanzibar itakwenda mbele katika sekta ya kilimo kutokana na programu mbali mbali zinazotekelezwa na Wizara hiyo.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema kuwa Wizara hiyo imelenga kuendeleza mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kuifanya ya kisasa, jumuishi na chenye ushindani ambacho kinachangia sekta ya viwanda na utalii ili kuleta tija na maisha bora ya wananchi wa Zanzibar na maendeleo ya uchumi.Alisema kuwa sekta ya kilimo ikijumuisha mazao, mifugo, uvuvi, misitu na rasilimali zisizorejesheka bado inaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar.

Aliongeza kuwa sekta hiyo inatoa mchango wa moja kwa moja kwa wananchi katika kujikimu kimaisha ambapo asilimia 40 wameajiriwa na sekta hiyo na inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo ambapo kwa mwaka 2019 imechangia asilimia 21.2 ya Pato la Taifa.Akieleza kuhusu wizi na uchimbaji holela wa rasilimali ya mchanga, Waziri Mjawiri alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ imeunda kikosi shirikishi cha doria ambacho kinaendelea kupambana na wizi na uchimbaji wa mchanga kiholela pamoja na udhibiti wa ukataji ovyo wa miti.

Alieleza Mpango Kazi wa mwaka 2020/2021 ambao umelenga kuleta Mapinduzi ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kutoka Kilimo duni cha kujikimu kuelekea kilimo endelevu cha kibiashara na chenye tija pamoja na uhifadhi na matumizi.Aidha, alieleza kuwa jumla ya wafanyakazi 263 wameajiriwa ikiwemo wahudumu shambani, maafisa katika ngazi tafauti na wataalamu 68 kuanzia Digriihadi PhD,

Alieleza dhamira ya Wizara hiyo ya kuibadilisha sekta ya kilimo kuwa ya kibiashara kwa kushajiisha ukuaji wa viwanda vidogo vidogo, miradi ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu, utumiaji wa teknolojia za kisasa za uzalishaji na usindikizaji wa mazao ya kilimo, kuongeza uzalishaji pamoja na kuweka mazingira bora katika sekta hiyo.Pia, alieleza kuwa Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 inalengo la kujenga miundombinu ya umwagiliaji maji katika eneo la hekta 65 na kukarabati hekta 87 kupitia mradi wa ERPP pamoja na kukarabati hekta 87.

Kuongeza uzalishaji wa Mpunga kufikia wastani wa tani 50,000 pamoja na kuendelea kutoa huduma za matrekta na zana zake kwa wakulima na kufuatilia ukulima wa zao la mpunga katika eneo la ekari 33,800 pamoja na mazao mengine ya kilimo.Wizara hiyo pia, ilieleza lengo la kufanya tafiti 26 za kisayansi ambapo 16 ni za kilimo, 5 za mifugo na 5 za uvuvi, kufanya tafiti za kiuchumi na kijamii kwa mujibu wa ‘Zanzibar Research Agenda’, kuwajengea uwezo watafiti wa kilimo, mifugo na uvuvi na kuimarisha miundombinu ya utafiti.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa mikutano hiyo ya (Bango Kitita) imekuwa na msaada mkubwa katika kujitathmini na kujipima na kueleza haja ya kuendelezwa huku akisisitiza haja kwa viongozi na wafanyakazi wa Wizara hiyo kuendelea kuchapa kazi hasa katika kipindi hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Nae Mshauri wa Rais Pemba Dk. Mauwa Abeid Daftari akichangia katika kikao hicho alieleza haja kwa Wizara hiyo kufanya tafiti za kutosha ili kuwasaidia wakulima katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Nao viongozi wa Wizara hiyo walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuwafanya kuwa makini na kujitathmini katika utendaji wa kazi zao na kueleza jinsi ya vikao hivyo vilivyoaza katika uongozi wa Rais Dk. Shein na vilivyowasaidia kwa kuwa na nidhamu na ubunifu katika utendaji wa kazi zao.