Maelezo hayo yametolewa na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee alishiriki kikamilifu, Wizara hiyo ilieleza kuwa mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi 6.7 mwaka 2011.Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdilahi Jihad Hassan alisema kuwa kiwango cha uvuvi wa samaki kimeongezeka kutoka tani 25,693 mwaka 2010 na kufikia tani 28,759 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.6.Pia, Waziri jihadi alieleza mafanikio mengine katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha mabwa mawili ya mfano ya kufugia samaki katika maeneo ya kiungoni na Pujini Pemba kama ni mashamba darasa kwa wafugaji wa samaki.
Kuongezeka kwa idadi ya samaki kulikotokana na kuimarisha usimamizi kwa maeneo ya hifadhi na kuendelea kutoa elimu kwa wavuvi pamoja na kuongezeka kwa taaluma juu ya athari ya matumizi ya mitego haramu na njia haramu za uvuvi.
Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza mafanikiokatika sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mwamko wa ufugaji wa ngombe na mbuzi wa maziwa na kuku wa kienyeji ambapo jumla ya shamba darasa 180 za mbuzi wa maziwa, ngombe wa maziwa na kuku zimefanywa.
Uongozi huo pia, ulieleza kuwa Wizara imeandaa mipango kwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari, kutoa nafasi za ajira kwa vijana kupitia shughuli za ufugaji na uvuvi na kufanya utafiti juu ya maradhi ya mifugo.