HOTUBA YA MHESHIMIWA DK.HUSSEIN ALI MWINYI, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO LA 6 LA USAFIRI WA ANGA LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KATIKA HOTELI YA VERDE JIJINI ZANZIBAR.

TAREHE 15 - 16 MEI 2024

Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (Mb), Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki;

Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;

Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Dkt. Mngereza Mzee Miraji, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,

Ndugu Hamza Johari, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CASSOA),

Mhandisi  Richard Gatete, Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CASSOA),

Ndugu Adefunke Adeyemi, Katibu Mkuu Tume ya Usafiri wa Anga Afrika,

Naibu Mkurugenzi wa Kanda, Ofisi ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika,

Wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Wakurugenzi Watendaji wa Zamani;

Wawakilishi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,

Mwakilishi wa Shirika la Kusimamia Usalama la Kundi la Banjul Accord,

Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO-RCTP),

Mwakilishi wa  Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya,

Ndugu Waandishi wa Habari,

Wageni waalikwa,

Washiriki wa Kongamano,

Mabibi na Mabwana,

 

Assalamu Aleikum

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na afya njema tukaweza kuhudhuria Kongamano hili la sita (6)  la Usafiri wa Anga la Jamhuri ya Afrika ya Mashariki lililoamuliwa kufanyika hapa Zanzibar.

Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na   wananchi wa Zanzibar,  napenda kuwakaribisha wote hapa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakukaribisheni wajumbe wote na ninafurahi kujumuika nanyi katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la 6 la Jumuiya ya Afrika Mashariki la Usafiri wa Anga lenye kauli mbiu “Mustakabali wa Usafiri wa Anga: Kudumisha Mifumo ya Usafiri wa Anga yenye Ustahimilivu, Uendelevu, Ubunifu na Usalama".

Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bodi ya Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC CASSOA) kwa kuipa nafasi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuandaa Kongamano la 6 la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Wageni Waalikwa na Washiriki wa Kongamano

Kama inavyofahamika moja ya malengo ya CASSOA ni kusaidia Nchi Wanachama katika kutimiza majukumu yao ya udhibiti wa usalama chini ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mkataba wa Chicago. Kwa hakika, uandaaji wa Kongamano hili, na ushiriki wenu hapa, ni utekelezaji wa malengo ya Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Napenda nikupongezeni sana kwa kuwa makini katika kuhakikisha mnayafanikisha na kuyatekeleza ipasavyo malengo ya Jumuiya hii.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua jukumu muhimu la CASSOA katika kuimarisha uwezo wa usimamizi wa usalama wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi yetu inaendelea kunufaika na uhusiano mzuri wa kufanya kazi na Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaozingatia dira ya pamoja na uelewa wa kina kwa madhumuni ya usalama wa anga na kwa maendeleo ya Mataifa yetu.

Wageni Waalikwa na Washiriki wa Kongamano

Utalii ni muhimu kwa mikakati ya maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, na Usafiri wa Anga ndio kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi wetu. Katika kufikia malengo tuliyojiwekea katika utalii na biashara, tunatakiwa kusaidia ipasavyo sekta ya usafiri wa anga. Kwa maana hiyo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia mikataba yote ya usafiri wa anga ya kimataifa ili kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unaendelea kuwa salama. Nchi yetu inajivunia  mafanikio ambayo yamefikiwa katika sekta ya usafiri wa anga. Nachukua fursa hii kuwataka wadau na washirika wa usafiri wa anga kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua kwa usalama. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni kama ifuatavyo:

  1. Tanzania imeendelea kushirikiana na nchi washirika chini ya mwavuli wa Taasisi ya Udhibiti wa Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika kuoanisha kanuni za usafiri wa anga ndani ya ukanda wetu kwa lengo la kuwianisha taratibu, kuimarisha usalama, na kuongeza ufanisi. Ni dhahiri kwamba tumefikia hatua kubwa katika juhudi zetu za kuoanisha kanuni. Hata hivyo, tusipuuze changamoto zinazoendelea kama vile tofauti za kanuni na utekelezaji wake. Changamoto hizi zinahitaji umakini wetu wa pamoja na hatua za pamoja ili kuzishinda.
  2. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata asilimia 87 katika kuhakikisha usalama na ufanisi  katika Mpango wa Kimataifa wa Ukaguzi wa Usalama wa Kimataifa (Universal Security Audit Programme Continuous Monitoring Approach -USAP-CMA) uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) mwaka jana. Lengo la ukaguzi huu ni kukuza usalama wa usafiri wa anga duniani kupitia ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa utendaji wa usalama wa anga wa Nchi Wanachama.
  3. Ni uboreshaji wa mradi wa Masafa ya Mbali (VHF) unaojumuisha piaufungaji wa vituo 18 vipya na redio katika Viwanja vya Ndege 12, na uwekaji wa mifumo ya kinasa sauti katika viwanja vinne vya ndege. Uwekaji wa Mfumo wa Kutua kwa ndege (ILS) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume ni ushahidi wa wazi kuhusu nia yetu ya kufanya usafiri wa anga kuwa salama na hivyo kuwa mwezeshaji wa sekta ya utalii ambayo, kama nilivyosema awali, ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Wageni Waalikwa na Washiriki wa Kongamano

Napenda pia kuelezea hatua iliyofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukidhi ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga kwa kutekeleza miradi kadhaa kama ifuatavyo:

  1. Kukamilika mradi wa ujenzi wa  jengo jipya la abiria (Terminal 3) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Jengo hili sasa linafanya kazi kikamilifu na limewezesha kupatikana kwa ufanisi mkubwa wa huduma za usafiri wa anga hapa Zanzibar tokea kuanza kutumika kwake.
  2. Kuanza ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal 2) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Jengo la sasa liliopo lilijengwa mwaka 1974 na hivyo linahitaji marekebisho makubwa. Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa jengo jipya lenye ukubwa wa mita za mraba 16,000 na lenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 1,300,000 kwa mwaka. Ujenzi huo utaenda sambamba na ujenzi wa sehemu ya kuegesha magari yenye uwezo wa kuhudumia magari 200 kwa wakati mmoja. Kazi ya ujenzi ilianza Januari, 2024 na inatarajiwa kumalizika katika muda wa miezi 18.
  3. Mradi wa ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa jengo la zamani la (Terminal 1) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Jengo hili lilijengwa miaka ya 1950. Mpango wetu ni kuliboresha kwa viwango vya kimataifa ili liweze kutuongezea uwezo wa kuhudumia mahitaji yanayoongezeka ya umma.
  4. Mradi wa ujenzi wa Kituo cha biashara katika Jengo la Tatu la Abiria kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa lengo la kuboresha huduma za biashara katika uwanja wa ndege wa kimataifa na kulingana
  5.  na ongezeko kubwa la uhitaji wa maeneo ya biashara na ofisi, Serikali imeanza kazi ya ujenzi wa kituo kikubwa cha biashara kitakachojumuisha maduka, migahawa, huduma za kibenki na ofisi.
  6. Mradi wa ujenzi wa mradi wa eneo la kuhifadhi na kusafirisha chakula (Logistic center) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Serikali imeanza kazi ya ujenzi wa kituo cha kuhifadhia chakula na vifaa. “Logistic Centre” inayojengwa ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa ajili ya kuhifadhi na kusafirisha mizigo hasa vyakula vinavyoharibika haraka.
  7. Mradi wa ujenzi wa vituo vipya vya kutolea huduma za mafuta ya anga (fuel farm) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume. Kama mnavyofahamu Uwanja huu wa ndege wa AAKIA kwa sasa una kituo kimoja cha huduma ya mafuta ya ndege. Serikali imeamua kuongeza vituo vingine vitatu kwa  kuruhusu ushindani wa utoaji huduma ili kupata  unafuu wa bei kwa mashirika ya ndege na walaji kwa ujumla. Katika kufanikisha hili, Serikali imeingia mikataba na makampuni yafuatayo:
  8. Oilcom
  9.  GBP
  10. Lake Oil
  11. Mradi wa ujenzi na upanuzi wa Kiwanja cha ndege cha Pemba unaojumuisha upanuzi wa urefu wa njia ya kurukia ndege kutoka mita 1,525 hadi mita 2,510, ujenzi wa maegesho ya ndege (apron) yenye uwezo wa kuchukua ndege 2 kubwa aina ya Code C (B 737-800) na 8 ndege ndogo Code B na ujenzi wa jengo jipya la abiria lenye ukubwa wa mita za mraba 9,170. Mradi huo pia unajumuisha ujenzi wa maegesho ya magari, eneo la biashara, na jengo jipya la kuongozea ndege. Mradi huu unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
  12. Mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nungwi unaolenga kuhudumia zaidi shughuli za utalii zinazoongezeka hapa Zanzibar

Wageni Waalikwa na Washiriki wa Kongamano

Katika Kongamano la 5 la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki, lililofanyika Bujumbura, Burundi kuanzia tarehe 27 hadi 28 Februari 2020 lilikuwa ni fursa muhimu kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Wadau wa Usafiri wa Anga kuweza  kujadili masuala yanayohusu Usalama wa Anga katika Kanda yetu na Dunia kwa ujumla. Hivyo pamoja na mambo mengine, Kongamano hili la 6  litoe  fursa ya kutathmini  utekelezaji wa maazimio ya Kongamano  lile na kuunganisha na mada mpya za Kongamano na hili la 6. Nimefurahi kuona  kuwa katika Mpango wa Kongamano la 6 la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki, zipo mada mbalimbali zinazohusiana na usalama, mfumo wa udhibiti, ulinzi wa mazingira na teknolojia kwa lengo  la kuongeza ufanisi katika usafiri wa anga katika mataifa yetu.

Napenda kuwahimiza washiriki wote wa Kongamano hili kujadili na kutoa mapendekezo sio tu jinsi changamoto zilizoainishwa katika maeneo hayo zinavyoweza kutatuliwa, bali pia kubainisha jinsi fursa zinazohusiana na maeneo hayo zinavyoweza kutumika kikamilifu kwa manufaa ya usalama wa anga, uwezo, ufanisi na ulinzi wa mazingira katika Ukanda wa nchi zetu za  Afrika Mashariki.

Wageni Waalikwa na Washiriki wa Kongamano

Pamoja na  kubanwa na ratiba ya Kongamano, napenda kuwahimiza kutafuta muda ili kutembelea vivutio mbali mbali vilivyopo hapa Zanzibar. Nchi yetu imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii, ikiwa ni pamoja Mji Mkongwe, fukwe za kuvutia, majengo ya kihistoria na mambo mbali mbali ya kiutamaduni ambayo mtayafurahia na kuwapa kumbukumbu nzuri ya kuwepo kwenu hapa Zanzibar.  Wenyeji wenu kwa kushirikiana na Maafisa wetu kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar watafurahi kuwasaidia katika mipango yenu ya matembezi ya maeneo ya utalii. Tafadhali msiache kuitumia fursa hio sambamba na Kongamano hili.

Namalizia hotuba yangu kwa kutoa shukurani zangu tena kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano hili. Napenda  kuwatambua na kuwashukuru washirika wote ambao kwa njia moja au nyingine wameunga mkono katika kufanikisha  tukio hili. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia nyote ushirikiano wa karibu kwa manufaa ya sekta ya usafiri wa anga katika ukanda wetu na kwingineko. Nakutakieni nyote ushiriki mwema na mafanikio katika Kongamano letu hili.

Baada ya kusema hayo, nachukua fursa hii kutangaza kuwa  Kongamano la 6 la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa kuwa limefunguliwa rasmi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza