HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA WAFANYAKAZI DUNIANI (MEI MOSI) KATIKA UWANJA WA GOMBANI MKOA WA KUSINI PEMBA 

TAREHE: 01 MEI,2024

Mheshimiwa Sharifu Ali Sharifu; 

Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Kazi, 

Uchumi na Uwekezaji,

Waheshimiwa Mawaziri na  Manaibu Mawaziri Mliopo,

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi,

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba,

Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, 

Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,

Ndugu Katibu Mkuu Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Makatibu Wakuu nyote Mliopo,

Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kusini Pemba,

Katibu Mkuu Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi – Zanzibar,

Ndugu Maafisa Wadhamini,

Ndugu Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Serikali,

Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO),

Mkurugenzi Mtendaji – Jumuiya ya Waajiri Zanzibar,

Ndugu Viongozi wa Dini na Vyama vya sSiasa,

Ndugu Wafanyakazi Wenzangu,

Ndugu Waandishi wa Habari,

Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana,

ASSALAAM ALEIKUM,

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa rehema kwa kutujaaliya uhai na afya njema na kutuwezesha kujumuika kwa wingi, katika kilele cha Maadhimisho ya siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani – Mei Mosi ambayo huadhimishwa kila mwaka katika tarehe kama hii.

Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru viongozi na watendaji wa Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji kwa ushirikiano na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa maandalizi mazuri ya Maadhimisho haya.

Aidha, natoa shukrani kwa Uongozi wa Mkoa wa Kusini Pemba, wenyeji wetu kwa kufanya maandalizi mazuri ya Maadhimisho haya mwaka huu ambayo kwa hakika yamefana sana. Kwa dhati kabisa nalishukuru Shirika la Kazi Diniani (ILO) kwa kuwa pamoja nasi leo hii na kwa hatua yake ya kuendelea kushirikiana na kuisaidia Zanzibar kwa mambo mbali mbali yenye kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.  Shukrani za kipekee napenda kuzitoa kwenu nyinyi Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi nyote mliohudhuria katika maadhimisho haya pamoja na wale ambao wanatufuatilia kupitia vyombo mbali mbali vya habari

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Nafarijika kuungana na Wafanyakazi kwa mara ya nne mfululizo katika siku hii ya Mei Mosi tangu nilipochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nimefahamishwa kwamba sherehe hizi hapa Pemba zilifanyika miaka mitatu iliyopita kabla ya Serikali ya Awamu ya Nane. Kwa hakika, Maadhimisho haya ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwangu ni fursa adhimu sana ya kujumuika na wafanyakazi wa sekta za umma na sekta binafsi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema: “Kuimarika kwa Maslahi na Mazingira ya kazi ni msingi wa ufanisi kazini”. Nakubaliana na kauli mbiu hii ya Maadhimisho ya mwaka huu kwa kuzingatia kuwa Serikali imeweka kipaumbele cha kuimarisha mazingira na maslahi ya Wafayakazi wote kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi na kuchochea kasi ya maendeleo nchini.

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Serikali inaendelea kukuhimizeni kuheshimu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya haki za binaadamu na utawala bora. Tunaamini kuwa iwapo wafanyakazi watazingatia misingi hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwatumikia wananchi, ni wazi kuwa ufanisi katika kazi utaongezeka. Serikali kwa upande wake itazidi kuhakikisha mazingira ya kazi pamoja na maslahi yanaimarika ili kuongeza ufanisi kazini. Tunajivunia mafaniko ambayo Serikali imeendelea kuyapata katika kuimarisha haki za wafanyakazi, kuongeza fursa za ajira pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Katika kipindi cha  miaka mitano  Serikali imejipangia kutengeneza ajira 300,000 kwa wananchi wake kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025. Katika kipindi cha miaka mitatu, Serikali kupitia shughuli mbali mbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea zikiwemo ujenzi wa barabara, Skuli, vituo vya afya  na hospitali, bandari, miundombinu ya maji, umeme  na shughuli nyenginezo, imepelekea kupatikana kwa ajira mpya zipatazo laki moja na themanini na saba elfu, mia sita na hamsini na moja (187,651) sawa na asilimia 104 ya lengo la ajira 180,000 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.  

Aidha, Serikali imeimarisha upatikanaji wa ajira nje ya nchi ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa mashirikiano na nchi ya Qatar, Saudia na ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba na Oman. Upatikanaji wa ajira za nje umeongezeka kwa asilimia 35 kutoka ajira 1,080 kwa mwaka 2022/2023 hadi ajira 3,078 kwa mwaka 2023/2024. Kwa upande wa ajira za ndani umeongezeka kwa asilimia 65.9 kupitia mikataba iliyothibitishwa kutoka ajira 6,348 mwaka 2022/2023 hadi 9,630 kwa mwaka 2023/2024. Kwa upande wa Serikali kuu jumla ya ajira 6,735 zimetolewa kwa ajili ya watumishi wapya wa umma katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Sekta ya uwekezaji ni miongoni mwa chanzo cha upatikanaji wa ajira za ndani ya nchi. Sekta hii imezidi kuimarika. Kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 jumla ya miradi mipya 63 imesajiliwa yenye thamani ya Dola za Kimarekani 1,499 Milioni na inatarajia kutoa ajira zipatazo 4,392. Aidha, Serikali imetoa TZS. Bilioni 15 kwa ajili ya program ya Inuka yenye lengo la kutoa mikopo kwa wajasiriamali.

Programu hii hadi sasa imeshatoa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 22.4. Ongezeko la thamani la mikopo hiyo limetokana na fedha za marejesho ambazo zinaendelea kutolewa mikopo mipya (Revolving Fund). Mikopo hiyo imewezesha kuzalisha ajira za moja kwa moja (direct employment) kwa Wananchi 43,360. Aidha, programu ya Khalifa Fund imetoa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 2.10 kwa miradi 18 na kuwanufaisha wananchi 19,373 ambao wameweza kujiajiri na kuajiriwa. Kadhalika, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi jumla ya TZS Milioni 852.17 zimetolewa kwa wananchi. Fedha hizi zinatokana na makusanyo kutoka Halmashauri za Wilaya.

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Kwa lengo la kuhakikisha wananchi hususani wafanyakazi wanapata huduma bora za afya pamoja na familia zao, Serikali imetunga sheria iliyoanzisha mfuko wa Bima ya afya Zanzibar.  Hadi kufikia mwezi Aprili, 2024 jumla ya wanachama 48,929 na wategemezi wao wapatao 187,641 wamesajiliwa katika Bima ya Afya Zanzibar. Idadi hiyo inafanya jumla ya wanufaika wa huduma za afya kupitia ZHSF kufikia wanachama 236,570. Hivi sasa, watumishi wa Umma wanaendelea kupata huduma za matibabu kupitia vituo vya afya na hospitali mbali mbali za Zanzibar kuanzia mwezi Oktoba mwaka jana (2023). 

Hatua zinazoendelea sasa ni za usajili wa wafanyakazi wa sekta binafsi ili nao pia waweze kunufaika katika kupata huduma hizo za Bima ya afya na tunatarajia kuanza kutoa huduma hiyo mnamo mwezi Julai mwaka huu wa 2024. Hatua hii itafikia malengo ya kuwapa ulinzi na kinga wafanyakazi dhidi ya majanga ya ajali, maradhi na vifo vinavyotokana na kazi.

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) imetekeleza ahadi niliyoitoa Mwaka 2022, katika sherehe za Mei Mosi kwamba tutatoa mafao mawili mapya kwa ajili ya wanachama wake wakiwemo wafanyakazi wa sekta zote. Mafao hayo ni Fao la Kuumia kazini na Fao la upotevu wa ajira. Napenda niwaarifu wafanyakazi kwamba ahadi hiyo imeanza kutekelezwa na sasa ZSSF wameanza kutoa mafao hayo. 

Aidha, mwaka jana katika Maadhimisho ya Mei Mosi yaliyofanyika  Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, tuliahidi kupandisha kima cha chini na pensheni kwa wastaafu wanaopokea pensheni chini ya TZS. 180,000. Ahadi hiyo tumefanikiwa kuitekeleza katika Serikali na pia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) umeanza kuwalipa wastaafu wote kima cha chini cha pensheni kuanzia 180,000.

Kadhalika, kwa kuzingatia kuwa wafanyakazi wanaostaafu kwa hiari wakiwa na umri wa miaka 55 wanapata kiinua mgongo pungufu tofauti na wale wanaopokea wakistaafu kwa lazima wakiwa na umri wa miaka 60, Serikali tayari imeshaiagiza ZSSF kufanya tathmini juu ya hili ili wafanyakazi wanaostaafu kwa hiari wakiwa na miaka 55 wapate kiinua mgongo bila upungufu.

Kwa madhumuni ya kuimarisha hifadhi ya jamii wakiwemo wafanyakazi, Serikali imefanya uamuzi wa kutoa mafao 8 kati ya mafao 9 yanayotambulika na Shirika la kazi Duniani ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao pindi wanapopatwa na maafa, maradhi ama kukosa ajira. Kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Serikali itatoa mafao  yafuatayo:

 1. Mafao ya Kukosa Ajira (Unemploymentbenefit).
 2. Mafao ya Uzee (Old Age Benefit).
 3. Mafao ya Watakaopata Ajali Kazini (Employment Injury Benefit).
 4. Mafao ya Uzazi (Maternity Benefit).
 5. Mafao ya Ulemavu (invalidity benefit)na
 6. Mafao ya warithi (survivorbenefit).

Mafao mengine yatakayotolewa na Serikali kupitia Taasisi nyengine ni mafao ya matibabu na mafao ya ugonjwa. Aidha, Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha kituo maalum cha utoaji wa huduma za afya kwa wafanyakazi nchini. Hatua hii itakuwa na mchango muhimu katika kuhakikisha wafanyakazi wanapewa fursa maalum kwa ajili ya kuwapatia huduma za afya.

 Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Kwa lengo la kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa taarifa, Serikali imeanzisha mifumo mbali mbali katika taasisi zake. Miongoni mwao ni Mfumo wa Tehema wa Serikali e-government unaotumika katika taasisi zetu kwa shughuli za kiutendaji zote na  Mfumo wa ununuzi wa vifaa, mali na utoaji wa huduma mbali mbali ambao umeweza kuwapa nafasi wafanyabiashara wote walioko Zanzibar waliosajiliwa kisheria na kuweza kuuza bidhaa zao kihalali bila upendeleo kwa kutumia mfumo wa manunuzi (e-procurement). 

Mfumo mwengine ni Sema na Rais (SNR) wenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wakiwemo wafanyakazi wa Taasisi mbali mbali za umma na binafsi. Kupitia mfumo huu, jumla ya malalamiko 1,903 ya wafanyakazi yamepatiwa ufumbuzi. Sawa na asilimia 97 ya malalamiko yaliyowasilishwa yakihusisha madai ya posho, marekebisho ya mishahara na mafano ya kiinua mgongo. Jumla ya TZS. Bilioni 3.9 zimetumika kulipa stahiki hizo. Aidha, jumla ya malalamiko 224 yamewasilishwa na wafanyakazi wa sekta binafsi ambapo asilimia 88 kati yao yamepatiwa ufumbuzi. Malalamiko hayo yakihusisha madai ya mishahara, fedha za ZSSF, fidia, wafanyakazi kutokupatiwa mikataba na kutokufuatwa sheria, kanuni na miongozo ya ajira. 

Napenda kutumia fursa hii kwa kutoa rai kwa wafanyakazi kuendelea kutumia mifumo iliyopo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yenu, na vile vile kuwasilisha changamoto zinazohusiana upatikanaji wa haki na stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, nasisitiza sekta binafsi kuzingatia haki za watumishi zikiwemo kuwapatia mikataba, kuwasilisha makato yao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii pamoja na kuwapatia watumishi stahiki zao kwa mujibu wa sheria na mikataba ya kazi. 

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Kwa lengo la kuweka mazingira bora ya kazi na kuhakikisha uwepo wa kazi za staha nchini na zenye heshima, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Shirika la kazi duniani (ILO), tumeweza kupiga hatua katika kuweka viwango vya kazi nchini kwa kuzingatia miongozo ya Mikataba ya Kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO). Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesharidhia mikataba 37 ya kazi.

Hivi sasa Serikali inaendelea na hatua za kuangalia uwezekano wa kuridhia na kusaini mikataba 6 mipya ya kazi ikiwemo mkataba wa kulinda haki za Wafanyakazi wa majumbani, Mkataba wa Hifadhi ya Jamii, Mkataba wa Sera ya Ajira, Mikataba miwili inayohusu Usalama na Afya kazini pamoja na Mkataba wa kinga kwa wanaopata majanga ya ajali, maradhi na vifo katika kazi. Kusainiwa kwa mikataba hii kutaweka mazingira mazuri zaidi ya kazi na kuimarisha utoaji wa maslahi mazuri 

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Kwa madhumini ya kuimarisha mazingira bora ya Wafanyakazi hapa Zanzibar, Serikali imekuwa ikiendelea kuangalia maslahi mbali mbali ya kazi ikiwemo mishahara, upandishwaji madaraja, nyongeza za mwaka, maposho, fidia, nauli kwa wenye kustahiki pamoja na matibabu. 

Napenda niwahakikishie kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendelea kuimarisha mazingira ya kazi na utoaji wa maslahi bora kwa wafanyakazi. Katika utekelezaji wa dhamira hiyo, Serikali itachukuwa hatua, kuanza kutoa Posho la nauli za kwenda kazini na kurudi nyumbani ya TZS. 50,000 kwa watumishi wote wanaostahiki kulipwa posho. Jumla ya TZS. 34,099,500,000  zimetengwa na Serikali kwa ajili ya posho la usafiri. Aidha, Serikali imedhamiria kuhakikisha inaongeza fedha kwa ajili ya posho ya likizo.  Jumla ya TZS. 2,523,814,700 zimetengwa na Serikali kwa ajili ya likizo katika bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Ni dhahiri kuwa, Serikali yenu ni sikivu na inaendelea kutoa maslahi na kuimarisha mazingira ya kazi kwa lengo la kuleta ufanisi na maendeleo ya nchi yetu. Aidha, Serikali haitosita kuzitatuwa changamoto za wafanyakazi na watu wote kwa kadri ya uwezo wake ili kulinda hadhi na heshima yao. Lengo ni kupata maslahi bora ya Utumishi na jamii kwa ujumla kwa kutoa huduma stahiki na kuinua uchumi wa nchi yetu. 

Kufuatilia changamoto 5 zilizowasilishwa katika sherehe za Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka jana 2023, yaliyofanyika Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja, napenda kutoa maelezo ya utekelezaji wa hoja hizo kama ifuatavyo:-

 1. Kuhusu malimbikizo ya mishahara kwa Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA). Utaratibu umeshafanywa ya kuyahakiki madeni hayo na yameshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya malipo yatakayoanza kufanywa mwezi wa Juni mwaka huu.
 2. Kuhusu madeni ya kazi ya muda wa ziada kwa wafanyakazi wa Wakala wa Serikali Uchapaji Zanzibar. Hatua za uhakiki wa madeni zimefanywa kwa ushirikiano na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, ili Serikali iweze kuchukua hatua stahiki hasa baada ya kubainika kuwepo baadhi ya makosa katika madai yaliyowasilishwa. Katika suala hili, hivi karibuni Wakala wataanza kulipa kwa awamu ya kwanza.
 3. Kuhusu madeni ya nauli kwa wanaofanya kazi maeneo ya mbali hususani Walimu, hali ambayo imejitokeza baada ya kuondoshwa kwa ugatuzi 2021. Tayari hatua ya ulipaji wa madeni hayo ya nauli yameshaanza kwa Walimu wa Skuli za Msingi. Karibuni, watalipwa Walimu wa Skuli za Sekondari ili kukamilisha deni hilo kwa wote wanaostahiki.
 4. Kuhusu kipato cha kukatwa kodi nyingi kwenye mishahara, kiinua mgogo na pencheni. Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji imefanya ufuatiliaji wa hoja hii na kubaini kuwa ipo kwa mujibu wa sheria na kanuni za fedha ziliopo. Hata hivyo, Serikali kupitia taasisi zinazohusika zimepokea hoja hii na zinaiwekea mazingatio.
 5. Hoja ya kuwepo kwa wafanyakazi wa mkataba wa muda mfupi katika Mabaraza ya Manispaa, Miji na Halmashauri. Tayari suala hili limejadiliwa kupitia vikao vya pamoja na taasisi husika ili kulipatia ufumbuzi, Serikali imezitaka taasisi zinazohusika kurekebisha kasoro zilizopo kwa kufuata kwa sheria za kazi. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora umezingatia hoja hiyo na wapo katika hatua ya kusubiri kupatikana kwa muundo wa taasisi za Serikali za Mitaa ili kuwapanga watumishi hao kwa mujibu wa mahitaji.

Ndugu Wafanyakazi na ndugu Wananchi,

Kwa lengo la kuzidi kupata mafanikio katika nchi yetu, napenda kuhimiza kuwa tuendelee kudumisha amani, utulivu, maelewano na mshikamano katika sehemu zetu za kazi. Tufanye kazi kwa bidii na juhudi kwa pamoja ili kuimarisha maendeleo ya uchumi wetu na kuimarisha ustawi wa jamii. Aidha, kwa kuzingatia kuwa “Haki na Wajibu ni watoto pacha”. Nawahimiza watumishi wenzangu  tuache uzembe, tusifanye kazi kwa mazowea, tujiepushe na rushwa na ubadhirifu ili uchumi wetu ukuwe zaidi. Lengo Taifa letu linufaike na wananchi waendelee kupata huduma bora. Aidha, ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa wananchi wote, wafanyakazi wakiwa ni sehemu ya wananchi wananufaika na fursa ziliopo katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na maslahi mapana ya maisha yao na familia zao kwa ujumla.