Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk Hussein Ali Mwinyi katika uzinduzi wa Duru ya kwanza ya utoaji wa Vitalu kwa Kampuni kwa Maeneo ya Baharini Katika Hoteli Ya Golden Tulip, Zanzibar

TAREHE : 20 MACHI, 2024

Mheshimiwa Othman Masoud Othaman; 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla; 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid; 
Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Mheshimiwa Khamis Ramadhan Abdallah; 
Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Mheshimiwa Shaaban Ali Othman; 
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi,

Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya 
Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania,

Mhandisi Zena Ahmed Said, 
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,

Mheshimiwa Dkt Mohammed Said Mohammed; 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,

Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali ya 
Mapinduzi ya Zanzibar na  Serikali ya 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Waheshimiwa Mabalozi,

Wawakilishi kutoka Sekta ya Mafuta na Gesi,

Mwakilishi kutoka SLB na Frontier

Ndugu Wageni Waalikwa,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana

Assalam Aleikum
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujaalia neema ya uhai na afya njema na kutuwezesha kuhudhuria hafla hii yenye lengo la kuwakaribisha wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi Asilia hapa Zanzibar. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi na wadau wote waliohusika kwa maandalizi ya shughuli hii na kwa kunialika kuwa mgeni Rasmi. Aidha, nawashukuru watu wote mliokuja kushuhudia tukio hili la kihistoria la kuzindua Duru ya kwanza la Utoaji wa vitalu kwa maeneo ya baharini kwa Zanzibar.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Shughuli za utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa upande wa Zanzibar, zilianza miaka ya 1950 wakati Kampuni ya British Petroleum (BP) kwa kushirikiana na Kampuni ya Shell zilipofanya uchunguzi wa kina na kuchimba visima viwili kwa pande zote mbili za visiwa vya Zanzibar. Shughuli hizo zilikamilika mwaka 1963 na kutoa msingi mkubwa katika kuendeleza shughuli za Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar.

Baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania mwaka 1964, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi zilikua chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo la Petrolii Tanzania (TPDC). Tafiti mbali mbali zilifanyika kwa upande wa nchi kavu na baharini mwa Zanzibar na kupelekea kupatikana kwa vitalu vya Pemba – Zanzibar na Vitalu nambari 6 hadi 12 na Latham.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Hatua mpya ya maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi Zanzibar ilianzishwa mwaka 2015 kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Petroli Na 21 ya mwaka 2015 ya Tanzania iliyoiruhusu kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia shughuli za Mafuta na Gesi Asilia wenyewe. Kwa mantiki hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliandaa Sera ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016 pamoja na Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2016. Sheria hiyo ya mwaka 2016, ilianzisha taasisi za usimamizi wa shughuli za Utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ambazo zilifanyika kati ya 2017 na 2019. Matokeo ya shughuli hizo yameonesha kuwepo kwa miamba na viashiria  vyenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia hapa Zanzibar.

Baada ya hatua hiyo, sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kutekeleza sera ya Uchumi wa Buluu, sekta ya mafuta na gesi imewekwa miongomi mwa maeneo makuu ya kipaumbele katika Sera ya Uchumi wa Buluu.  Dhamira ya Serikali katika uchumi wa buluu ni kuimarisha uchumi wa nchi kwa haraka na kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu ya vyanzo vya nishati ya uhakika. Serikali inaamini kuwa Uchumi wa Buluu unafursa nyingi za kukuza mipango ya maendeleo ya kiuchumi yenye lengo la kupunguza umaskini na kutengeneza fursa za ajira nchini.

Ndugu Wananchi na Wageni Waalikwa,
Katika utekelezaji wa dhana ya Uchumi wa Buluu, Serikali inatoa fursa kubwa kwa wawekezaji wa sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ili kuwa na mazingira rafiki ya utekelezaji wa shughuli hizo. Ikumbukwe kuwa, eneo letu la Zanzibar limepata sifa ya kutambulika kuwa ni mahali pazuri kwa makampuni kuwekeza na palipo salama. Katika dhamira yetu ya kuzindua duru ya kwanza ya utoaji wa Vitalu, Serikali imefanya mapitio ya mifumo ya kisheria na kimkataba ya Mafuta na Gesi Asilia ili kuvutia uwekezaji, iliolenga kuimarisha masharti ya fedha ili kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi Asilia hapa Zanzibar.

Matarajio yangu ni kuwa, uzinduzi huu tunaoufanya leo wa Duru ya kwanza utasababisha kufungua na kuharakisha shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika vitalu hivyo vipya vya baharini na hatimae kuitangaza Zanzibar kuwa sehemu ya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia. Napenda kuwahakikishia wawekezaji wote wa sekta ya mafuta na gesi na sekta nyengine za uchumi kwamba, Serikali iko tayari kuwahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji kwa manufaa yetu sote.