HOTUBA YA WAZIRI WA NCHI AFISI YA RAIS -IKULU MHESHIMIWA JAMAL KASSIM ALI
KUHUSU MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024
MEI, 2023
YALIYOMO
YALIYOMO i
ORODHA YA VIAMBATISHO ii
VIFUPISHO VYA MANENO iv
UTANGULIZI 1
MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU ZA AFISI YA RAIS – IKULU KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023 5
MAFANIKIO YA FUNGU A01 5
MAFANIKIO YA FUNGU A02 BARAZA LA MAPINDUZI 44
MWELEKEO WA BAJETI YA AFISI RAIS IKULU KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024 46
PROGRAMU KUU NA NDOGO NA MAKISIO YA FEDHA ZINAZOHITAJIKA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024 47
PROGRAMU KUBWA NA NDOGO ZA FUNGU A01 49
PROGRAMU KUBWA NA NDOGO ZA FUNGU A02 53
PROGRAMU KUBWA NA NDOGO ZA FUNGU A09 56
PROGRAMU KUBWA NA NDOGO ZA FUNGU A10. 58
MAMBO MAKUU YATAKAYOTEKELEZWA NA AFISI YA RAIS -IKULU KWA MIRADI YA MAENDELEO KWA MWAKA WA FEDHA WA 2023/2024 60
MAOMBI YA FEDHA YA KAZI ZILIZOPANGWA KUTEKELEZWA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024 61
HITIMISHO 61
ORODHA YA VIAMBATISHO
Kiambatisho 1. Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2023/2024 63
Kiambatisho 2. Malalamiko yaliyowasilishwa na Wananchi kwa Taasisi 59 za Serikali zilizounganishwa katika Mfumo wa Sema na Rais kwa Julai – Machi 2022/2023 70
Kiambatisho 3. Orodha ya Malalamiko yaliyowasilishwa na Wananchi kwa Kipindi cha Miezi 9 Julai - Machi 2022/2023
................................................................................ 74
Kiambatisho 4. Mchanganuo wa Takwimu za Malalamiko kwa Mwezi katika kipindi cha Julai – Machi 2022/2023 kupitia Mfumo wa Sema na Rais 75
Kiambatisho 5. Idadi ya Watumishi Waliopekuliwa kwa Wizara/Taasisi 90
Kiambatisho 6. Idadi ya Watumishi Waliopatiwa Mafunzo kwa Wizara/Taasisi. 93
Kiambatisho 7. Idadi ya Majengo ya Serikali yaliyofanyiwa Ukaguzi wa Kiusalama 94
Kiambatisho 8. Orodha ya Wizara, Idara na Taasisi zilizofanyiwa Ukaguzi kwa kipindi cha Julai-Machi, 2023 96 Kiambatisho 9. Idadi ya Watafiti wa Ndani na kutoka Nje ya Nchi walaiotembelea Taasisi ya Nyaraka na Kumbukumbu kwa kipindi cha Julai-Machi 2023 100
Kiambatisho 10. Wageni wa ndani ya Nchi 101
VIFUPISHO VYA MANENO
AfCFTA
African Continental Free Trade Area (Eneo huru la Biashara Barani Afrika)
AFD
Jumuiya ya Maendeleo ya Ufaransa
CCM
Chama cha Mapinduzi
EAC
East Africa Community (Jumuiya ya Afrika Mashariki)
GCC
Global Cooperation Committee
IORA
Indian Ocean Rim Association (Jumuiya ya Nchi zilizopakana na Bahari ya Hindi
JPC
Joint Permanent Commission (Tume ya kudumu ya Pamoja)
PDB
Presidential Delivery Beaureu
SADC
TADIO
Southern African Development Community (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika)
Tanzania Diaspora in Oman (Jumuiya ya Wanadiapora wa Tanzania Nchini Omani).
UNFPA
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu
UNHIF
Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya
WTTC
World Travel and Tourism Council Global Summit
ZACADIA
Jumuiya ya Wazanzibari Wanaoishi Nchini Canada (ZACADIA)
ZADEP
Zanzibar Development Plan
ZAWA
Mamlaka ya Maji (Zanzibar Water Authority)
ZBA
Wakala wa Ujenzi Zanzibar
ZBC
Shirika la Utangazaji Zanzibar (Zanzibar Broadcasting Corporation)
ZCTV
Zanzibar Cable Televishion
ZEMA
Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar
ZIPA
Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi Zanzibar
ZPDC
Zanzibar Petroleum Development company
ZPRA
Zanzibar Petroleum Regulatory Authority
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwa Baraza lako tukufu kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya Afisi ya Rais–Ikulu kwa kazi za kawaida na Maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujaalia mazingira ya amani na utulivu ambayo yametupa nguvu, mshikamano na imani ya kuendelea kumsaidia Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutekeleza majukumu ya kuongoza Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kumshukuru Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuendelea kuniamini kusimamia Afisi ya Rais–Ikulu Zanzibar. Vile vile namshukuru Mheshimiwa Rais kwa safu nzuri ya Watendaji wa Afisi yangu ambao amewaidhinisha.
Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii, kumpongeza Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kutimiza miaka miwili (2) na kupata mafanikio makubwa ya utendaji wa kazi yanayoonekana katika sekta mbali mbali nchini. Aidha kipekee nampongeza kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Zanzibar. Mheshimiwa Rais wetu amedhihirisha kuwa yeye ni kiongozi bora, muadilifu, mzalendo, mchapa kazi, mpenda mashirikiano na mwenye nia ya kweli katika kuleta maendeleo nchini.
Mheshimwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake bora, uliojaa uzalendo na maono ambao umechochea kuimarika kwa diplomasia hususani diplomasia ya uchumi baina ya nchi yetu na nchi yengine na mashirika ya kimataifa
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Othman Masoud Othman Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mhe Hemed Suleiman Abdallah Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kufanikisha majukumu yake ya kuiletea nchi yetu maendeleo.
Mheshimiwa Spika, naomba pia kuwapongeza Mawaziri wenzangu wote wa Serikali ya Awamu ya nane kwa kuendelea kupewa nafasi ya kuwatumikia Wananchi na kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mhandisi Zena Ahmed Said, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi kwa kazi nzuri anazozifanya katika kutekeleza majukumu yanayoiwezesha Serikali kufikia malengo yake, ikiwa ni pamoja na kuwasimamia Makatibu Wakuu kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naishukuru Kamati ya Kudumu ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Machano Othman Said, Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini na Makamu wake Mheshimiwa Mtumwa Peya Yussuf, Mwakilishi wa Jimbo la Bumbwini, pamoja na Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano, maelekezo na ushauri mzuri wanao tupatia ambao umetuwezesha kuimarisha utendaji wetu wa kazi.
Mheshimiwa Spika, aidha, naishukuru Kamati ya Bajeti ya Baraza lako tukufu chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Abdullah Hussein Kombo Mwakilishi wa Jimbo la Mkoani pamoja na Makamu wake Mhe. Asha Abdallah Mussa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda pamoja na wajumbe wa kamati kwa michango na miongozo waliotupatia tulipopata bahati ya kuwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Uimarishaji wa Nyumba za Viongozi kwa mwaka 2022/2023 sambamba na kufanya ziara katika maeneo ya mradi.
Mheshimiwa Spika, naomba nikamilishe pongezi zangu kwa namna ya pekee kwako wewe binafsi Mhe. Spika, naibu wako na wenyeviti wa Baraza kwa kuendelea kuliongoza Baraza letu kwa umahiri na mafanikio makubwa. Pili wawakilishi wote kwa kazi nzuri wanazozifanya na ushirikiano wanaonipatia katika utekelezaji wa majukumu ya yangu. Tatu na mwisho napenda kuipongeza na kuishukuru familia yangu na wapiga kura wa jimbo la Magomeni ambao wameendelea kunipatia upendo, ushirikiano na uvumilivu mkubwa hata pale ninapokuwa nimebanwa na majukumu ya kitaifa nje ya Jimbo langu la uchaguzi. Naahidi kuendelea kushirikiana nanyi katika kuliletea maendeleo jimbo letu na nchi yetu kwa ujumla.
MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU ZA AFISI YA RAIS–IKULU KWA MWAKA WA FEDHA 2022/2023.
Mheshimiwa Spika, Afisi ya Rais-Ikulu, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilijipangia kutekeleza Programu Kuu sita (06) zenye jumla ya Programu ndogo kumi na tatu (13). Kiambatisho nambari 01 kinamaelezo ya ziada kuhusu Programu Kuu na Programu Ndogo.
MAFANIKIO YA FUNGU A01
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Fungu A01 lilitengewa jumla ya TZS. 15,101.6 Milioni. Kati ya hizo TZS. 6,463.9 Milioni kwa ajili ya Matumizi Mengineo na TZS. 4,637.6 Milioni kwa ajili ya Mishahara na TZS. 4,000.0 Milioni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 Fungu A01 liliingiziwa jumla TZS. 1,850.9 Milioni kwa Matumizi Mengineo ambazo ni sawa na asilimia 28.64 na TZS. 470.0 Milioni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambazo ni sawa na asilimia 12 ya bajeti iliyopangwa.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya utekelezaji wa Programu Kuu za Fungu A01 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 yako kama ifuatavyo:-
i.Programu Kuu ya Kusimamia na Kuratibu Shughuli na Huduma za Mheshimiwa Rais na Kuimarisha Mawasiliano Ikulu.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Programu hii iliidhinishiwa jumla ya TZS. 5,908.4 Milioni. Kati ya hizo TZS. 2,908.8 Milioni kwa ajili ya Matumizi Mengineo na TZS.2,999.5 Milioni kwa ajili ya Mishahara. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 programu hii iliingiziwa jumla ya TZS. 973.4 Milioni sawa na asilimia 33.46 kwa ajili ya Matumizi mengineo. Utekelezaji wa Programu ndogo katika Program kuu hii ni kama ifuatavyo:-
a.Programu Ndogo ya Kusimamia Huduma na Kuratibu Shughuli za Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, kupitia Programu Ndogo ya Kusimamia Huduma na Kuratibu Shughuli za Mheshimiwa Rais Afisi ya Rais-Ikulu imepata mafanikio yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, naomba kukuarifu kuwa utekelezaji wa Programu hii, umewawezesha watumishi wa Afisi ya Rais- Ikulu Zanzibar kufanikiwa kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika masuala ya Siasa, Uchumi, Jamii, Sheria, Diplomasia, Mawasiliano na Habari, Uhusiano wa Kikanda, Kimataifa na ushauri mwingine kwa lengo la kumsaidia Mheshimiwa Rais kufanya maamuzi sahihi. Aidha, ratiba za matukio ya kila siku zimeendelea kuandaliwa na kufuatwa kulingana na miongozo anayoitoa. Vile vile Afisi imefanikisha kwa ukamilifu jukumu la msingi la kumpatia huduma anazozihitaji Mheshimiwa Rais pamoja na familia yake.
Mheshimiwa Spika, kupitia utaratibu wa kupokea na kuwakirimu wageni wa ndani na nje ya nchi wanaofika Ikulu kuonana na kuzungumza na Mheshimiwa Rais. Afisi imefanikiwa kuimarisha mahusiano mazuri na nchi marafiki, mashirika ya kimataifa pamoja na wadau wengine wa maendeleo nchini. Kwa kipindi cha miezi tisa ya utekelezaji wa Programu hii, jumla ya wageni elfu moja mia sita na arubaini na tano (1,645) wa ndani na mia saba na hamsini (750) wa nje ya nchi waliweza kufika na kuonana na kuzungumza na Mhe. Rais kwa shughuli mbali mbali za kiserikali na kibinafsi. Aidha, Mhe. Rais katika kipindi hiki alikutana na Mabalozi na viongozi kutoka Mataifa mbali mbali na Jumuiya za Kimataifa waliofika Ikulu. Miongoni mwao ni Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo Mhe. Felex Tshisekedi, Balozi wa Japan Mhe. Misawa Yasushi, Balozi wa Kenya Mhe. Isaac Njenga. Wengine ni Balozi wa Sweden Mhe. Charlotta Ozaki Macias, Balozi wa Afrika Kusini Mhe. Noluthando Mayende Mapele na Balozi mdogo wa U.A.E Mhe. Saleh Ahmed Alhemeir.
Mheshimiwa spika, katika kipindi hiki Mhe. Rais ameweza kuonana na Wawekezaji wa Makampuni kutoka Mataifa mbali mbali duniani. Miongoni mwa Wawekezaji hao ni kutoka Korea, Kampuni ya Global Cooperation Committee (GCC) wakiongozwa na Mwenyekiti wao na Wawekezaji kutoka Uingereza na Uturuki ambao wote wameonesha nia ya kutaka kuwekeza Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, kwa nia ya kukuza na kuendeleza Diplomasia ya uchumi (Economic Diplomacy) kwa maslahi ya nchi na wananchi kwa ujumla. Afisi imefanikiwa kuratibu na kusimamia ziara mbili (02) nje ya nchi. Moja nchini Oman aliyoifanya mwezi Oktoba 2022. Kupitia ziara hii, Mhe. Rais amepata fursa ya kuwaelezea hali ya utulivu ilivyo Zanzibar na kuwaomba kuja kwa lengo la kuekeza. Ametumia ziara hiyo kuelezea vivutio vya uwekezaji vilivyopo Zanzibar kwa wafanya biashara wa Oman.
Mheshimiwa Spika, mambo muhimu yaliyohusishwa katika majadiliano kati ya Zanzibar na Oman ni pamoja na ushirikiano wa eneo la elimu, ujenzi wa kituo cha data, Uhifadhi wa nyaraka za historia na ukusanyaji wa ushuru kupitia mfumo wa mtandao. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitiliana saini na Serikali ya Omani juu ya Mashirikiano (MOU) kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Beit–El-ajaib lililopo Forodhani Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, ziara nyengine ni ya Riyadh nchini Saudi Arabia, ambayo Mhe. Rais Mwinyi alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la Kimataifa la World Travel and Tourism Council Global Summit (WTTC) lililojadili mustakabali mzima wa sekta ya Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ziara za ndani ya nchi, Afisi imefanikiwa kuratibu na kusimamia ziara ya Mhe. Rais katika Wilaya zote za Unguja na Pemba zilizofanyika kati ya tarehe 16 Julai hadi tarehe 28 Julai, 2022. Kupitia ziara hizo,Mhe. Rais alikagua na kuweka mawe ya msingi miradi 54 ya maendeleo ikiwemo ya Serikali 44 na ile ya Binafsi 10. Miongoni mwa miradi hiyo ni ile ya Ujenzi wa Skuli kwa Unguja na Pemba. Aidha, miradi mingine ni Mabanda ya Wajasiriamali Chumbuni na Pale Kiongele, ukaguzi wa mradi wa Hospitali ya Mkoa ya Lumumba na Hospitali ya Panga tupu. Kwa upande wa sekta binafsi Miradi iliyotembelewa na kuwekwa mawe ya msingi ni viwanja vya michezo vya Kisakasaka, Skuli ya Combrige Nyamanzi na Hoteli ya Palolo Matemwe.
Mheshimiwa spika, ziara hizi pia zilihusisha ufunguzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya Riu Jambo iliyopo Wilaya ya Kaskazini ‘A’, ufunguzi wa Tawi la CRDB Bank Wete Pemba, Mradi wa Umwagiliaji maji Kinyasini, Ukaguzi na ufunguzi wa miradi ya maji katika maeneo ya mjini na vijijini pamoja na kuweka mawe ya msingi katika miundombinu ya barabara. Sambamba na yote hayo, Mhe. Rais alitumia ziara hizi kusikiliza kero za wananchi zikiwemo za migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa spika, ziara hii imeweza kuleta mafanikio makubwa sana kwa kutatua changamoto mbali mbali zilizokua zinawakabili wananchi zikiwemo zile za huduma ya maji safi, miundombinu, umeme, afya na masuala ya ardhi.
Mheshimiwa Spika, Afisi imefanikiwa kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa ahadi na maagizo ya Mheshimiwa Rais katika sekta mbali mbali nchini. Jumla ya ahadi thalathini na nne (34) zimeweza kutekelezwa. Miongoni mwa ahadi hizo ni pamoja na kuwapatia wananchi wa maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba boti za uvuvi za kisasa 107 (Unguja boti 30 na Pemba boti 77), kuwapatia kompyuta mpakato “laptop” 1,000 wanafunzi wa Kidato cha nne na cha sita waliofaulu vizuri. Ahadi nyengine zilizotekelezwa ni kufanya matengenezo ya Msikiti wa Forodhani, kushughulikia maslahi ya wafanyakazi wa kawaida wa Tume ya Maadili ya Viongozi Zanzibar ili walingane na taasisi zenye majukumu yanayofanana na taasisi yao pamoja na kuipatia tume hiyo watumishi wanne wa kada ya sheria ili kukidhi mahitaji.