RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuhimiza suala la kudumisha amani, umoja na mshikamano nchini.Al hajj Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo mara baada ya ibada ya sala ya Ijumaa Msikiti wa Mbuyuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, suala la kudumishwa amani nchini ndio chachu ya maendeleo na kuimarika kwa uhuru wa kufanya ibada.Alisema, uhuru wa kuabudu unachangiwa zaidi na kuwepo kwa utulivu wa amani na ushirikiano wa nchi na watu wake.Al hajj Dk. Mwinyi, alieleza, kuna mataifa kadhaa duniani hawana uhuru wa kufanyaibada kutokana na kuvurugika kwa amani za nchi zao ikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe na michafuko ya kisiasa.

Pia, Alhaj Dk. Mwinyi alihimiza suala la kudumisha ibada baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na kuiasa jamii ya kiislam kuendeleza utamaduni huo kwa miezi yote iliyobakia.Akizungumzia suala na kuuendeleza msikiti huo wa Mbuyuni, Alhaj Dk. Mwinyi aliwaahidi wananchi waumini wa kiislamu wa msikiti huo kwamba anaunga mkono jitihada za ujenzi wa msikiti na madrasa baada ya kupata maelekezo ya ujenzi huo kutoka Mamkala ya Hifadhi ya Mji Mkongwe nakueleza kuwa naye atakua miongoni mwa watakaojitolea kuchangia ujenzi wa msikiti huo.

Mapema akikhutubu kabla ya sala ya Ijumaa, Khatib wa sala hiyo Sheikh, Farid Hadi Ahmeid aliwasihi wananchi na waumini wa dini ya Kiislam kuendeleza ibada kama ilivyokua Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ili kuendelea kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alimtembelea Bibi Fatma Muhamed Hassan, Mjane wa aliekua Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Marehemu Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, na Mjane wa Marehemu Mzee Hafidh Suleiman,  bibi Mtumwa Hussein Farahan.Marehemu Mzee Hafidh Suleiman, alikua mmoja wa waasisi wa Mapinduzi, matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.