RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Baraza la Wauguzi na Wakunga la Zanzibar kusimamia vyema Sheria ya Baraza hilo sambamba na maadili kwa lengo la kuwahudumia vyema wananchi na kuzifanya huduma za afya zizidi kuimarika na kuendelea kuijengea sifa Zanzibar kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.

Dk. Shein, aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Wajumbe wa Baraza la Wauguzi na Wakunga waliofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais wakiwa wameongozana na uongozi wa Wizara ya Afya chini ya Waziri wa Wizara hiyo Mahmoud Thabit Kombo.Katika maelezo yake Dk. Shein aliwaeleza Wajumbe hao haja na umuhimu mkubwa wa kuipitia na kuisoma vyema vifungu vyote na hatimae kuifanyia kazi Sheria ya Baraza la Wauguzi na Wakunga la Zanzibar ya mwaka 2014 ili waweze kuliongoza vyema na kwa ufanisi zaidi Baraza hilo.Dk. Shein, alisema kuwa iwapo Sheria hiyo itasimamiwa vyema  fani ya Uuguzi itaendelea kuwa na mafanikio makubwa sana hapa Zanzibar.

Alieleza matumaini yake makubwa kwa wajumbe hao ambao wamechaguliwa kutokana na kuwa kazi hiyo wanaiweza na kuwapongeza kwa kufanya mambo mengi tokea kuzinduliwa Baraza hilo lenye Wajumbe 13 Mrajis na wasaidizi wake wawili mmoja Pemba na mmoja Unguja mnamo mwezi June mwaka 2015.Aidha, Dk. Shein alisisitiza suala zima la maadili ambalo ndio jambo muhimu katika fani yoyote duniani na kueleza kuwa katika fani ya Uuguzi suala la maadili ndio jambo la kulipa kipaumbele ili kuweza kutoa huduma nzuri ya afya kwa jamii.

Sambamba na hayo, Dk.Shein alieleza umuhimu wa kuwepo kwa usimamizi katika suala zima la uuguzi kwani hatua hiyo itaipelekea Zanzibar iweze kutajika na kuirudisha katika hali yake ya zamani ambapo wananchi kutoka ndani na nje ya Zanzibar walikuwa wakija hapa nchini kufuata huduma za afya.Akieleza suala zima la upungufu wa wauguzi, Dk. Shein alisema kuwa upungufu wa wauguzi ni suala la muda mrefu na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha inatatua changamoto hiyo hatua kwa hatua.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Baraza hilo kwa hatua yake ya kusimamia vyema suala la mafunzo kwa wauguzi ambapotayari kwa maelezo ya Wajumbe hao kuna wauguzi 893 wenye Diploma ya Uuguzi, 97 wenye Digirii ya Kwanza, 25 wenye Digrii ya Pili na 1 anaefanya Shahada ya Uzamivu (Phd) katika kada hiyo.Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa kada hiyo, Baraza lina kazi kubwa ya kuteua Kada muhimu za mafunzo katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) sambamba na wajibu mkubwa wa kusimamia utafiti.

Katika kutilia mkazo jambo hilo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wake imeamua kwa makusudi kuanzisha Taasisi ya Utafiti ya Afya kwa kutambua kuwa utafiti husaidia kutoa huduma bora za matibabu katika sekta ya afya.

Mapema Waziri wa Wizara ya Afya Mahamoud Thabit Kombo  alieleza kuwa mkutano kati ya Rais pamoja na Baraza hilo umekuja wakati muwafaka ambapo Wizara yake imeahidi mambo mbali mbali katika Baraza la Wawakilishi linaloendelea na kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Wizara na Baraza hilo yanaweza kutekeleza kile alichokiahidi katika Baraza hilo hivi karibu katika Bajeti yake.Waziri Kombo alieleza miongoni mwa changamoto ni pamoja na kuwekwa pembeni maadili ya uuguzi, lugha isiyofaa zidi ya wagonjwa, wagonjwa kutozwa fedha za dawa ambazo zipo hospitalini na zimenunuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili yao mambo ambayo ameahidi kuyavalia njuga katika kupambana nayo kwa mashirikiano na Baraza hilo.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja ya kujua mahitaji ya wauguzi pamoja na upangaji wa wauguzi katika hospitali za hapa nchini kwani licha ya kuwepo kwa idadi ndogo ya wauguzi lakini suala zima la usimamizi limekuwa likikosekana katika eneo hilo kama ilivyo kwa taasisi nyengine za Serikali.Dk.Abdulhamid alisisitiza kuwa licha ya Utumishi kufanya juhudi za makusudi katika sekta ya afya lakini kinachoonekana ni kuwa wengi wanaoajiriwa katika sekta hiyo hufanya kazi kinyume na ajira yao na ndipo unapotokea upungufu wa wafanyakazi huku akieleza kuwa ni vyema mafunzo yakawa yanaleta mabadiliko ya kiutendaji kwa watendaji wa kada hiyo ya Uuguzi pamoja na kada nyengine ndani ya taasisi za Serikali. 

Nae Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi Amina Abdulkadir Ali alitumia fursa hiyo kutoa historia kwa ufupi ya Baraza hilo hapa Zanzibar pamoja na hatua,utekelezaji na maendeleo ya kazi za Baraza sambamba na mafanikio na changamoto zilizopo.Akitaja miongoni wma mafanikio, Bi Amina aliseama kuwa ni pamoja na kupata ofisi na vitendea kazi, kuweza kufungua akaunti,kudumisha mashirikiano na Wauguzi wa Tanzania Bara pamoja na wale wa nchi za Afrika ya Mashariki na Jumuiya za Kimataifa.Aliongeza kuwa kuweza kuwachukulia hatua kwa onyo au kusimamisha kwa wauguzi waliokuwa na makosa ya maadili na kosa la kughushi vyeti, idadi ya wanafunzi wanaotaka kusoma Uuguzi imeweza kuongezeka ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita sambamba na kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani tarehe 12, Mei mwaka huu huko Pemba kwa pesa za Baraza kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bila ya kuwahusisha
wahisani.