RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi ameiomba Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China, kuangalia uwezekano wa kutuma Madaktari Bingwa katika nyanja mbali mbali, ili kwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuimarisha huduma za Afya kupitia Hospitali za Wilaya zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba.
Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu zanzibar katika hafla ya kuwaaga Madaktari 21 kutoka China, ambao walikuwepo nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoa huduma katika Hospitali mbali mbali Unguja na Pemba.
Amesema wakati huu Serikali ikikamilisha ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika Wilaya kumi na moja (11) za Unguja na Pemba, Hospitali ya Mkoa pamoja na Hospitali ya Rufaa Binguni, kuna umuhimu wa China kutuma madaktari bingwa katika nyanja mbali mbali, kupitia utaratibu huo wa kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya Hospitali hizo ili kuondokana na changamoto ya kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi.
Alisema Hospitali hizo za Wilaya, Mkoa na Hospitali ya Rufaa pale zitakapokamilika zitakuwa na vifaa na maeneo yote muhimu katika utoaji wa huduma, hivyo timu ijayo ya madaktari kutoka China itakuwa katika mazingira bora ya kufanya kazi.
Dk. Mwinyi aliipongeza Timu hiyo ya Madaktari wa Kichina kwa kazi kubwa waliyofanya wakiwa hapa nchini kwa kusaidia utoaji wa huduma za kinga, tiba, dawa pamoja na vifaa, sambamba na kufanya upasuaji wa magonjwa mbali mbali.
Aidha, aliwashukuru madaktari hao kwa kutoa mafunzo, pamoja na kuwajengea uzoefu Madaktari wazalendo, wauguzi na wafanyakazi wa sekta Afya.
Nae, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor alipongeza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya watu wa China na Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.
Alisema tangu mwaka 1964 kumekuwepo utaratibu kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutuma timu ya Madaktari hapa nchini kila mwaka, na akatumia fursa hiyo kuipongeza timu hiyo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutoa huduma bora katika jamii.
Alisema wakati wakiwa nchini, timu hiyo ilifanya kazi mbali mbali ikiwemo za upasuaji , kutoa ushauri pamoja na kutoa huduma za Afya katika Hospitali za Mnazi mmoja, Abdalla Mzee, Kivunge, Mkaunduchi na Chakechake.
“Timu hiyo haikuishia kufanya kazi katika Hsopitali kubwa pekee bali ilifika hadi katika Vituo vya Avya vilioko Vijijini, hatua hii ilibainisha ari kubwa waliyonayo madaktari hawa katika utendaji wao wa kazi uliotukuka”, alisema.
Alisema utendaji wao umeacha athari kubwa hapa nchini na utasaidia kuwajengea uzoefu madaktari wazalendo.
Mapema, kwa niaba ya Timu hiyo ya Madaktari kutoka China Dr. Son (Machano) alisema utaratibu wa China kutuma Madaktari hapa nchini uliasisiwa tangu mwaka 1964 kwa lengo la kujenga mashirkiano katika utatuzi wa changamoto za huduma za Afya, ikiwa ni hatua ya kuendeleza ushirikiano kati ya China na Zanzibar.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Dr. Marijani Msafiri Marijani , alisema timu hiyo ya Madaktari kutoka China wakati ikiwa nchini mbali na kutoa huduma katika Hospitali kubwa, pia ilipata fursa ya kufika maeneo ya vijijini na kutoa huduma za uchunguzi wa maradhi mbali mbali.
Huu ni mkupuo wa 31 kwa Timu ya Madaktari kutoka China kuja Zanzibar kwa ajili ya kutoa huduma za Afya, hii ikiwa ni timu ya 21, ambapo imehusisha madaktari katika fani mbali mbali, wakiwemo madaktari wa magonjwa ya Pua; Koo na masikio,meno pamoja na macho
Aidha katika timu hiyo pia kulikuwa na madaktari wa njia ya Mkojo, maradhi ya akinamama, mfumo wa njia ya chakula, moyo , Dawa za usingizi pamoja na mishipa ya fahamu.
Katika hafla hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alikabidhi Medali, Vyeti na zawadi kwa madaktari hao.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alikuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Chuo Kikuu cha Almustafa kutoka nchini Iran, ikulu Zanzibar.
Ujumbe huo ulioongozwa na Balozi wa Iran nchini Tanzania Hossein Alvandi Bahiney ulikutana na Rais Dk. Mwinyi ikiwa ni muendelezo wa mazungumzo kati ya Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian yaliofanyika Ikulu Zanzibar Agosti 26 mwaka huu, yakiwa na lengo la kukuza ushirikiano kati ya nchi mbili hizo kupitia sekta za Elimu, Afya, Sayansi na Teknolojia, Viwanda pamoja na Uchumi wa Buluu.
Katika mazungumzo hayo Rais wa Chuo Kikuu cha Almustafa Dk. Abass alibainisha azma ya Uongozi wa Chuo hicho kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kuanzisha tawi la chuo hicho hapa nchini.
Akizungumzia suala hilo, Rais Dk. Mwinyi aliishukuru Serikali ya Irani kwa hatua hiyo inayolenga kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya nchi mbili hizo.
Alitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa uharaka wake katika kuendeleza mazungumzo yalioasisiwa na Waziri Amir, wiki mbili zilizopita wakati viongozi hao walipokutana.
Aidha Dk. Mwinyi alibainisha utayari wa Serikali katika kushirikiana na Uongozi huo kuendeleeza sekta ya Elimu nchini.