RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameongoza mazishi ya marehemu Profesa Ishau Abdullah Khamis yaliyofanyika huko Donge, Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Viongozi mbali mbali wa vyama na serikali walihudhuria  akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd.

Mapema Alhaj Dk. Shein alifika kijijini kwa marehemu Profesa Ishau na kuipa pole familia ya marehemu na kuwaomba wawe na moyo wa subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba na baadae aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Profesa Ishau huko katika Msikiti wa Ijumaa  Donge Pangamaua.

Katika uhai wake marehemu Ishau aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Mbunge wa Jimbo la Kitope, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Utalii na Misitu, Katibu wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chuo cha Sayansi Jamii Chuo cha Kivukoni, Dar-es-Salaam, Mwalimu katika  Chuo cha Uchumi Dar-es-Salaam.

Kwa upande wa  Chama cha Mapinduzi (CCM), marehemu aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Afisa Mwandamizi Idara ya Oganaizesheni, Katibu wa Fedha, Uendeshaji na Miradi ya Chama, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika Idara ya Oganaizesheni Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, cheo alichoshikilia hadi mwaka 2014, alipostaafu Utumishi wa Chama.

Aidha, kwa kutambua mchango wake mkubwa katika Utumishi wa Umma, mwaka 2016, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu ya Zanzibar, cheo ambacho alikuwa nacho hadi umauti ulipomfika.

Marehemu Profesa Ishau amezaliwa mwaka 1945 huko Donge Mtambile, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pia, Marehemu ameacha watoto sita, Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.