Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemtumia salamu za pongezi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza mwaka mmoja tokea kushika madaraka ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika salamu hizo,  Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kwa niaba yake na kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanziba na wananchi wake wote wanamtakia kila la kheri Rais Samia katika uongozi wake uliotukuka na kuahidi kuendelea kumuunga mkono ili maendeleo zaidi yaendelee kupatikana hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi  alieleza kuwa uongozi wa Rais Samia utaendelea kuwa Dira ya Maendeleo hasa kwa kuzingatia kauli mbiu yake aliyokuja nayo na “KAZI IENDELEE”, akimaanisha kwamba yale mazuri yote aliyoyaacha mtangulizi wake Hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli anayaendeleza kwa vitendo na kwa ustadi mkubwa.

Hivyo, alisisitiza kwamba wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana kila sababu ya kuendelea kumuunga mkono sambamba na kuiunga mkono kauli mbiu hiyo ili yale maono ya Rais Samia aweze kuyafikia na kuyatekeleza.

Aidha, alieleza imani kubwa waliyonayo wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais wao mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan kwani wanathamini jitihada zake kubwa anazozichukua katika kuhakikisha maendeleo endelevu yanapatikana hapa nchini.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi amemuombea kwa MwenyeziMungu kumpa maisha marefu yenye afya na nguvu Rais Samia ili aendelee kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake