RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK HUSSEIN ALI MWINYI YA KUUAGA MWAKA 2025 NA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA WA 2026

Ndugu Wananchi,

Assalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uhai na Afya njema na kwa kutuwezesha kuifikia siku ya leo, siku ya kuuga mwaka wa 2025 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2026.

Inapofika siku kama hii ya leo tuna wajibu wa kufanya tathmini ya mambo makubwa ambayo yametokea katika nchi yetu kwa kipindi cha mwaka unaomalizika na yale ambayo tunayatarajia kwa mwaka mpya unaokuja. Aidha, huu ni wakati wa kutakiana kheri ya mwaka mpya na kumuomba Mwenyezi Mungu atuengezee ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu.

Ndugu Wananchi,

Moja ya mambo makuu ambayo nchi yetu imepitia katika mwaka unaomalizika ni uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo wananchi walipata fursa ya kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wa kuiongoza nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kwa mara nyengine tena napenda kutumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar wote kwa kushiriki zoezi la uchaguzi mkuu kwa wingi na kwa amani na utulivu. Aidha, navipongeza vyama vyote vya siasa vilivyojitokeza kutumia haki yao ya kushiriki uchaguzi na hatimae kuyapokea na kuyakubali matokeo kwa mujibu wa Tume za Uchaguzi za ZEC na INEC. 

Ndugu Wananchi,

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar kwa kuzingatia Ilani ya CCM ya mwaka 2025 – 2030, mipango mikuu ya maendeleo ya nchi yetu na ahadi tulizozitoa wakati wa kampeni. Tumekamilisha uundaji wa Wizara 20 za Serikali, kuteua Viongozi na Watendaji wakuu wa Wizara hizo na kuwaelekeza matarajio yangu katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Nane. 

Hadi tunapoukamilisha mwaka huu wa 2025, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua kubwa ya mafanikio tuliyoifikia nchini katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa utekelezaji wa miradi mbali mbali ikiwemo ya utalii, ujenzi wa miundombinu, huduma za jamii ikiwemo elimu, afya ,maji safi na salama pamoja na sekta ya michezo kwa kutaja kwa uchache. 

Ndugu wananchi,

Jitihada zetu za kukuza uchumi zimewezesha uchumi wa nchi yetu kukua kwa wastani wa asilimia 7.1. Pato la Taifa kwa bei ya soko limeongezeka kufikia TZS trilioni 6.57 kwa mwaka wa 2024 kutoka TZS trilioni 4.78 mwaka 2021. Aidha, ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka TZS bilioni 856 mwaka 2020/2021 hadi kufikia TZS trilioni 2.104 mwaka 2024. Serikali pia imefanikiwa kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kubaki katika tarakimu moja hadi kufikia asilimia 5.

Kwa upande wa uwekezaji, hadi kufikia mwisho wa mwezi Disemba, 2025, jumla ya miradi 1,657 yenye mtaji wa Dola za Kimarekani bilioni 20,206 imesajiliwa na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) ikihusisha uwekezaji katika sekta za utalii, viwanda, nyumba za biashara na sekta nyengine na kutarajiwa kutoa ajira zaidi ya 87,669. Aidha, mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya utalii ambapo jumla ya watalii 816,438 wameingia Zanzibar kati ya mwezi Januari hadi Novemba, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 27 ya watalii walioitembelea Zanzibar katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2024.

Ndugu Wananchi,

Ujenzi wa miundombinu ya barabara ni hatua muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi. Mafanikio makubwa yamepatikana nchini katika jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya barabara kuu na za ndani kwa mijini na barabara za vijijini. Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, Serikali imekamilisha ujenzi wa km 82.887 wa Barabara za mjini na km 247 wa Barabara za vijijini kwa kiwango cha lami na zege. Sambamba na hilo, Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la juu (flyover) la Mwanakwerekwe kwa asilimia 99, daraja la juu (flyover) la Amani kwa asilimia 30, daraja la Uzi - Ngámbwa kwa asilimia 70 na daraja la Pangatupu kwa asilimia 90. Utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea kwa kasi na unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika Uchumi wa nchi yetu.

Ndugu Wananchi,

Kwa upande wa huduma za jamii, tumepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta ya afya kwa kuimarika kwa mfumo wa rufaa na kuanza kazi kwa hospitali za Wilaya zote 11 na hospitali moja ya Mkoa wa Mjini Magharibi zenye huduma bora za tiba na uchunguzi wa maradhi baada ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya. Aidha, Serikali iliongeza bajeti ya sekta ya afya kutoka TZS bilioni 17 mwaka 2020/2021 hadi TZS bilioni 40 mwaka 2024/2025, kuongeza idadi ya watumishi wa kada mbali mbali za afya na kufanya ukarabati na ujenzi wa vituo vipya vya afya na ujenzi wa nyumba za makaazi za watumishi.

Ndugu Wananchi,

Kwa lengo la kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, Serikali ilifanya uwekezaji mkubwa ambapo bajeti ya elimu imefikia TZS bilioni 830 mwaka 2024/2025 kutoka TZS bilioni 265.5 mwaka 2021/2022, sawa na ongezeko la asilimia 212.6.

 Aidha, Serikali iliimarisha ujenzi wa miundombinu ya elimu ikiwemo kujenga Skuli mpya za ghorofa 35, zenye vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia ili kuimarisha mazingira ya Skuli na  kukabiliana na changamoto ya msongomano wa wanafunzi madarasani. Aidha, Serikali ilitoa ajira mpya za walimu hasa wa masomo ya sayansi ambapo zaidi ya walimu wapya 3,531 waliajiriwa. Hatua hizi zimewezesha kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya Taifa. Aidha, Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu kutoka TZS bilioni 11.5 mwaka 2021/2022 hadi kufikia TZS bilioni 33.4 mwaka 2024/2025, hali iliyowezesha kuongezeka kwa wanufaika wa mikopo hiyo kutoka vijana 4,045 hadi 11,495 wakiwemo wa ngazi ya diploma. 

Ndugu wananchi,

Kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi, Serikali imechukua hatua za kuwapatia mikopo isiyo na riba makundi mbali mbali katika jamii. Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, jumla ya mikopo 6,238 yenye thamani ya TZS 50,773,111,774.00 imetolewa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi kwa wananchi 27,563 (Wanaume 10,917 na Wanawake 16,646) Mikopo hiyo imetolewa kwa sekta mbali mbali zikiwemo kazi za mikono, kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo, huduma za chakula na huduma za kifedha. Kati ya wanufaika wa mikopo hiyo, asilimia 16% ni vijana, asilimia 60% ni wanawake na asilimia 1.8% kwa watu wenye ulemavu. 

Kadhalika, mafanikio makubwa yamepatikana katika uimarishaji wa sekta ya michezo nchini baada ya kukamilika kwa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya michezo kwa viwango vya kimataifa ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Amani Complex, Uwanja wa Gombani, Uwanja wa Mao, Pamoja na viwanja vya michezo vya Maisara. Vile vile, ujenzi wa viwanja vya michezo vya Wilaya unaendelea ambapo baadhi vimefunguliwa katika sherehe za maadhimisho hayo  ya miaka 62 ya Mapinduzi. Viwanja  hivi vina mchango muhimu katika maendeleo ya sekta ya michezo nchini, kukuza vipaji vya vijana wetu katika michezo mbali mbali, kuwa na mazingira bora kwa timu zetu za michezo nchini na kuchochea utalii wa michezo kwa kuvutia timu za nje ya Zanzibar.

Ndugu Wananchi,

Taarifa za kina za mafanikio ambayo tumeyapata kwa kila sekta nitaitoa katika hotuba yangu ya Maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar usiku wa tarehe 11 Januari.

Malengo ya Serikali katika mwaka ujao na kipindi hiki cha pili cha Serikali  ya awamu ya nane ni kuyaendeleza mafanikio tuliyoyapata. Tutaongeza kasi katika kuimarisha ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 7.1 ya sasa, tutaongeza jitihada ili kuongeza kiwango cha mapato ya Serikali, tutaimarisha shughuli za kiuchumi zikiwemo biashara, viwanda na uwekezaji. Sekta ya utalii itaendelea kutiliwa mkazo ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni. Aidha, Serikali itaongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege, kujenga masoko mapya na kuwawezesha wananachi kiuchumi. Aidha, juhudi kubwa zitafanywa katika kuimarisha sekta ya elimu na afya kwa kuongeza ujenzi wa miundombinu zikiwemo Skuli za ghorofa na dakhalia na kuendeleza ujenzi wa hospitali za Mikoa, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Hospitali ya Rufaa na ya Kufundishia na Kituo cha Tiba za Saratani Binguni

Natumia fursa hii kuwasihi wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo. Aidha, tuendelee kushirikiana kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano katika nchi yetu kwa faida yetu sisi na vizazi vijavyo. Nawaomba viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na vyombo vya habari waendelee kuhimiza umuhimu wa kuitunza  amani ili nchi yetu iendelee kuwa salama na izidi kupata maendeleo.

Ndugu Wananchi,

Katika mwaka 2026 tunaoukaribisha, nchi yetu itaadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964. Kama kawaida maadhimisho hayo yataambatana na shughuli tofauti zikiwemo za uzinduzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi, matamasha na mabonaza ya michezo pamoja na matukio mbali mbali yakiwemo ya siku ya kilele tarehe 12 Januari, 2026.

Natumia fursa hii kuwasihi wananchi wajitokeze kwa wingi na kushiriki katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa kwa lengo la kufanikisha sherehe hizi muhimu katika historia na maendeleo ya nchi yetu. Kwa hakika kushiriki kwa kila mmoja wetu ni  ishara ya kudumisha malengo ya Mapinduzi Matukufu na kuthamini jitihada za waasisi wetu za kufanya Mapinduzi ili kuikomboa nchi yetu na kuiletea maendeleo ambapo sote tunaendelea kunufaika na matunda ya Mapinduzi hayo.

Ndugu Wananchi,

Napenda kuhitimisha risala yangu kwa kutoa wito kwetu sote kuazimia kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yetu ili tuweze kuyafikia malengo tuliyojiwekea. Aidha, natumia fursa hii kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar na wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Kadhalika, natoa salamu za kheri ya mwaka mpya, kwa viongozi wa Serikali wa nchi rafiki, Taasisi za Kimataifa na washirika wetu wote wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi yetu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aujaalie mwaka mpya uwe wa neema na wenye baraka nyingi. Aizidishie nchi yetu amani, umoja, mapenzi na mshikamano na atuwezeshe kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo kwa ufanisi zaidi ili tuzidi kupata mafanikio. Nakutakieni nyote kheri za mwaka mpya wa 2026.

 

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR

MUNGU IBARIKI TANZANIA

Ahsanteni kwa kunisikiliza.