HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI, KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 60 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR TAREHE: 11 JANUARI, 2024

Assalamu Aleikum

Ndugu Wananchi,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutupa uhai na afya njema na kutuwezesha kufikia siku ya leo, tukiwa katika mkesha wa Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. 

Tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi, tuna wajibu pia wa kuwakumbuka Waasisi wetu chini ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, viongozi na wananchi wenzetu waliotangulia mbele ya haki, ambao waliitumikia nchi yetu kwa moyo, ujasiri na uzalendo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze pema peponi. Na wale walio hai, Mola awape afya njema na umri mrefu tuendelee kushirikiana nao katika kujiletea maendeleo. 

Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wote kwa kujitokeza kwa wingi katika matukio mbali mbali yaliyoandaliwa katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi. Ni matarajio yangu kuwa na kesho siku ya kilele, mtajitokeza tena kwa wingi katika uwanja wa Amani ili kufanikisha sherehe zetu. 
Tofauti na mara nyengine zote safari hii sherehe yetu itafanyika mchana ili kutoa fursa kwa waumini wa Dini ya Kiislamu kupata nafasi ya kutekeleza ibada ya sala ya Ijumaa.

Mara hii tulikuwa na miradi iliyozinduliwa 65 na miradi 45 imeekewa mawe ya msingi. Hii ni idadi kubwa sana ya miradi ambayo hatujawahi kuifikia katika kipindi cha sherehe kama hizi. Vile vile, tumeandaa matukio makuu maalum na sherehe za aina yake ambazo kilele chake kitafanyika katika uwanja wa Amani. Kadhalika, tuna ujio wa baadhi ya wageni mashuhuri tutakao kuwa nao katika maadhimisho yetu haya. 

Ndugu Wananchi,
Mafanikio tuliyoyapata miaka 60 tokea Mapinduzi ya mwaka 1964, yametokana na uongozi thabiti wa Waasisi wa Taifa letu na viongozi wote wa awamu zilizotangulia kwa ushirikiano na uzalendo kati yao na nyinyi wananchi. Serikali ya Awamu ya Nane tokea ilipoingia madarakani miaka mitatu iliopita, inayaendeleza mafanikio hayo na kufanya juhudi za kuhakikisha Zanzibar inazidi kupiga hatua za maendeleo katika sekta zote na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.

Nilipoingia madarakani mwaka 2020, nilieleza dhamira yangu ya kuunganisha Malengo ya Mapinduzi na uchumi, nikilenga kuimarisha jitihada za kukuza uchumi ili kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar. Lengo la Serikali ninayoiongoza ni kuendeleza umoja, mshikamano na maridhiano ili kila Mzanzibari apate fursa ya kuchangia maendeleo na kunufaika na matunda ya Mapinduzi kwa misingi ya usawa. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika kuifikia dhamira hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Ndugu Wananchi,
Katika kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, tunafurahia mafanikio tuliyo nayo katika kudumisha na kuendeleza Amani, Umoja na Mshikamano. Misingi hii muhimu imetuwezesha kupiga hatua katika maendeleo ya uchumi, ujenzi wa miundombinu, kuimarisha huduma za jamii, biashara na kuendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Natoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM kwa ushirikiano mkubwa anaonipa. Vile vile, nawashukuru viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini na asasi za kijamii, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wote kwa kunipa ushirikiano na kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini kwa faida ya kizazi cha sasa cha baadae.
 Nawahakikishia wananchi na wageni wote wanaotutembelea kwamba nchi yetu ipo salama na kwamba Serikali zetu zote mbili zitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria katika kulinda amani, utulivu na usalama wa mali zao.

Ndugu Wananchi. 
Katika hotuba yangu hii ya kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na miaka mitatu Serikali ya Awamu ya Nane, nitaelezea kwa muhtasari mafanikio, changamoto na mipango yetu ya utekelezaji wa majukumu ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Serikali iliwapa jukumu mawaziri wote kuelezea kwa kina kupitia vyombo vya habari, mafanikio, changamoto na mipango ya kila wizara ili wananchi wafahamu utendaji wa Serikali yao. Nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kutekeleza kwa mafanikio agizo hilo.

Ndugu Wananchi
Juhudi zinazochukuliwa na Serikali zimewezesha uchumi wetu kuzidi kuimarika. Thamani ya Pato halisi la Taifa (GDP at constant Price) imeongezeka kutoka TZS. Trilioni 3.116 kwa mwaka 2020 na kufikia thamani ya TZS. Trilioni 3.499 mwaka 2022. Vile vile ukusanyaji wa mapato umeongezeka kufikia TZS. Trilioni 1.4 mwaka 2022/2023 kutoka TZS. Bilioni 790.48 mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asimilia 56.4. Aidha, kasi ya ukuaji wa uchumi mwaka 2022 imefikia wastani wa asilimi 6.8 ikilinganishwa na asilimia 1.3 ya mwaka 2020. Kiwango cha ukuaji wa uchumi wetu ni kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea. 

Kukuwa kwa uchumi wetu kumetokana na kuongezeka kwa uwekezaji kwa kutekelezwa miradi ya Maendeleo ya kipaumbele ikiwemo miundombinu ya barabara, bandari, viwanja vya ndege, huduma za maji safi na salama, uimarishaji wa huduma za nishati ya umeme, masoko na kuimarika kwa sekta ya huduma kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii. Pato la mtu binafsi nalo limeongezeka kutoka USD 1,099 sawa na TZS. Milioni 2.5 mwaka 2020 na kufikia USD 1,230 sawa na TZS. Milioni 2.8 mwaka 2022. Aidha, jitihada zilizochukuliwa na Serikali zimeweza kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kuendelea kuwa katika tarakimu moja. Kwa mwaka 2023 mfumko wa bei ulikuwa ni wa wastani wa asilimia 6.8 hali inayomuhakikishia mwananchi kupata mahitaji ya lazima.

Ndugu Wananchi
Serikali za awamu zote zilizopita baada ya Mapinduzi zilichukuwa juhudi za uwekezaji kwa ujenzi wa miundombinu, majengo ya Ofisi, huduma na maakazi, viwanda na kuwakaribisha wawekezaji kuzitumia fursa na rasilimali zilizopo nchini katika kuchangia ukuaji wa uchumi. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na Miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane tumeshuhudia mafanikio makubwa katika jitihada zetu za kuvutia wawekezaji.  Kasi ya uwekezaji nchini imeongezeka ambapo jumla ya miradi 296 yenye thamani ya USD. Bilioni 4.5 imeidhinishwa. Miradi hiyo inakadiriwa kutoa ajira zipatazo 17,479 ikihusisha uwekezaji katika visiwa vidogo 16 wenye thamani ya USD. Milioni 377.5, ujenzi wa hoteli za kitalii 112, viwanda 36, biashara ya majengo 56 na miradi mingine ya kiuchumi. 

Mafanikio haya yametokana na mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ikiwemo uimarishaji wa huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambapo sasa wawekezaji wanaweza kupata huduma zote za uwekezaji katika kituo kimoja (One Stop Center) ndani ya masaa 24. Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutangaza fursa zilizopo katika maeneo ya bandari jumuishi ya Mangapwani na ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, maji na umeme katika maeneo ya uwekezaji.

Ndugu Wananchi
Kwa kuzingatia umuhimu wa biashara kwa Zanzibar, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua hatua mbali mbali kuimarisha mazingira ya ufanyaji wa biashara. Tunapoadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na mitatu ya Serikali ya Awamu ya Nane, sekta ya biashara ya usafirishaji na uingizaji bidhaa kwa ujumla inaendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022 Zanzibar imefanya biashara yenye thamani ya TZS. Trilioni 1.4 ukilinganisha na TZS. Bilioni 913.1 kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 57.6.
 
Zanzibar imesafirisha nje bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 180.4 kwa mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 174.7 ikilinganishwa na usafirishaji wa bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 65.7 kwa mwaka 2020. Kwa mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha tani 6,452.8 za karafuu yenye thamani ya TZS. Bilioni 118.3 ikilinganishwa na tani 3,506.8 zilizosafirishwa mwaka 2020, zenye thamani ya TZS. Bilioni 38.37 sawa na ongezeka la fedha la asilimia 208.1. Kwa upande wa mwani Zanzibar imesafirisha Tani 13,972.5 zenye thamani ya TZS. Bilioni 16.0 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na tani 11,382.6 wenye thamani ya TZS. Bilioni 11.7 kwa mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 36.8.  

 Kuhusu biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, mwaka 2022, Zanzibar imesafirisha bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 37.64 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 15.03 zilizosafirishwa mwaka 2020. Kwa upande wa uagiziaji katika kipindi cha mwaka 2022, Zanzibar imeagizia bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 375.80 kutoka Tanzania Bara ikilinganishwa na uagiziaji wa bidhaa zenye thamani ya TZS. Bilioni 243.81 kwa mwaka 2020.

Ndugu Wananchi
Kwa madhumuni ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi, Serikali imechukua hatua za kuimarisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kupambana na umaskini. Serikali imepata mafanikio katika uimarishaji wa vikundi vya ushirika ambapo jumla ya vikundi 1,546 vya ushirika vimesajiliwa. Idadi hiyo imewezesha kufikia vikundi 3,662 vya ushirika vilivyosajiliwa nchini. Kupitia fedha za Ahuweni ya UVIKO - 19, Serikali imetoa jumla ya TZS Bilioni 60. Fedha hizi zinajumuisha TZS. Bilioni 29 zilizotolewa kwa ajili ya sekta za Uchumi wa Buluu, TZS Bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa Masoko na TZS. Bilioni 15 kwa ajili ya Programu ya Inuka yenye lengo la kutoa mikopo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara.

Programu ya Inuka ilianza na mtaji wa TZS. Bilioni 15.0. Hadi sasa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 22.4 imeshatolewa kupitia programu hii. Ongezeko la thamani la mikopo hiyo limetokana na fedha za marejesho ambazo zinaendelea kutolewa mikopo mipya (Revolving Fund). Mikopo hiyo imewezesha kuzalisha ajira za moja kwa moja (direct employment) kwa Wananchi 43,360. Aidha, programu ya Khalifa Fund imetoa mikopo yenye thamani ya TZS. Bilioni 2.10 kwa miradi 18 ya wananchi. Kadhalika, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi jumla ya TZS Milioni 852.17 zimetolewa kwa wananchi.

Kupitia Programu ya Mikopo kwa Makundi Maalum, hadi sasa Serikali imefanikiwa kukusanya jumla ya TZS. Bilioni 1.9 kutoka Halmashauri za Wilaya. Fedha hizi zimelengwa kutumika kwa ajili ya kutoa mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. 

Ndugu Wananchi
Katika kuhakikisha suala la uwezeshaji wananchi kiuchumi linapata mafanikio, Ujenzi wa miundombinu umezingatiwa ambapo vituo viwili vya kusarifu asali vinavyogharimu TZS. Milioni 529.29 vimejengwa Unguja na Pemba.  Aidha, ujenzi wa kituo cha mafunzo ya usarifu mazao utakaogharimu USD. Milioni 1.29 umeanza kwa matayarisho ya awali.
Kadhalika, wajasiriamali wamepatiwa vifaa vya uzalishaji wa asali ikiwemo Mizinga yenye thamani ya TZS. Milioni 459.98, vifaa vya nyuki vyenye thamani ya TZS Milioni 194.34, Vifaa vya maabara vyenye thamani ya TZS Milioni 34.40 na Pikipiki 9 zenye thamani ya TZS Milioni 35.91.

Serikali pia, imeanzisha Wakala ili kuimarisha usimamizi wa utoaji wa Mikopo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB. Vile vile, mafunzo yanaendelea kutolewa kwa wajasiriamali ili kuwajengea uwezo zaidi ambapo wajasiriamali 2,225 wameshapatiwa mafunzo hayo kwa kipindi hiki.Jitihada hizi za Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi cha miaka mitatu, zimewezesha kupatikana kwa jumla ya ajira 187,651. Idadi hiyo imevuka malengo ya ajira 180,000 kwa miaka mitatu, sawa na ongezeko la asilimia 104.3

 Ndugu Wananchi,
Serikali imezingatia haja ya kuwapatia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo mazingira bora ya kufanyia kazi zao. Ujenzi wa vituo 14 vya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo vilivyogharimu TZS Bilioni 16.03 vimejengwa Unguja na Pemba ambapo baadhi yake vimeanza kutumika. Vile vile, jumla ya masoko 10 yamejengwa kwenye Wilaya 6 yenye thamani ya TZS. Bilioni 4.93. Aidha, ujenzi wa masoko makubwa ya kisasa unaogharimu TZS. Bilioni 102.41 unaendelea katika maeneo ya Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini. Ni matumaini yetu kuwa masoko haya yatakamilika mwaka huu 2024 na kuanza kutumika. 

Hadi kufikia tarehe 20 Disemba, 2023 jumla ya wajasiriamali 7,227 wamesajiliwa na kupatiwa vitambulisho katika Serikali za Mitaa Unguja na Pemba. Vile vile, mafanikio yamepatikana katika ukusanyaji wa mapato kwa Serikali za Mitaa, ambapo ukusanyaji wa mapato umeongezeka kwa asilimia 26 kutoka TZS Bilioni 15.24 zilizokusanywa mwaka 2020 hadi kufikia TZS Bilioni 20.71 mwaka 2023.  

Ingia kwenye kiunganishi cha PDF kwa kuipata hutuba nzima