HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI

KATIKA UFUNGUZI WA JENGO LA HUDUMA ZA MATIBABU YA DHARURA NA MAABARA KWENYE KITUO CHA AFYA MAKUNDUCHI WILAYA YA KUSINI MKOA WA KUSINI - UNGUJA

17 JANUARI 2024

 

Waheshimiwa mawaziri Mliopo

Mheshimiwa Hassan Khamis Hafidh, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar,

Mheshimiwa Ayoub, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,

Mhandisi Zena Ahmed Said, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja,

Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja,

Dkt Amour Suleiman Mohamed, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya

Viongozi wa vikosi vya ulinzi na Usalama mliopo,

Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi mliopo

Wakurugenzi wa Wizara ya Afya na Wizara nyengine mliopo,

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Kusini,

Viongozi wa Vyama na Serikali mliopo,

Ndugu wafanyakazi na waandishi wa habari

Wageni waalikwa,

Ndugu Wananchi,

Mabibi na Mabwana,

ASSALAM ALAYKUM

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai  na afya njema na kutuwezesha kukutana kwa madhumuni ya kulifungua rasmi jengo jipya la Huduma za matibabu ya dharura na Maabara ya kisasa katika kituo chetu cha Afya hapa Makunduchi. Napata faraja kuhudhuria tukio hili kwani wiki chache zilizopita, nilipokuja Makunduchi kwa ajili ya kisomo cha Duwa, niliwaahidi viongozi wakiwemo masheha kuwa penye majaaliwa, nitakuja mwenyewe katika sherehe za ufunguzi wa jengo hili. Namshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kufikia dhamira yangu hiyo. Aidha, naishukuru Wizara ya Afya na wafadhili waliondaa shughuli hii ya leo na kwa heshima waliyonipa ya kuwa Mgeni Rasmi. Pia, natoa shukrani zangu za dhati kwenu ndugu wananchi, viongozi na waalikwa wote kwa kuamua kuja kuungana nasi katika tukio hili muhimu la maendeleo ya sekta ya afya.

Ndugu Wananchi,

Ujenzi wa jengo jipya la huduma za matibabu ya dharura  na maabara ya kisasa hapa Makunduchi ni miongoni mwa  juhudi zinazochukuliwa na  Serikali katika kuimarisha miundombinu ya huduma za Afya ili ziweze kwenda sambamba na mabadiliko ya maendeleo ya huduma za afya duniani. Hatua hii vile vile ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020- 2025 pamoja na ahadi tulizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020. Nyote ni mashahidi wa mafanikio ambayo tumeyapata katika kipindi cha miaka mitatu tu ya uongozi wa Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta ya afya kama ilivyo katika sekta nyengine zikiwemo elimu, maji safi na salama, umeme, ujenzi wa barabara na nyenginezo.

Katika sekta hii ya afya, tunathibitisha utekelezaji  wa ahadi  zetu kwa kumaliza kujenga na kufungua hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa ya Lumumba ambazo zote tumeziwekea vifaa vya kisasa na wataalamu kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwa mujibu wa ngazi ya hospitali husika. Leo hii tupo hapa Makunduchi katika tukio jengine la ufunguzi rasmi wa jengo jipya la  huduma za tiba za dharura pamoja  na maabara ya kisasa. Huu ni mwendelezo wa mageuzi makubwa ya maendeleo ya sekta ya afya hapa nchini.

Ndugu wananchi,

Serikali ya  Awamu ya Nane inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha huduma za afya katika ngazi zote. Tumekamilisha ujenzi wa Hospitali katika ngazi ya wilaya na kuanza ngazi ya mkoa. Tutaendelea kujenga hospitali za mikoa katika mikoa iliyobaki ikiwemo Mkoa huu wa Kusini Unguja ambapo taarifa njema ni kuwa mfadhili ameshapatikana. Eneo lipo tayari na mfadhili ameshawasilisha michoro ya awali ya hospitali hiyo itakavyokuwa. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali pia inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa ngazi ya msingi. Hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango mpya wa serikali katika utoaji wa huduma za Afya ngazi ya msingi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu kwa kujenga majengo mapya na kutanua  baadhi ya vituo vya afya nchi nzima, kuweka vifaa vya kisasa kwa lengo la kutoa huduma bora za afya ikiwemo za dharura na uchunguzi wa awali katika ngazi ya msingi ili kupunguza vifo visivyotarajiwa.

Ndugu wananchi,

Serikali imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mipango na mikakati ya kuendeleza sekta ya afya nchini kupitia programu mbali mbali zinazoendeshwa kwa ushirikiano na Washirika wa Maendeleo. Jambo hilo limesaidia kuimarisha huduma za afya katika ngazi ya msingi. Vile vile ujenzi wa miundombinu kama hii na utoaji wa elimu ya afya na uibuaji wa wananchi wenye matatizo mbali mbali ya kiafya mapema kupitia programu hizi ikiwemo ya wafanyakazi wetu katika ngazi ya jamii (CHW) tuliyoizindua rasmi tarehe 16 Disemba 2023 pale Maisara mjini Zanzibar na Afya Call Center. Huduma ambayo mwananchi sasa anaweza kupiga simu kupitia namba 190 bure na kupata ushauri wa kiafya. Serikali ina lengo la kuunganisha kituo hiki muhimu na huduma za dharura nchi nzima. Jambo hili linaisaidia serikali kuimarisha afya ya jamii, mfumo wa rufaa, kupunguza vifo pamoja na kupunguza gharama za matibabu kwani wagonjwa hupatiwa matibabu mapema na kupewa ushauri unaofaa ili kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari, presha na saratani.