HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI KATIKA UZINDUZI WA BARAZA LA KUMI NA MOJA (11) LA WAWAKILISHI TAREHE: 10 NOVEMBA, 2025
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;
Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla;
Makamo wa Pili wa Rais,
Mheshimiwa Dk. Aman Abeid Karume;
Rais Mstaafu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein;
Rais Mstaafu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;
Makamo wa Pili wa Rais Mstaafu,
Mheshimiwa Khamis Ramadhan Abdalla;
Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Sheikh Saleh Omar Kaab;
Mufti Mkuu wa Zanzibar,
Sheikh Hassan Othman Ngwali;
Kadhi Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Dkt. Mwinyi Talib Haji;
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa
Mashirika ya Kimataifa Mliohudhuria,
Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Siasa mliopo,
Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama,
Viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia,
Wageni Waalikwa na Wanahabari,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Mabibi na Mabwana,
Assalam Aleikum,
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uhai na afya njema na kwa kutuwezesha kuhudhuria katika tukio hili muhimu la uzinduzi wa Baraza la Kumi na Moja la Wawakilishi hatua ambayo inaambatana na kuanza kwa kipindi cha Pili cha Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Nane.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuchaguliwa na Waheshimiwa Wajumbe kusimamia majukumu ya chombo hiki muhimu cha uwakilishi wa wananchi na kuisimamia Serikali. Aidha, nawapongeza waheshimiwa Wawakilishi wote kwa kuchaguliwa na wananchi kuwawakilisha katika Baraza hili tukufu. Kwa hakika kuchaguliwa kwetu sote kwa kura nyingi ni ishara ya matumaini makubwa waliyonayo kwetu wananchi wa Zanzibar.
Kwa mnasaba huo tuna wajibu wa kufanya kazi zetu kwa uadilifu na uaminifu kwa kuzingatia matarajio hayo ya wananchi ya kuwaletea maendeleo na kuzipatia ufumbuzi changamoto zao. Naahidi kukupeni ushirikiano ili kuhakikisha tunatimiza ahadi zetu na kuleta maendeleo makubwa kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Katika Baraza hili la Kumi na Moja, mbali na nyinyi Wawakilishi wa kuchaguliwa, kwa mamlaka niliyopewa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, nimefanya uteuzi wa Makamu wa Pili wa Rais ambaye anakuwa ni kiongozi wa shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi. Aidha, nimemteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwenye jukumu la msingi la kuisaidia Serikali katika masuala yote ya kisheria.
Natumia fursa hii kuwapongeza na kuwatambulisha kwenu viongozi wetu hao. Ni matumaini yangu kuwa mtawapa ushirikiano wa kutosha ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mheshimiwa Spika,
Kabla ya kuelezea vipaumbele na mwelekeo wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi hiki cha pili, napenda kutumia fursa hii kukipongeza Chama changu cha Mapinduzi kwa kupata ushindi mkubwa wa asilimia 74.8 kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar, asilimia 80 ya majimbo kwa nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na asilimia 86.4 kwa nafasi za Udiwani katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 29 0ktoba, 2025. Kwa upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupata ushindi wa kishindo wa asilimia 97.66 sambamba na mgombea mwenza Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi. Ushindi huu ni kielelezo thabiti cha imani ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa Chama Cha Mapinduzi. Hivyo, natambua jukumu kubwa lililo mbele yangu pamoja na viongozi sote tuliochaguliwa kwa tiketi ya CCM kwenda kukidhi matarajio ya wananchi. Namuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kutekeleza vyema wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika,
Natoa shukrani tena kwa viongozi wa vyama vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi ambavyo vimepokea matokeo na kuheshimu uamuzi wa wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2025. Nimefarijika sana na kauli ya Mheshimiwa Hamad Rashid aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama cha ADC kwa niaba ya wagombea wengine wa vyama vya siasa aliyoitoa katika ukumbi wa Afisi ya Tume baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais ya kuwa tayari kushirikiana na chama tawala na kuweka mbele maslahi ya nchi yetu.
Kwa mara nyengine napenda nisisitize msimamo wangu wa kuheshimu maridhiano na matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ya kushirikiana na vyama vyengine vya siasa katika kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa misingi ya amani, umoja na mshikamano. Niko tayari kuyatekeleza maridhiano na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Kwa namna ya pekee napenda kuishukuru tena na kuipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa majukumu yake ya kikatiba ya kuendesha uchaguzi kwa uhuru na haki. Aidha, nawashukuru waangalizi wa ndani na wa Kimataifa kwa kushiriki na kutoa maoni yao kuhusiana na namna uchaguzi ulivyoendeshwa kwa misingi ya sheria. Tutazingatia maoni yao iwapo kuna mapungufu waliyoyabaini ili kuzidi kuimarisha zoezi hili kwa ufanisi zaidi.
Natumia fursa hii kuwashukuru sana wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa amani na utulivu. Uchaguzi wa mwaka huu umeweka histori ya kuwa umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa. Shukrani pia nazitoa kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vya SMZ na SJMT kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
VIPAUMBELE NA MWELEKEO WA SERIKALI YA AWAMU YA NANE KATIKA KIPINDI CHA PILI.
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza la Kumi na Moja la Wawakilishi, napenda kuelezea muhtasari wa vipaumbele na mwelekeo wa mipango ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi chake cha pili. Serikali nitakayoiunda ina dhamira ya kutafsiri na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya 2025 – 2030, mipango mikuu ya maendeleo, ahadi tulizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2025 pamoja na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika awamu zote za uongozi wa nchi yetu. Ni matarajio yangu kuwa Baraza hili tukufu la Kumi na Moja litanipa ushirikiano mkubwa mimi na Serikali yangu katika kufanikisha jukumu letu la kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar kwa mafanikio zaidi.
AMANI NA UMOJA WA KITAIFA
Mheshimiwa Spika,
Kipaumbele muhimu cha Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi chake cha pili ni kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano kama msingi mkuu wa maendeleo nchini. Ni dhamira yangu kuzidi kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa wamoja bila ya kujali rangi, imani ya dini, jinsia, asili ya mtu, au itikadi ya kisiasa, jambo ambalo litazingatiwa katika uteuzi wa viongozi na watendaji katika utumishi wa umma pamoja na kuwapatia fursa mbali mbali wananchi wote na kuhakikisha wanafaidika na huduma za Serikali kwa misingi ya usawa.
KUCHOCHEA MAPINDUZI YA UCHUMI WA KISASA NA ENDELEVU
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuzingatia kuwa ukuaji wa uchumi ni chachu ya kuleta maendeleo endelevu, na ustawi wa wananchi, Serikali katika kipindi hiki cha pili cha Awamu ya Nane itahakikisha ukuaji wa uchumi unafungamana na uimara wa sekta za uzalishaji, kuwepo kwa fursa za uwekezaji, upatikanaji wa mitaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi. Katika kufikia dhamira hio, Serikali itaendelea kuimarisha hali ya uchumi kwa kuchukua hatua mbali mbali zikiwemo kuwajengea mazingira wezeshi wananchi wanaoishi kwa kipato cha chini ili kuwawezesha kujikimu kwa huduma za msingi.
Pamoja na mambo mengine, Serikali itachukua hatua za kudhibiti mfumko wa bei kuwa chini ya asilimia 5 kwa mwaka, kuongoza ukuaji wa Pato la Taifa kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka, kuzalisha fursa mpya za ajira laki tatu na nusu (350,000) na kuongeza kipato cha mwananchi kutoka Dola za Kimarekeni 1,241 (sawa na TZS 3,219,898.6) hadi Dola za Kimarekani 1880 (Sawa na TZS 4,877,848).
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaongeza usimamizi wa Sera za Uchumi, Fedha na Mapato kwa kuimarisha mifumo ya kifedha na upatikanaji wa mitaji ili kuimarisha uwekezaji na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Tutafanya mapitio ya Sera na Sheria zinazosimamia fedha ili kuboresha huduma za fedha, tutaimarisha ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika usimamizi wa Sera za fedha na kodi kwa kuzingatia mazingira maalum ya Zanzibar, tutaimarisha na kusimamia upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa wajasiriamali na vikundi vya kijamii, tutaboresha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wananchi wa mijini na vijijini pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za kifedha ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa Sekta Binafsi katika kuimarisha ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii. Hivyo Serikali imedhamiria kuleta maendeleo ya nchi na wananchi kwa kuzidi kuyaimarisha mazingira ya biashara na kuhamasisha uwekezaji kwa kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuwa na uchumi shirikishi.
Serikali itaweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi kwa kupunguza urasimu na kuweka vivutio vya uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi (PPP), kutoa fursa kwa wajasiriamali kupitia mafunzo, mikopo nafuu na kuimarisha miundombinu ya masoko, kuhamasisha uwekezaji katika ubunifu na teknolojia za kisasa, kuendeleza sekta za kilimo, viwanda na huduma na kuweka mazingira ya kubaini fursa za ajira hususan kwa vijana na wanawake kupitia miradi ya maendeleo, ujasiriamali na kufanya uwekezaji katika viwanda vinavyoongeza thamani.
UCHUMI WA BULUU
Mheshimiwa Spika,
Uchumi wa buluu unaojumuisha utalii, uvuvi, mafuta na gesi asilia, mazao ya baharini, kilimo cha mwani, bandari na biashara zinazohusiana na usafiri wa baharini ni sera kuu ya Serikali ya Awamu ya Nane. Katika kipindi cha pili cha uongozi, Serikali itaongeza jitihada za kuimarisha sekta za uchumi wa buluu ili kuchochea kasi ya kukuza uchumi wetu.
Katika utalii, Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa wanaoitembeleza Zanzibar kutoka 800,000 hadi watalii 1,500,000 sambamba na kuongeza wastani wa matumizi ya siku kwa mtalii kutoka Dola za Kimarekani 418 mwaka 2024 hadi Dola 506 kwa siku. Aidha, tumedhamiria kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Pemba kutoka 200,000 hadi 300,000 kwa mwaka. Aidha, tutaimarisha utalii wa mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa, matamasha, utalii wa matibabu, maonesho na michezo, tutaongeza vyumba vyenye hadhi ya juu kutoka 7,626 hadi 10,000 ili kuvutia watalii wenye hadhi kubwa pamoja na kuibua na kuimarisha utunzaji wa vivutio vya utalii vya kimaumbile, mashamba ya viungo na maeneo ya Hifadhi za misitu kwa ushirikiano na wanajamii.
Mheshimiwa Spika,
Uvuvi, mazao ya baharini na kilimo cha mwani ni sekta muhimu katika Uchumi wa buluu ambapo katika kipindi hiki, Serikali itaendeleza sekta hizi kwa kuimarisha miundombinu ya uvuvi kwa kujenga madiko na masoko makubwa mawili, Fungurefu kwa Unguja na Mkoani kwa Pemba pamoja na masoko madogo matano (5). Aidha, tutajenga bandari kubwa mbili za uvuvi, eneo la Ngalawa kwa Unguja na Shumba Mjini kwa Pemba. Pia tutajenga viwanda vya kuchakata samaki na kununua meli kubwa za uvuvi.
Kwa upande wa mazao ya bahari, tutawakuza wafugaji wa mazao ya bahari wakiwemo wafugaji wa samaki, matango bahari na kaa kwa kuwawezesha kufuga kibiashara na pia tutajenga mabwawa ya ufugaji wa samaki na vizimba vya kufugia samaki baharini. Katika kilimo cha mwani, tutaongeza uzalishaji wa mwani mkavu kutoka tani 19,715 mwaka 2024 hadi tani 40,000 kufikia mwaka 2030 pamoja na kuanzisha vituo saidizi vya kusarifu mwani ili kuuongeza ubora na thamani ya bidhaa zinazozalishwa kutokana na mwani. Aidha, tutatafuta fursa zaidi za masoko ya mwani na bidhaa zake ili kuwapa tija zaidi na faida wakulima wa mwani.
Mheshimiwa Spika,
Kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia, jitihada zilizofanyika za kuimarisha sekta hizi zimeanza kupata mafanikio. Tayari Serikali ilishatangaza vitalu 10 vya mafuta na gesi asilia vikiwemo 8 vya baharini na viwili vya nchi kavu kwa wawekezaji wa utafutaji wa rasilimali hizo. Aidha, Serikali imekamilisha marekebisho ya modeli ya mkataba wa mgawanyo wa mapato ya uzalishaji kwa lengo la kuwavutia wawekezaji na kulinda maslahi ya nchi yetu. Katika kipindi hiki, tunalenga pamoja na mambo mengine kuendeleza utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, kuendelea kutangaza na kugawa vitalu vipya vya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia na kujenga kituo cha kudumu cha kuhifadhi taarifa za sampuli za mafuta na gesi asilia.
Mheshimiwa Spika,
Bandari na usafiri wa bahari vina umuhimu mkubwa kwa nchi za visiwa kama ilivyo Zanzibar. Katika kipindi hiki, tutandeleza ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani inayojumuisha bandari ya mizigo, uhifadhi wa makontena, uhifadhi wa mafuta na gesi pamoja na uhifadhi wa nafaka. Aidha, tutajenga bandari za kisasa za abiria Mpigaduri na Kizimkani kwa Unguja na Shumba na Wete kwa Pemba pamoja na kuimarisha bandari ya Malindi kwa ajili ya huduma za utalii.
Katika kuimarisha usafiri wa bahari, Serikali imeingia mkataba wa ujenzi wa boti 2 za kisasa za mwendo kasi zitakazofanya safari za kusafirisha abiria katika bandari za Unguja, Pemba, Tanga na Dar es salaam. Lengo letu katika kipindi hiki ni kuimarisha na kupanua wigo wa huduma za usafiri wa baharini ili kukuza biashara, kuongeza mapato na kurahisisha usafiri wa mizigo na abiria kati ya Zanzibar, Bara na nchi jirani.
SEKTA ZA UZALISHAJI
Mheshimiwa Spika,
Sekta za uzalishaji zina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji, fursa za ajira na kukuza Pato la Taifa. Katika kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Nane, Serikali imedhamiria kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha na kukuza maendeleo ya Sekta za Uzalishaji zikiwemo Kilimo, Mifugo, Maliasili na Viwanda.
Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta za kilimo kwa maendeleo na ustawi wa uchumi, upatikanaji wa chakula na kipato kwa wananchi wengi wa Zanzibar hasa wanaoishi vijijini, Serikali ina dhamira ya kuongeza uzalishaji na huduma katika sekta ya Kilimo ikiwemo kufanya mageuzi makubwa yanayozingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Tutaimarisha miundombinu ya uzalishaji, ikiwemo mifumo ya umwagiliaji, upatikanaji wa mikopo nafuu na masoko kwa bidhaa za kilimo.
Aidha, Serikali itaanzisha hifadhi ya Taifa ya chakula kwa kukarabati maghala manne 4 na kujenga vihenge (Silos) Dunga Unguja na Chamanangwe Pemba vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000 kwa wakati mmoja. Serikali pia itaanzisha mfumo wa upatikanaji wa huduma za pembejeo muhimu za kilimo ikiwemo mbolea, viatilifu, mbegu na miche bora, huduma za ugani na zana za kisasa za kilimo kwa kushirikiana na sekta binafsi. Pamoja na hayo, Serikali itaandaa program maalum ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya karafuu, matunda, mboga na viungo kwa kuwahusisha vijana na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa za kilimo ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itachukua hatua za kuimarisha Sekta ya mifugo kutokana na umuhimu wake kiuchumi kwa kuwezesha matumizi ya teknolojia za kuongeza uzalishaji na tija, kuimarisha miundombinu ya uzalishaji na upatikanaji wa mikopo nafuu na masoko ya bidhaa za mifugo. Serikali itaongeza uzalishaji wa kuku, mayai, nyama na kulinda masoko ya bidhaa hizo kwa kudhibiti uingizaji wa bidhaa za mifugo kutoka nje ya nchi. Kwa kushirikiana na sekta binafsi, Serikali itaweka vivutio katika uanzishaji wa viwanda vya uzalishaji wa vifaranga na vyakula vya mifugo. Pia, tutajenga vituo vya kisasa vya matibabu ya mifugo na kutoa ushauri wa kitaalamu wa ufugaji katika kila Wilaya pamoja na kuwezesha vijana kushiriki katika ufugaji kwa kuwapatia taaluma, mikopo yenye masharti nafuu na masoko.
Mheshimiwa Spika,
Misitu na maliasili ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar na watu wake. Kwa kuzingatia hilo, Serikali itachukua hatua za makusudi kulinda na kusimamia maliasili na misitu yetu kwa matumizi endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Kwa lengo la kufikia dhamira hio, Serikali itaongeza ushiriki wa jamii katika udhibiti na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa kuongeza misitu mipya ya hifadhi, kuongeza vivutio katika maeneo ya uhifadhi na kuboresha miundombinu ya huduma. Pia, Serikali itatekeleza mpango wa kurithisha Zanzibar ya kijani kwa kupanda miti ya aina mbali mbali ya matunda, bustani, miti ya vivuli, mikoko na miti ya asili, kuwezesha vijana kwa mitaji na taaluma katika kuzalisha na kusarifu asali kibiashara pamoja na kuandaa programu za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia itayozingatia utoaji wa ruzuku katika bei na vifaa vya nishati safi. Lengo ni kusaidia wananchi kujenga uwelewa juu ya umuhimu wa kutumia nishati safi na usalama wake.
Mheshimiwa Spika,
Serikali inathamini mchango wa vyama vya ushirika vikiwemo vya uzalishaji na SACCOS katika kukuza uchumi na kuinua kipato cha wananchi katika kujikimu kimaisha. Kwa kuzingatia umuhimu huu, Serikali itaanzisha mifumo ya kielektroniki kurahisisha usajili, usimamizi na ukaguzi wa vyama vya ushirika, kupata masoko ya uhakikia, kuhamasisha vyama vya ushirika kununua hisa katika benki ya Ushirika Tanzania na kuweka vivutio maalum kwa lengo la kuongeza ushiriki wa vijana na makundi mengine katika sekta ya ushirika.
Mheshimiwa Spika,
Upatikanaji wa nishati ya umeme, mafuta na gesi wenye kukidhi mahitaji muhimu katika kuchochea uzalishaji na upatikanaji endelevu wa huduma na ukuaji wa uchumi, ni mambo ya msingi yaliyopewa mazingatio katika kipindi cha pili cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane. Katika kufikia malengo hayo, Serikali imedhamiria kujenga miundombinu ya kisasa ya uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vipya ikiwemo jua, upepo na umeme unaotokana na taka ili kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja. Aidha, tutajenga vituo maalum vya gesi na umeme na kushajiisha matumizi ya magari maalum yanayotumia nishati ya umeme, kujenga miundombinu ya uhifadhi wa mafuta na gesi asilia na kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaozingatia uhimilivu wa bei na uwezo wa wananchi. Aidha, Serikali itaongeza matumizi ya nishati mbadala katika sekta ya kilimo, huduma za maji, elimu na afya.
Mheshimiwa Spika,
Sekta ya biashara ina umuhimu mkubwa katika mipango yetu ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii kwa kuchangia katika mzunguko wa fedha, fursa za ajira na upatikanaji wa bidhaa na huduma. Serikali katika kipindi hiki imedhamiria kuimarisha sekta ya biashara kwa kuchukua hatua mbali mbali zikiwemo kuimarisha urari wa biashara katika uchumi wa Zanzibar. Aidha tutajenga kituo cha Kimataifa cha Biashara Dimani, kuendeleza program ya mapitio ya ada na tozo ambazo ni kero kwa wananchi na wafanyabiashara, kudhibiti uingizaji wa bidhaa bandia kwa kuimarisha usimamizi kwenye vituo vya ukaguzi wa bidhaa na kujenga maabara za kisasa za upimaji (Testing House) Chamanangwe Pemba na Dunga kwa lengo la kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa na kuzalishwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Katika kuimarisha sekta ya viwanda yenye umuhimu mkubwa katika kukuza uchumi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kuleta ajira, Serikali imedhamiria kuchukua hatua za kuandaa programu maalum ya kukuza viwanda vya usindikaji wa bidhaa zinazotokana na mazao yenye thamani (high value crops) ikijumuisha viungo, mafuta ya mimea na mwani, kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 20.8 ya sasa hadi asilimia 25, kuweka mkakati wa kuongeza viwanda vipya ili kupunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje kwa bidhaa maalum na kukidhi asilimia 60 ya mahitaji ya ndani. Serikali pia itayaendeleza maeneo maalum ya uwekezaji wa viwanda (EPZ) ya Chamanagwe Pemba na Dunga Unguja kwa kuweka miundombinu muhimu ya uzalishaji na kuwawezesha wazalishaji wadogo kuyatumia maeneo hayo. Aidha, Serikali itawawezesha wawekezaji wa ndani katika kuzalisha vifungashio bora vya bidhaa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ndani hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Ardhi ni rasilimali muhimu kwa shughuli mbali mbali za maendeleo ikiwemo kilimo, viwanda, hifadhi ya mazingira na uwekezaji. Serikali itahakikisha inasimamia vyema na kwa ufanisi sera na sheria za matumizi ya ardhi ndogo tuliyonayo kwa matumizi endelevu ya maendeleo. Katika kufikia dhamira hiyo, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya sera, mipango na sheria za ardhi ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kimazingira na utekelezaji wa mkakati wa usimamizi wa ardhi. Aidha, Serikali itaendeleza upimaji na kuyatangaza maeneo maalum ya kuduma ya ardhi kwa matumizi ya viwanda na uwekezaji, maeneo ya kilimo na maeneo ya ardhi yaliyo wazi kwa matumizi ya jamii. Aidha, Serikali itaendelea na zoezi la utambuzi na usajili wa ardhi na kuanza mpango wa kufukia bahari (reclamation) kwa lengo la kupata ardhi kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
MIUNDOMBINU YA USAFIRI NA USAFIRISHAJI
Mheshimiwa Spika,
Miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo barabara na viwanja vya ndege ina umuhimu mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi, kuimarisha huduma na kuchochea uwekezaji.
Katika kipindi hiki, Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu ya usafiri kwa kujenga barabara ya Tunguu-Makunduchi (km 48), Fumba – Kisauni (km 12), Mkoani – Chake (km 43.5) na barabara za Utalii Nungwi (km 12) pamoja na kuweka taa za barabarani katika maeneo yote hayo ikiwemo barabara za ndani. Aidha, tutaweka taa za kuongozea gari kwenye makutano 10 ya barabara yakiwemo Mpendae, Mkunazini, Malindi, BOT Kinazini, Mikunguni kwa Pweza, Mtoni na Saateni kwa Unguja na Machomane, Chanjaani (njia ya uwanja wa ndege) na Melitano kwa Pemba. Pia tutaendeleza ujenzi wa barabara za mjini km 100.9, vijijini km 275 na barabra mpya za mjini km 333.7. Pia, tutakamilisha ujenzi wa daraja na barabara ya Unguja Ukuu - Uzi na kujenga daraja litakalopita baharini la kuunganisha kijiji cha Chwaka na Charawe ili kuunganisha barabra baina ya Mkoa wa Kusini (U) na Mkoa wa Kaskazini (U).
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi hiki tuna lengo la kuongeza idadi ya abiria wanaotumia viwanja vyetu vya ndege kutoka 2,140,986 kwa mwaka hadi kufikia abiria 2,824,011 ili kuongeza kipato na ajira. Ili kufikia azma hiyo, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa ujenzi wa majengo na ukarabati wa baadhi ya majengo ya zamani, kujenga vituo viwili vya mafuta ya ndege na karakana ya kufanyia matengenezo ya ndege na kuongeza eneo la maegesho ya ndege kwa mita za mraba 106,000. Aidha, tutaendeleza ujenzi wa njia ya kurukia ndege katika kiwanja cha ndege cha Pemba na kujenga jengo jipya la abiria.
MAENDELEO YA MIPANGO MIJI, NYUMBA NA MAKAAZI
Mheshimiwa Spika,
Tuliahidi kuendelea kusimamia maendeleo ya miji na kuwapatia wananchi nyumba bora za makaazi, katika kipindi hiki tutaendelea kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba mpya za makaazi 4,715 katika maeneo ya Chumbuni, Nyamanzi na Kisakasaka kwa Unguja na Mfikiwa Pemba kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini, tutaandaa sera maalum ya makaazi bora yenye kufuata mpangilio na kupendezesha miji yetu, tutaandaa mpango bora wa matumizi ya ardhi na kuongeza asilimia ya watu wanaoishi katika makaazi yaliyofuata mipango miji kutoka asilimia 18 mwaka 2025 hadi asilimia 40.
UWEZESHAJI WA WANANCHI KIUCHUMI
Mheshimiwa spika,
Serikali inazingatia umuhimu mkubwa wa haja ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kutokana na faida zake kwa maendeleo yao binafsi na nchi yetu kwa jumla. Katika kuendeleza dhamira hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi itatoa mikopo ya jumla ya TZS bilioni 100 kwa wananchi pamoja na kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wajasiriamali wazalishaji na wafanyabiashara. Pia itawapatia mafunzo ya uzalishaji na kuwaunganisha na masoko. Aidha, mikopo kutoka Serikali za Mitaa itatolewa kwa mgawanyo wa asilimia 40 kwa vijana, asilimia 40 kwa wanawake na asilimia 20 kwa watu wenye ulemavu. Vile vile, Serikali itatoa mikopo kwa wajasiriamali wakubwa ili kuwawezesha kuwaajiri vijana.
Serikali pia itaendelea kujenga masoko mapya kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali katika maeneo mbali mbali yakiwemo Kibanda maiti, Kwa haji tumbo, Fuoni, Kinyasini (U) na kukamilisha ujenzi wa soko la Mombasa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao katika mazingira bora.
FURSA ZA AJIRA KWA VIJANA
Mheshimiwa Spika,
Natambua uwepo kwa uhitaji mkubwa wa ajira kwa wananchi hususan vijana hapa nchini. Katika kukabiliana na changamoto ya ajira pamoja na mambo mengine, Serikali katika kipindi hiki itaendeleza program za kukuza ujuzi kwa vijana ambao watapewa mafunzo kazini na taaluma kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajirika katika sekta za umma na binafsi, kuendeleza utaratibu wa kulinda fursa za ajira kwa vijana wazawa kupitia sera na sheria, kuandaa program maalum za kuwavutia wawekezaji wa sekta binafsi kwa lengo la kuajiri vijana na kutoa mafunzo mahsusi ikiwemo ujuzi wa fani adimu ambazo vijana wanashindwa kupata fursa za ajira kwa kukosa ujuzi unaohitajika.
Aidha, Serikali itaandaa mpango maalum wa kuwaibua vijana wajasiriamali mabingwa na kuwawezesha kukuza miradi yao ili waweze kuajiri vijana wengine na kutoa mafunzo na usimamizi kwa wajasiriamali wapya. Lengo la jumla la Serikali katika kipindi hiki ni kuzalisha ajira mpya 350,000 kwa wananchi wa Zanzibar hasa vijana katika sekta rasmi na zisizo rasmi.
MAENDELEO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika,
Serikali itatilia mkazo maendeleo ya Sayansi na Teknolijia ili kuongeza kasi ya maendeleo kiuchumi na huduma za jamii. Serikali itaimarisha mazingira ya uchumi wa kidijitali na kuongeza upatikanaji wa teknolojia mpya. Serikali itaimarisha uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA na kujenga vituo vya teknolojia vinavyokidhi viwango vya kimataifa, pamoja na kuanzisha majukwaa ya mtandaoni na mifumo ya biashara inayosaidia masoko ya ndani, ya kanda na kimataifa. Kadhalika, Serikali itaimarisha uchumi wa kidijitali kwa kuzingatia thamani yake kubwa kama nyenzo muhimu kwa ustawi wa sekta nyengine, utoaji wa huduma na uendeshaji wa shughuli za Serikali. Pia shughuli za utafiti na ubunifu zitapewa msukumo ili kuchochea ufanisi katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo.
HUDUMA ZA JAMII
Mheshimiwa Spika,
Kuimarisha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji safi na salama ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa huduma hizo kwa ustawi wa wanajamii. Katika sekta ya afya Serikali ina lengo la kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kujenga hospitali 4 mpya za Mikoa ya Kusini (U), Kaskazini (U) Kusini (P) na Kaskazini (P), kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kuendelea na ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, kujenga hospitali ya rufaa na kufundishia ya kisasa Binguni, kuendeleza ujenzi wa hospitali ya wagonjwa wa akili Pemba na kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa huduma bora za afya ya msingi ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu katika kuandaa nguvukazi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Serikali itaendelea kuimarisha sekta hii katika miaka mitano ijayo. Serikali itaendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya elimu, kuzipatia skuli vifaa vya kujifunza na kufundishia, vifaa vya maabara za masomo ya Sayansi na Teknolojia, kutoa mafunzo ya ualimu na kuhakikisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa kinazidi kuongezeka. Tutajenga madarasa mapya 2,000 katika skuli 29 za ghorofa za msingi na sekondari. Skuli 3 za sekondari za wanawake zitajengwa kwa kila Mkoa ili kuimarisha upatikanaji wa fursa ya elimu ya sekondari kwa watoto wa kike, tutaimarisha mafunzo ya elimu ya amali na tutajenga dakhalia katika kila Wilaya kwa mujibu wa mahitaji. Pia Serikali itaimarisha utoaji na usimamizi wa mikopo ya wanafunzi na kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka 8,870 mwaka 2024 hadi kufikia 20,000. Vile vile, tutaimarisha mafunzo ya ualimu kwa kujenga Chuo cha kisasa cha mafunzo ya ualimu, tutaajiri walimu wapya 7,691 na kuimarisha maslahi ya walimu.
Kuhusu huduma za maji safi na salama, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa kuendeleza jitihada zilizoanza za ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama katika maeneo yote ya nchi yetu. Serikali itaongeza juhudi kwa kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usambazaji na kuunganisha huduma za maji safi na salama wananchi.
USTAWI WA MAKUNDI MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Serikali katika kipindi chake cha pili cha uongozi, itaendelea kuweka mazingatio makubwa katika kuhakikisha ustawi na maendeleo ya makundi maalum yakijumuisha watu wenye ulemavu, wanawake, watoto na wazee. Serikali itashajiisha upatikanaji wa ajira zenye staha kwa watu wenye ulemavu, itahakikisha wanashirikishwa katika shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na kuzilinda na kuziimarisha haki zao. Tutaongeza uwiano wa watu wenye ulemavu katika kupata huduma na kuendelea kutoa ruzuku kwa jumuiya za watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wa wanawake, Serikali inatambua umuhimu wa kuliwezesha kundi hili kwa kukuza usawa na haki katika jamii. Serikali itaimarisha mifumo ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, kuimarisha jitihada za kupambana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, kuanzisha na kuimarisha mitandao ya wanawake ili kusaidia kubadilishana maarifa na fursa za maendeleo pamoja na kuendelea kuimarisha ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi katika sekta za umma na binafsi. Aidha, mazingatio pia yatawekwa kwa kuwasaidia wajane waweze kujikimu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuzingatia kuwa watoto ndio Taifa la kesho, Serikali itahakikisha wanalindwa dhidi ya changamoto mbali mbali ikiwemo udhalilishaji na kukosa malezi bora. Serikali itaimarisha mifumo ya hifadhi ya mtoto na kutoa ulinzi ili wawe na mustakabali mwema. Tutahamasisha wazazi kuwalea watoto kwa misingi bora na maadili ili wawe raia wema na kuwaepusha na mazingira hatarishi pamoja na kudhibiti ajira na ndoa za utotoni.
Kuhusu wazee, Serikali inatambua kuwa wao ni hazina kubwa ya hekima, uzoefu, urithi wa mila, desturi na maadili yetu. Serikali itaendelea kuhakikisha hifadhi ya wazee wetu na kuwatunza wakiwemo wanaoishi katika nyumba za wazee Sebleni, Welezo na Limbani. Aidha, wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 wataendelea kupatiwa Pencheni jamii. Ahadi yangu ni kuongeza kiwango wanachopata sasa kwa kadiri hali yetu ya uchumi itakavyoruhusu.
Katika kuimarisha hifadhi ya jamii, Serikali itaimarisha mifumo ya huduma za jamii ili iwafikie wananchi wengi zaidi. Mafao kwa wastaafu yataendelea kulipwa kwa wakati, tutaendeleza huduma za Bima ya Afya kwa wote na kusaidia kaya maskini kwa kuongeza idadi ya wananchi wanaonufaika na fedha za TASAF na fursa za kujiongezea kipato.
UTUMISHI WA UMMA
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa watumishi wa umma, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira yao ya kufanyia kazi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kufanyiakazi na kuongeza maslahi yao ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Katika kipindi hiki cha pili cha Serikali ya Awamu ya nane, tutaimarisha uzalendo, nidhamu na uwajibikaji katika Utumishi wa Umma kwa kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi wa tabia, uadilifu na utendaji. Ofisi ya Usalama wa Shughuli za Serikali (GSO) itakua chombo kikuu cha uratibu na ufuatiliaji wa nidhamu Serikalini, ikihakikisha kuwa uwajibikaji na uadilifu vinakua utamaduni wa kudumu katika utumishi wa Umma.
Serikali itaendeleza jitihada za kukabiliana na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora ikiwemo Rushwa, Uhujumu wa Uchumi na ukiukaji wa maadili ya utumishi. Serikali itazidi kuijengea uwezo wa vifaa vya kisasa, mafunzo na watumishi Mamlaka ya kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Aidha, jitihada za makusudi zitafanywa ili kuiwezesha Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuongeza uwezo wa Ofisi hii kutumia mifumo na kwenda sambamba na mabadiliko ya tasnia ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma.
Aidha, tutahakikisha viongozi wote katika utumishi wa umma wanazingatia sheria na maadili ya utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa dhamira ya Serikali ya kuwa na Utumishi wa umma bora, wenye nidhamu na uwajibikaji kuna tegemea mchango wa kila mmoja wetu. Naomba waheshimiwa wawakilishi na wananchi wote mniunge mkono katika kuifikia dhamira hii.
HABARI NA MAWASILIANO
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya habari na mawasiliano kwa maendeleo ya nchi yetu. Serikali itaendelea kuimarisha ubora na upatikanaji wa habari kupitia redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii katika maeneo yote ya Zanzibar. Tutaendelea kuwekeza na kuimarisha miundombinu ya Shirika ka Utangazaji la Zanzibar (ZBC) ili kuimarisha huduma za utangazaji. Aidha, Serikali itakamilisha miundombinu ya kiwanda cha uchapishaji wa magazeti ya Serikali ili kuongeza ufanisi.
Kwa upande wa sekta ya mawasiliano, Serikali itaanzisha mji wa kidijitali (smart city) katika maeneo ya uwekezaji Fumba, tutaboresha mawasiliano ya simu katika visiwa vidogo vidogo, tutaimarisha mfumo wa Serikali mtandao katika utendaji wa Serikali ili kuongeza ufanisi pamoja na kuweka majina ya mitaa na barabara kwenye mfumo wa anwani za makaazi kwa wananchi ili wazitumie na kuimarisha huduma za mawasiliano nchini.
UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
Mheshimiwa Spika,
Serikali inatambua na kuthamini umuhimu wa sekta ya utamaduni, sanaa na michezo katika kuimarisha maendeleo ya nchi yetu. Sanaa na utamaduni zitaendelezwa kwa kuimarisha juhudi za kuendeleza urithi wa Kiswahili, historia, sanaa na utamaduni wa Mzanzibar ili kuvutia watafiti, wanafunzi na watalii wa utamaduni duniani kote. Serikali itajenga vituo viwili (2) vya kuendeleza sanaa na urithi wa utamaduni katika maeneo ya kimkakati Unguja na Pemba ambapo wageni watajifunza historia, mapishi na mavazi ya Kizanzibari pamoja na kuandaa matamasha ya kimataifa ya utamaduni ikiwemo ya chakula na ya mavazi ya Mzanzibari ili kuvutia watalii na kuutangaza utamaduni wetu.
Kwa upande wa michezo, Serikali itaimarisha sekta hii kwa kuendelea kujenga miundombinu bora ya michezo. Serikali itajenga na kukarabati miundombinu ya michezo na burdani ikiwemo viwanja na vituo vya michezo na utamaduni vinavyokidhi hadhi ya kitaifa na kimataifa kila Wilaya. Serikali itaanzisha Skuli mbili (2) za akademia za michezo kwa lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo. Tutafanya juhudi za kuongoza ushiriki wa wanamichezo wa Zanzibar katika mashindano ya kikanda na kimataifa na kukamilisha maandalizi yetu ya kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON, 2027 kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya michezo na kuboresha miundombinu wezeshi ya malazi usafiri na huduma za tiba
KUDUMISHA MAPINDUZI NA KUENDELEZA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Mapinduzi matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania ni tunu muhimu kwa maendeleo na ustawi wa taifa letu. Serikali itaendelea kuyatafsiri malengo ya Mapinduzi kwa vitendo na kuhakikisha yanadumishwa kwa dhamira ile ile ya waasisi wetu kuwa ni kupata uhuru na maendeleo ya Zanzibar. Serikali ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha tunauendeleza Muungano wetu kwa kuuimarisha ili uzidi kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili na kuwa msingi muhimu wa amani, umoja na maendeleo yetu.
Aidha, tutaendeleza ushirikiano na wadau wote wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi zikiwemo nchi rafiki, mashirika na taasisi za kimataifa, jumuia za wafanya biashara na taasisi za dini, asasi za kiraia na wengineo wenye nia ya kushirikiana nasi katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo.
Ni dhahiri kuwa mafanikio ya utekelezaji wa vipaumbele na mwelekeo wa mipango ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kipindi hiki, hayawezi kufikiwa bila ya kuitunza amani na kufanya kazi kwa ushirikiano, bidii na uzalendo na kuweka mbele maslahi ya nchi yetu. Natumia fursa hii kukuombeni wananchi wote tuwe tayari kutekeleza wajibu wetu ili tuifikie dhamira ya kuwa na Zanzibar yenye maendeleo zaidi. Namuomba Mwenyezi Mungu atusaidie.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kukushukuru wewe binafsi na Naibu Spika, Sekretarieti ya Baraza na Wajumbe wote wa Baraza la kumi na moja la Wawakilishi kwa maandalizi mazuri ya shughuli hii. Nakutakieni nyote kila la kheri na mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yenu. Aidha, nawashukuru Wageni Waalikwa wakiwemo viongozi wakuu wastaafu, waheshimiwa mabalozi, viongozi na watendaji wa Serikali na wale wote waliohudhuria hafla hiii. Navishukuru vyombo vya habari vinavyowatangazia wananchi tukio hili. Kadhalika, nawashukuru wananchi wote wanaofuatilia uzinduzi huu kupitia vyombo vya habari. Tumuombe Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamano na atuwezeshe kutekeleza mipango yetu ya maendeleo kama tunavyoitarajia.
Baada ya kusema hayo, kwa mamlaka niliyo nayo katika Ibara ya 91 ya kifungu (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, sasa natamka kuwa Baraza la Kumi Moja (11) la Wawakilishi la Zanzibar limezinduliwa rasmi, leo tarehe 10 Novemba, 2025.
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kuniskiliza.