HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI YA MAADHIMISHO YA MIAKA 62 YA MAPINDUZI MATUKUFU YA ZANZIBAR

TAREHE: 11 JANUARI, 2026

Ndugu Wananchi,

Assalamu Aleikum

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uhai na afya njema na kwa kutuwezesha kuifikia siku ya leo ambapo wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla tunaadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Kwa hakika, Mapinduzi ya Januari 1964 ni tukio muhimu katika historia ya nchi yetu na ni mwanzo wa safari yetu ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa mnasaba huo, maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ni wakati wa kutathmini japo kwa muhtasari mafanikio ya malengo ya Mapinduzi kwa dhamira ile ile ya waasisi wetu ya kujikomboa na kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wote.

Ndugu Wananchi

Mwaka huu wa 2026, nchi yetu inatimiza miaka 62 ya Mapinduzi tukiwa na kauli mbiu isemayo: Amani na Umoja, Ndio Msingi wa Maendeleo Yetu,Mapinduzi Daima”. Kauli mbiu hii inaakisi ukweli kuwa mafanikio makubwa ambayo nchi yetu imeyapata tokea Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964, yametokana na msingi wa amani na umoja wetu kwa jitihada za viongozi wa Awamu zote za uongozi hapa Zanzibar na ushirikiano mkubwa wa wananchi. Serikali ya Awamu ya Nane ilipoingia madarakani mwaka 2020, tuliahidi kudumisha mafanikio ya Awamu zilizotangulia za uongozi na kuyatafsiri malengo ya Mapinduzi kwa vitendo kwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano kwa manufaa ya wananchi wote.

Ndugu Wananchi,

Tunaadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ikiwa ni mwanzo wa kipindi cha pili cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane. Katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza la 11 la Wawakilishi tarehe 10 Novemba, 2025 nilielezea vipaumbele na mwelekeo wa mipango ya Serikali kwa kipindi chake cha pili. Katika hotuba yangu hii, nitaeleza kwa muhtasari mafanikio na mwelekeo wa mipango ya Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Moja ya mafanikio makubwa ambayo tunajivunia ni kuendelea kuwepo kwa amani nchini. Hii ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mipango yetu yote ya maendeleo na ustawi wa Taifa letu. Napenda kutumia fursa hii kwa mara nyengine kusisitiza umuhimu wa kuitunza amani na kuendelea kuwa wamoja na wenye mshikamano. Kwa kufanya hivyo, nchi yetu itazidi kupiga hatua kubwa zaidi za maendeleo tunayoyatarajia kwa faida yetu sote.

Ndugu wananchi,

Katika miaka 62 ya Mapinduzi, tunajivunia mafanikio tuliyoyapata katika ukuaji wa uchumi nchini. Juhudi tulizozifanya katika usimamizi wa sera za Uchumi na fedha pamoja na makusanyo ya mapato kwa kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki na upatikanaji wa mitaji, zimewezesha kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika vyema ambapo kwa mwaka 2024, umekua kwa kasi ya asilimia 7.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.3 mwaka 2020.

Pato la Taifa kwa bei ya soko limeongezeka kufikia TZS trilioni 6.57 kwa mwaka wa 2024 kutoka TZS trilioni 4.78 mwaka 2021. Aidha, ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka TZS bilioni 856 mwaka 2020/2021 hadi kufikia TZS trilioni 2.104 mwaka 2024. Serikali pia imefanikiwa kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kubaki katika tarakimu moja hadi kufikia asilimia 5. 

Kwa upande wa uwekezaji, hadi kufikia mwisho wa mwezi Disemba, 2025, jumla ya miradi 1,657 yenye mtaji wa Dola za Kimarekani bilioni 20.206 imesajiliwa na Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) ikihusisha uwekezaji katika sekta za utalii, viwanda, nyumba za biashara na sekta nyengine na kutarajiwa kutoa zaidi ya ajira 87,669. 

Katika kuendelea kuvutia uwekezaji, Serikali kupitia ZIPA itayaimarisha maeneo maalum ya uchumi ya (SEZs) Micheweni na Fumba kwa kutoa vivutio maalum kwa wawekezaji wa miradi ya viwanda, utalii na mingine. Aidha, Serikali itaongeza uwekezaji kwa kuwavutia wawekezaji wa Kimataifa (FDI) katika sekta za uchumi wa buluu, utalii, viwanda, nishati mbadala, sekta ya ICT, usafiri wa anga na wa baharini na kilimo. Aidha, Serikali ina lengo la kuongeza idadi ya miradi ya uwekezaji wa pamoja na sekta binafsi (PPP) kutoka 21 iliyopo sasa, kutokana na umuhimu wa miradi ya aina hii katika kuchochea ukuaji wa uchumi. 

Ndugu Wananchi,

Jitihada za kuendeleza uchumi wa buluu unaojumuisha sekta kuu za utalii, uvuvi, ukulima wa mwani, ufugaji wa mazao ya baharini, bandari, mafuta na gesi asilia pamoja na biashara zinazohusiana na usafiri wa majini zimeanza kupata mafanikio.

Sekta ya utalii imeendelea kupewa mazingatio makubwa kutokana na mchango wake katika kutupatia fedha za kigeni na ajira. Idadi ya watalii wanaoingia nchini imeendelea kuongezeka ambapo katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2025, jumla ya watalii 816,438 wameitembelea Zanzibar, sawa na ongezeko la asilimia 27 ya watalii waliotembelea nchini katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2024. 

Katika kuimarisha sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar, Serikali inadhamira ya kuendeleza utalii wa matamasha ya michezo na utamaduni, makongamano na mikutano ya kimataifa pamoja na kuendeleza urithi wa majengo ya kale na utamaduni Pamoja na vivutio vya maumbile yakiwemo mapango ya kale na misitu ya asili.

Ndugu Wananchi, 

Tumeimarisha sekta ya uvuvi, ukulima wa mwani na ufugaji wa mazao ya baharini ili kuongeza tija katika shughuli hizi na kuchangia ukuaji wa uchumi. Katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Nane, Serikali iliwapatia wananchi vifaa vya kufanyia kazi zikiwemo boti za uvuvi na kilimo cha mwani, vifaranga vya samaki na majongoo bahari kwa wafugaji wa mazao ya baharini, mikopo kwa ajili ya mitaji, mafunzo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya uvuvi yakiwemo madiko na masoko ya kisasa ya kuuzia samaki ili wawe na mazingira mazuri ya kufanyia shughuli zao.

Mafanikio yamepatikana kwa kuongezeka samaki wanaovuliwa kwa zaidi ya asilimia 110 kutoka tani 38,107 za samaki mwaka 2020 hadi tani 78,943 mwaka 2024. Mapato yameongeza kutoka TZS bilioni 205.35 mwaka 2020 hadi TZS bilioni 618 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 201. Aidha, uzalishaji wa zao la mwani umeongezeka kwa asilimia 120 kutoka tani za mwani mkavu 8,785 zenye thamani ya TZS bilioni 5.387 mwaka 2020 hadi tani 19,716 zenye thamani ya TZS bilioni 16.41 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 94. Sekta hizi kwa pamoja zinatoa ajira za moja kwa moja kwa takriban wananchi 100,000.

Lengo la Serikali ni kuendelea kuziimarisha sekta hizi kwa kuwawezesha wavuvi, wakulima wa mwani na wafugaji wa mazao ya baharini. Serikali itaendelea kutoa vifaa vya kufanyiakazi, mafunzo na mikopo nafuu kwa ajili ya mitaji. Aidha, tutaendelea na ujenzi wa miundombinu ya uvuvi kwa kujenga madiko na masoko ya samaki katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.

Ndugu Wananchi, 

Serikali itaendelea kuliimarisha zao la mwani kwa kuongeza uzalishaji, kuimarisha utendaji wa Kampuni ya mwani katika kuwasaidia wakulima kupata bei nzuri na soko la uhakika, kuliongezea thamani zao la mwani na kuendeleza jitihada za Serikali za kuwezesha kuanza kazi kwa kiwanda cha kusarifu mwani cha Chamanangwe. Aidha, tutakiimarisha kituo cha uzalishaji wa vifaranga vya samaki na majongoo bahari Beit ras ili kuongeza kasi katika maendeleo ya ufugaji wa samaki na mazao ya baharini.

Kadhalika, Serikali itaendeleza jitihada za kushughulikia sekta ya mafuta na gesi asilia kutoka hatua ya sasa ya ugawaji na kuvitangaza vitalu 10 vya mafuta na gesi asilia kwa wawekezaji wa kimataifa. 

Ndugu Wananchi, 

Juhudi kubwa zimefanywa katika kuimarisha huduma za bandari zetu na usafiri wa bahari kwa kuzingatia umuhimu wake kwa uchumi wa Zanzibar ambayo ni nchi ya kisiwa. Kwa upande wa bandari, kazi ya ujenzi wa bandari jumuishi ya kisasa ya Mangapwani yenye uwezo wa kuhudumia makontena 250,000 TEUs na mizigo ya tani 1,000,000 imeanza. Ujenzi wa bandari hii unaotarajiwa kumalizika mwaka 2028. Kukamilika kwa mradi huu, kutaleta mapinduzi makubwa ya huduma za bandari hapa Zanzibar. 

Awamu ya kwanza ya ujenzi wa bandari ya Shumba umekamilika kwa kujenga gati yenye urefu wa mita 45 na upana wa mita 20. Ujenzi wa bandari ya Fumba wa kujenga gati yenye urefu wa mita 350 kuelekea baharini pia umeshaanza. Aidha, awamu ya kwanza ya ujenzi wa bandari ya abiria ya kisasa na mizigo katika eneo la Maruhubi nao umeshaanza. Mradi huo utahusisha ujenzi wa bandari ya meli za mizigo na abiria ujenzi wa jengo la abiria lenye uwezo wa kuchukua abiria 1,500, ujenzi wa ghala la kuhifadhia mizigo na ujenzi wa jengo la mizani na njia.

Ndugu Wananchi, 

Huduma za usafiri wa bahari zimeendelea kuimarishwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi. Safari za meli za ndani zimeongezeka kutoka safari 5,696 mwaka 2023/2024 hadi kufikia safari 8,192 mwaka 2024/2025. Idadi za safari za meli za kigeni imeongezeka kutoka meli 98 mwaka 2023/2024 hadi meli 205 mwaka 2024/2025. Ongezeko hilo la meli za kigeni linaashiria kuzidi kuimarika kwa shughuli za biashara ya kimataifa kupitia usafiri wa baharini.

Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, jumla ya meli za ndani 87 zimesajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini na jumla ya meli 613 za Kimataifa zimesajiliwa. Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Baharini imefanikiwa kuongeza mapato kwa kukusanya jumla ya TZS bilioni 8.223 ikilinganishwa na TZS bilioni 6.435 zilizokusanywa mwaka 2023/2024.

Ndugu Wananchi, 

Serikali inazingatia umuhimu wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo barabara na viwanja vya ndege kutokana na umuhimu wake katika kuchochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji. Ujenzi wa miundombinu ya barabara ni hatua muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi. Mafanikio makubwa yamepatikana nchini katika jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya barabara kuu na za ndani kwa mijini na vijijini. Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, Serikali imekamilisha ujenzi wa km 82.887 wa Barabara za mjini na km 247 wa Barabara za vijijini kwa kiwango cha lami na zege. Sambamba na hilo, Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la juu (flyover) la Mwanakwerekwe, daraja la juu (flyover) la Amani kwa asilimia 30, daraja la Uzi - Ngámbwa kwa asilimia 70 na daraja la Pangatupu kwa asilimia 90. Utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea kwa kasi na unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika Uchumi wa nchi yetu.

Ndugu Wananchi, 

Mageuzi makubwa yamefanyika katika kuimarisha huduma za viwanja vyetu vya ndege na yamepata mafanikio makubwa. Idadi ya abiria wanaotumia viwanja vyetu vya ndege imeongezeka kutoka 2,133,166 mwaka 2023/2024 hadi kufikia abiria 2,578,025 mwaka 2024/2025. Aidha, idadi ya mizigo iliyohudumiwa katika Uwanja wa Ndege wa AAKIA imeongezeka kutoka tani 4,224 mwaka 2023/2024 hadi tani 4,603 mwaka 2024/2025. 

Ujenzi wa jengo jipya la pili la abiria (TB2) unaendelea na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 4. Ujenzi huo umefikia asilimia 71 ya utekelezaji. Aidha, utanuzi na ukarabati mkubwa wa jengo la Terminal One kwa ajili ya VIP na ndege binafsi, unaendelea na umefikia asilimia 99 ya utekelezaji. Kwa upande wa uimarishaji wa uwanja wa ndege wa Pemba, kazi ya kuongeza urefu wa barabara ya kutua na kurukia ndege, ujenzi wa jengo jipya la abiria na uwekaji wa miundombinu itakayowezesha uwanja huo kuhudumia ndege za Kimataifa imeshaanza. 

Ndugu Wananchi, 

Serikali imefanikiwa katika kusimamia na kuendeleza sekta ya ardhi na maakazi hapa nchini. Tunapoadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi, Serikali imefanikiwa kuimarisha sekta ya ardhi kwa kuandaa hati za matumizi ya ardhi 1,577 Unguja na Pemba na kuimarisha upatikanaji wa mikataba ya ukodishwaji ardhi 399 ili kuendeleza shughuli za uwekezaji. Aidha, jumla ya viwanja 961 vimepimwa kwa ajili ya maeneo ya makaazi, matumizi ya taasisi, mashamba, eka na maeneo ya vitega uchumi. Pia, maeneo 1,264 ya Serikali yamepimwa. Kwa kuzingatia mipango miji, Serikali imeendelea kuimarisha miji mitano ikiwemo Kisakasaka, Maungani na Makunduchi kwa Unguja na Mvumoni na Kojani kwa upande wa Pemba.

Katika kuimarisha ujenzi wa makaazi bora na majengo ya biashara, Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba 288 za makaazi na biashara katika eneo la Kisakasaka C, ujenzi wa nyumba 1,095 za bei nafuu kwa awamu ya kwanza Chumbuni na ujenzi wa jengo moja la nyumba za makaazi 22 katika eneo la Mombasa kwa Mchina. Aidha, matayarisho kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 548 za makaazi na biashara Kisakasaka B, ujenzi wa nyumba za makaazi Saateni na majengo ya biashara na makaazi Mfikiwa na Mabaoni Pemba yameshaanza kwa hatua za awali. Katika eneo la Kiembesamaki, Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la ghorofa 5 la makaazi na biashara lenye nyumba 22. Lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaishi katika makaazi bora ya bei nafuu na yaliyozingatia sheria za mipango miji na yenye kukuza haiba ya miji yetu.

Ndugu Wananchi, 

Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta ya kilimo inayojumuisha ukulima wa mazao ya chakula na biashara, mifugo na maliasili za misitu, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbali mbali za kuimarisha sekta hii inayoajiri takriban asilimia 35 ya wananchi na kutegemewa katika kujikimu kimaisha kwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi. Tunapoadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi, tumepata mafanikio kwa kuongezeka kwa tija katika kilimo cha mpunga baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde saba 7 Unguja na Pemba yenye ukubwa wa jumla ya hekta 1,325 na kuyagawa kwa wakulima. Serikali inalengo la kuongeza uzalishaji wa mpunga kufikia tani 15 kwa hekta kwa mwaka kwa kuimarisha huduma ya ugani, kuwapatia wakulima pembejeo na vifaa vya kisasa vya kilimo ili kufikia lengo la kuwa na uhakika wa chakula, sambamba na kukamilisha ujenzi na ukarabati kwa maghala ya kuhifadhia chakula. Aidha, jitihada za kuimarisha mazao ya biashara, mboga na matunda zitaendelezwa ili kuongeza tija inayotokana na mazao hayo. Jitihada za makusudi zitafanywa katika kuliendeleza zao la karafuu kutokana na umuhimu wake kama zao kuu la uchumi wa Zanzibar. 

Kwa upande wa mifugo, Serikali itaendeleza juhudi kwa kushirikiana na wawekezaji na wafugaji ili kuongeza idadi ya mifugo kwa ajili ya upatikanaji wa nyama, mayai, maziwa na kuku. Tutaongeza jitihada katika udhibiti wa magonjwa ya mifugo, kwa kuimarisha vituo vya utibabu wa wanyama na huduma za ugani. Aidha, juhudi zitafanywa za kuhakikisha wafugaji wanapatiwa mafunzo ya ufugaji wa kisasa wenye tija na upatikanaji mbegu za mifugo zenye ubora ili wafanye shughuli zao kwa tija.

Pia, Serikali itaendeleza juhudi za uhifadhi wa misitu na miti ya asili ili kuongeza manufaa yanayotokana na rasilimali za misitu. Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika ulinzi wa misitu ya hifadhi na kuhakikisha wananufaika na rasilimali hizo na pia kuwahamasisha katika upandaji wa miti ili kutunza mazingira na miti ya asili na matunda kwa ajili ya matumizi endelevu.

Ndugu Wananchi, 

Kwa lengo la kuleta Mapinduzi ya kiuchumi kwa wananchi, Serikali imechukua hatua za kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kupambana na umaskini na kujiongezea kipato. Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, jumla ya mikopo 6,238 yenye thamani ya TZS bilioni 50.773 imetolewa na Wakala wa Uwezeshaji wa Wananchi kiuchumi kwa wananchi 27,563 (Wanaume 10,917 na Wanawake 16,646). Mikopo hiyo imetolewa kwa sekta mbali mbali zikiwemo kazi za mikono, kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo, huduma za chakula na huduma za kifedha. 

Katika kuwapatia mazingira bora ya kufanyia kazi wafanya biashara wadogo na wajasiriamali, Serikali imekamilisha awamu ya mwanzo ya ujenzi wa masoko makubwa manne katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambayo yameanza kutumika pamoja na ujenzi wa masoko madogo (11) na karakana za wajasiriamali katika Wilaya zote za Unguja na Pemba. Tayari ujenzi wa soko la mboga la Mombasa umekamilika na limefunguliwa katika maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi. Serikali itaendelea na ujenzi wa masoko mpya ya kisasa katika maeneo mbali mbali yakiwemo kwa Haji Tumbo na Kibandamaiti kwa Mjini na yale yanayojengwa na Mabaraza ya Miji na Halmashauri ili kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuwa na masoko ya kisasa yenye mazingira mazuri ya kutolea huduma.

Ndugu wananchi

Katika kukabiliana na changamoto za ajira hasa kwa vijana, Serikali inaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia vikundi vipya 1,293 vilivyoanzishwa na klabu za vijana zenye wanachama 3,799. Jumla ya miradi 37 ya vijana yenye thamani ya TZS bilioni 28.9 imetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na wadau wa maendeleo ikihusisha ubunifu wa kidigitali, kilimo, lishe, stadi za maisha na ujasiriamali. Katika kipindi hiki, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na uzalishaji kwa vijana 500 na kuwaunganisha na fursa za masoko kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi. 

Ndugu Wananchi, 

Uimarishaji wa huduma wa jamii ikiwemo elimu, afya na maji safi na salama ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Serikali imeifanya sekta ya elimu kuwa kipaumbele kwa kuzingatia umuhimu wake katika kuandaa nguvu kazi na kuchochea maendeleo ya nchi yetu. Mageuzi makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya elimu ya ujenzi wa Skuli za kisasa zikiwemo za ghorofa 35, upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia, na kufundishia, vifaa vya maabara za masomo ya sayansi na teknolojia, ajira mpya za walimu na kuwapatia mafunzo, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mazingira ya Skuli na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya Taifa.

Kwa lengo la kuendelea kuimarisha sekta ya elimu, Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa kujenga Skuli za kisasa za ghorofa ili kukabiliana na changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani.

Katika kwenda sambamba na mageuzi ya elimu wa mtaala mpya, jumla ya Skuli 70 zitaunganishwa na mkonga wa mawasiliano, kompyuta 2,000 za mezani zitatolewa kwa ajili ya maabara za Skuli, laptop 4,000 zitatolewa kwa ajili ya wanafunzi na kuanzisha smart classrooms 25 ili kuimarisha kujifunza na kufundisha kwa kutumia TEHAMA. Kwa mwaka 2025/2026, Serikali imepanga kuajiri walimu wapya 1,500 ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi. Aidha, tutaendeleza ujenzi wa dakhalia za wanafunzi na utoaji wa mafunzo ya walimu ili kuwaongezea maarifa pamoja na kuimarisha maslahi yao. Vile vile, tunaongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwezesha wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu kutapa huduma hiyo kwa uhakika. 

Ndugu Wananchi, 

Kwa upande wa sekta ya afya, tumepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta hii kwa kuimarika kwa mfumo wa rufaa na kuanza kazi kwa hospitali za Wilaya zote 11 na hospitali moja ya Mkoa wa Mjini Magharibi zenye huduma bora za tiba na uchunguzi wa maradhi baada ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya. Aidha, Serikali iliongeza idadi ya watumishi wa kada mbali mbali za afya na kufanya ukarabati na ujenzi wa vituo vipya vya afya na ujenzi wa nyumba za makaazi za watumishi.

Lengo la Serikali ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuendelea kujenga miundombinu bora ya afya na kuboresha huduma za afya nchini. Serikali inaendelea kuimarisha mfumo rufaa kwa kuendeleza ujenzi wa hospitali ya Mnazi mmoja, hospitali ya rufaa na kufundishia pamoja  na taasisi ya tiba ya saratani Binguni. Aidha, tumeanza hatua za ujenzi wa hospitali tatu za Mikoa.

Tutaendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa kuongeza kiwango cha fedha za bajeti ya dawa. Serikali pia itaendelea kuajiri watumishi wa fani mbali mbali za afya hasa madaktari bingwa na madaktari bingwa wabobezi na wahudumu wa fani maalumu. Tutaendeleza ujenzi wa nyumba za makaazi za wafanyakazi na kuendelea na ukarabati wa vituo 14 vya afya ya msingi, tutaimarisha huduma za chanjo kwa mama na mtoto na mapambano dhidi ya maradhi yasioambukiza. Aidha, Serikali itaimarisha elimu ya afya kwa umma, kuimarisha huduma za Mfuko wa Bima ya Afya na kuongeza ushirikiano na sekta binafsi kwa lengo la kuzidi kuimarisha sekta ya afya Zanzibar.

Ndugu Wananchi, 

Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha upatikanaji, uhifadhi na usambazaji wa huduma za maji safi na salama kwa kuzingatia umuhimu wake kwa maisha ya wananchi wanaoishi mijini na vijijini. Tunapoadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi, tumefanikiwa kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kuongeza visima vya maji kufikia 405 kutoka 308 yenye uwezo wa kuzalisha lita 5,975,197 kwa saa, sawa na lita za maji 143,404,735 kwa siku. Aidha, tumejenga jumla ya matangi ya kuhifadhia maji 87 Unguja na Pemba. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, matangi 25 ya kuhifadhia maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita 144,000,000 yamejengwa kupitia Mradi wa uimarishaji wa Mfumo wa Usambazaji Maji wa Exim Bank ya India na Mradi wa Uimarishaji na Usambazaji Maji Zanzibar wa fedha za ahueni ya Uviko - 19. 

Aidha, Serikali kupitia ZAWA, imeongeza mtandao wa maji na kufikia jumla ya km 2,080 za mabomba. Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, jumla ya wateja wapya 31,357 wamesajiliwa na kuunganishwa na mtandao wa maji.  Pia, baada ya kukamilika kwa mradi wa Exim, jumla ya nyumba 5,820 zimeunganishwa na huduma ya maji. Katika kuhakikisha huduma za maji safi na salama zinazidi kuimarika, Serikali itatekeleza Miradi mengine ikiwemo wa Exim - India, Mradi wa Usambazaji Maji katika kisiwa cha Pemba kupitia taasisi ya KFW ya Ujerumani na Mradi wa Kuimarisha Miundombinu ya Maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi kupitia JICA ya Japan. Aidha, Serikali itatekeleza Mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mradi wa kutatua changamoto ya upatikanaji huduma ya maji katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Ndugu Wananchi, 

Uwajibikaji, nidhamu na maadili ni misingi ya utumishi bora wa umma. Serikali imefanya jitihada kubwa katika kuimarisha utumishi na utendaji wa viongozi na watumishi wa Serikali pamoja na kuhakikisha uwajibikaji, nidhamu, utawala bora na maadili ya utumishi yanazingatiwa. Jitihada za kukabiliana na vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi zimepata mafanikio ambapo Serikali kupitia ZAECA kati ya mwezi Januari hadi Disemba 2025, imefanikiwa kuokoa jumla ya TZS bilioni 6.687 na Dola za Kimarekani 94,370. Kesi za wahusika wa vitendo hivyo, zipo katika hatua mbali mbali kwa mujibu wa sheria.

 Aidha, Serikali kupitia Afisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeendelea kupata mafanikio kwa kufanya ukaguzi kwa njia za kisasa katika Wizara na Taasisi za Umma ikiwemo ukaguzi wa miradi ya kimkakati na ujenzi wa miundombinu ya Serikali ili kuongeza uwazi na kuimarisha matumizi bora ya fedha za Serikali. Ripoti ya Ukaguzi iliyowasilishwa hadharani ya mwaka jana, inatia moyo kuona idadi ya hati safi zimeongezeka. Aidha, makosa yaliyobainika yanachukuliwa hatua za kisheria. Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuzijengea uwezo taasisi zote zinazosimamia utawala bora ili ziweze kufanya shughuli zake kwa mafanikio zaidi.

Ndugu Wananchi,

Kwa upande wa Watumishi wa umma, Serikali imeendelea kuwapatia stahiki zao ikiwemo mishahara na posho mbali mbali, mafunzo na vifaa vya kufanyia kazi pamoja na stahiki nyengine ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi. Serikali imeimarisha matumizi ya miundo ya utumishi ambapo hivi sasa inatumika kwa ufanisi katika kupandisha vyeo, madaraja na marekebisho ya mishahara kuanzia mwaka 2022 jambo ambalo limewezesha kuondoa malalamiko. Serikali imetoa fursa za ajira mpya 742 kati ya Januari - Disemba, 2025 kwa kada maalum ili kuongeza nguvu kazi na kuziba mapengo ya wastaafu katika kuongeza rasilimali watu katika sekta ya Umma. 

Kwa lengo la kupima uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu, Serikali itatoa mikataba ya utumishi na kuweka mifumo maalum ya usimamizi wa nidhamu na utendaji wa watumishi wa umma ili kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kutokuzingatia kanuni na sheria za utumishi.

Kwa upande wa Sekta ya Sheria, mafanikio makubwa yamepatikana katika uimarishaji wa miundombinu ya Sekta ya Sheria kwa ujenzi wa Afisi za mahakama za kisasa za Mikoa na Wilaya, kuzipatia vifaa vya kazi vikiwemo vya kielektroniki na kuajiri watumishi wapya wakiwemo Majaji. Hatua hii kwa kiasi kikubwa imechangia ufanisi katika kuongeza ari na uwajibikaji wa Watendaji katika Mahakama na kuboresha kasi ya upatikanaji haki kwa wananchi. Aidha, kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, kwa ushirikiano na Serikali, jumla ya wananchi 422,908 kutoka Mikoa na Wilaya zote Zanzibar waliweza kupata huduma za kisheria wakiwemo wanawake 209,185 na wanaume 213,723.

Ndugu Wananchi,

Ushirikishwaji wa wananchi katika vyombo vya maamuzi ni msingi muhimu wa demokrasia na utawala bora. Tunapoadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi na kuanza kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Nane, nimeridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Wawakilishi wa wananchi kupitia Baraza la Wawakilishi, Mabaraza ya Miji, Manispaa na Halmashauri zote za Wilaya. Nachukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi na Waheshimiwa Madiwani wa Serikali za Mitaa kwa ushirikiano na uwajibikaji katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Wito wangu kwao tuendelee kushirikiana na kuweka mbele maslahi ya nchi yetu ili Zanzibar izidi kupiga hatua za maendeleo.

Ndugu Wananchi,

Katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanaoishi nchi za nje (Diaspora) wanashiriki katika utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo, Serikali imeanzisha kanzidata ya kidijitali ya kuwaorodhesha na kurahisisha kuwatambua. Lengo ni kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi za idadi ya Diaspora wenye asili ya Zanzibar, nchi wanazoishi, taaluma zao na uwekezaji wao. Hadi kufikia mwezi Disemba 2025, jumla ya diaspora 1,283 wamesajiliwa katika kanzidata. Kwa mujibu wa usajili uliyofanyika kuna jumla ya wawekezaji wakubwa na wadogo 55 waliowekeza miradi mbali mbali hapa Zanzibar ikiwemo ya afya, elimu, ujenzi wa hoteli na miradi mingine ya uchumi.

Kadhalika, kupitia Mfumo wa Sema na Rais (SNR), jumla ya malalamiko 21,725 yamepokelewa kutoka kwa wananchi ambapo malalamiko 19,008, sawa na asilimia 87.5 tayari yamepatiwa ufumbuzi. Malalamiko 2,717, sawa na asilimia 12.5 yanaendelea kushughulikiwa. Nawaomba wananchi waendelee kuutumia Mfumo wa Sema na Rais (SNR) ili kupata ufumbuzi wa changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Ndugu Wananchi,

Sekta ya habari, utamaduni na michezo zina umuhimu mkubwa katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu. Serikali imeendelea kuchukua hatua ya kuimarisha vyombo vya habari vya umma kwa kuvipatia vifaa vya kisasa vya utangazaji na kurushia matangazo, kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa wafanyakazi na kuimarisha utoaji wa maudhui kupitia matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki katika redio na televisheni ya Shirika la habari la Zanzibar (ZBC) na Shirika la Magazeti la Serikali.

Sekta ya Utamaduni na Sanaa imeimarishwa kupitia Matamasha ya muziki na shughuli mbali mbali za kitamaduni pamoja na uendelezaji wa Kongamano la Kiswahili la Kimataifa ambalo linahusisha pia shughuli za utamaduni wa Mswahili na kuhudhuriwa na washiriki kutoka mataifa mbali mbali duniani, hatua ambayo pia imechangia katika kukuza utalii. Hatua za kuendelea kuimarisha sekta ya Sanaa na utamaduni zitaendelezwa ili kudumisha urithi wa Sanaa na utamaduni tulioachiwa na wazee wetu na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Ndugu Wananchi,

Katika kuimarisha sekta ya michezo, Serikali inaendelea na dhamira yake ya kuimarisha sekta hiyo kwa ujenzi wa miundombinu ya michezo. Hivi sasa, ujenzi wa viwanja 17 vya michezo unaendelea kukamilishwa kwa hatua mbali mbali katika Wilaya na Mikoa yote Unguja na Pemba. Hatua hiyo ni baada ya kukamilika ujenzi wa viwanja vya Amani Complex, Gombani na Mao na viwanja vya michezo vya Maisara. Mafanikio makubwa  yaliyopatikana nchini katika sekta ya michezo, yamepelekea vilabu vikubwa vya Tanzania kuamua baadhi ya michezo yao ya kitaifa na kimataifa kuichezea hapa Zanzibar. Ni matumaini yetu kuwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya michezo ikiwemo uwanja wa michezo wa AFCOM tunaoendelea kuujenga Fumba, utazidi kuchochea maendeleo ya sekta ya michezo kwa kuibua vipaji vya wanamichezo, kukuza utalii wa michezo na kuifanya Zanzibar izidi kufahamika kimataifa. 

Ndugu Wananchi,

Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa Tanzania ni tunu muhimu katika kuimarisha amani, maendeleo na ustawi na Taifa letu. Tunapoadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi, mafanikio makubwa yamepatikana katika  kuimarisha Muungano wa Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii. Serikali zetu mbili zimeendeleza utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano kwa pamoja kwa kuandaa vikao vya mara kwa mara vya kisekta na vya Kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa kipindi cha karibuni, jumla ya hoja 15 za Muungano zimejadiliwa na kuondoshwa na hati 13 za maamuzi zimesainiwa.

Aidha, Serikali zetu zinaendelea kutekeleza kwa ushirikiano zaidi ya miradi 10 ya maendeleo ikiwemo ya miundombinu, uzalishaji na upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi. Kupitia TASAF kwa mwaka 2025, jumla ya miradi 23 ikiwemo 16 ya elimu na 7 ya afya inayohusisha ujenzi wa miundombinu imetekelezwa kwa gharama ya TZS bilioni 4.655. Pia, jumla ya TZS bilioni 56.107 zimetolewa ili kuzisaidia kaya maskini hapa Zanzibar. Aidha, hadi mwezi Septemba 2025, huduma zinazotolewa kupitia Mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF III) zimewafikia walengwa wa Shehia zote 388 za Zanzibar na kuzinufaisha jumla ya kaya 53,636.

Ndugu Wananchi,

Nahitimisha hotuba yangu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi kwa kukushukuruni tena kwa kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano katika Taifa letu na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo kwa mafanikio. Napenda kutumia fursa hii kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Makamo wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu na Viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa. Aidha, nawashukuru wasaidizi wangu Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Watendaji na Watumishi wote wa Serikali, Maafisa na wapiganaji wa vyombo vya Ulinzi na Usalama vya SMZ na SJMT, viongozi wa Dini na Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi na washirika wetu wote wa maendeleo kwa ushirikiano wao katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Shukrani maalum nazitoa kwa Chama changu cha Mapinduzi kwa kuwa pamoja nami katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na ahadi tulizozitoa wakati wa Kampeni.

Wito wangu kwenu tuendelee kushirikiana na kudumisha mafanikio tuliyoyapata kwa kuongeza kasi, uwajibikaji na kufanya kazi kwa uzalendo ili tuweze kuyafikia malengo yetu katika kukuza uchumi, kuimarisha huduma za jamii na ustawi wa nchi yetu kwa ujumla.

Tumoumbe Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamano na atupe uwezo wa kufanikisha utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo kwa mafanikio zaidi. Nakutakieni nyote kila la kheri katika Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

 

MAPINDUZI DAIMA

Ahsanteni kwa Kunisikiliza.