RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hatua ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa imelenga kuwawezesha wananchi kuishi kwa amani na utulivu na hivyo kuharakisha kasi ya kupata maendeleo.Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar, alipozungumza na Uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, uliofika kusalimiana nae.

Amesema uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umeleta ufumbuzi wa changamoto za kisiasa zilizokuwa zikiikabili Zanzibar.Aidha, alisema Serikali inakusudia kuweka nguvu zaidi katika kuyapatia ufumbuzi matataizo mbali mbali ya wananchi yanayowasilishwa kwake, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi alizozitowa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi mkuu wa 2020..

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali itashirikiana Tume hiyo kikamilifu ili iweze kufanikisha vyema majukumu yake na kutimiza matakwa ya Kikatiba.Alipongeza juhudi za Tume hiyo katika kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano ya kimtandao na kuwafikia wananchi wengi zaidi, akibainisha ukubwa wa Tanzania.

Dk. Mwinyi alisema tayari Serikali imeshalipatia ufumbuzi suala la kuwepo uwiano wa nafasi za ajira kati ya vijana wa Tanzania Bara na Zanzibar kupitia vikao vya Kamati ya masuala la Muungano, ambapo hivi sas Zanzibar itapata wastani wa asilimia 21 ya nafasi hizo zilizo katika sekta za Muungano, pale zitakazotangawa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha,  aliahidi kulipatia ufumbuzi tatizo la Ofisi linazoikabili Tume hiyo Unguja na Pemba ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 

Mapema, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania,  Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alisema tangu Rais Dk. Mwinyi kuchaguliwa kuiongoza Zanzibar amethibitisha nia ya dhati ya kuwaunganisha Wazanzibari, baada ya kushirikiana na Chama cha ACT Wazalendo na hivyo kuunda Serikali ya Umoja wa kitaifa.

Alisema kupitia busara zake na kwa kushirikiana na viongozi wa ACT Wazalendo, wananchi wa Zanzibar wameweza kushirikiana na kupiga kasi ya maendeleo.Amesema Uongozi wa Tume hiyo unafarijika na mafanikio makubwa yaliopatikana katika kipindi kifupi cha Uongzozi wa Dk. Mwinyi, ambapo pamoja na mambo mengine alimpongeza kwa kuimarisha na kutekeleza haki za binadamu pamoja na kukuza Utawala bora.

Jaji Mwaimu alisema suala la kupokea malalamiko ya wananchi lipo katik Ofisi nyingi za Serikali, hivyo hatua yake ya   kufungua milango na kusikiliza malalamiko ya wananchi yeye mwenyewe ni jambo jema linalolenga kuondokana na vikwazo vinavyoweza kujitokeza.

Alisema Tume hiyo imefanya ziara na kukutana na viongozi mbali mbali kwa lengo la kujenga mashirikiano na kufanyakazi pamoja ana Serikali

“Sisi utendaji wetu unazingatia Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, tunahakikisha Serikali inatetekeleza vizuri majukumu yake ili wananchi waweze kupata haki zao”, alisema.Aidha alisema hatua ya Rais Dk. Mwinyi kukutana na makundi mbali mbali ya kijamii, ikiwemo wazee na walemavu ni hatua nzuri katika kuendeleza Utawala bora.

Jaji Mwaimu alimpongeza Dk. mwinyi kwa juhudi zake za mapambano dhidi ya vitendo vya Rushwa pamoja na kuimarisha taasisi zinazosimamia suala hilo, sambamba na hatua zake za kuwawajibisha Viongozi wasiozingatia Utawala Bora.Aidha, alimpongeza kwa usimamizi na matumizi ya mapato ya Serikali, akibainisha jukumu la Serikali katika usimamizi na matumizi ya mapato ili kuziba mianya ili kuharakisha kasi ya maendeleo. 

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Mwinyi kwa azma yake ya kuimarisha uchumi wa Zanzibar, kupitia uchumi wa Buluu na kusema ni jambo muhimu kwa kuzingatia kuwa Zanzibar ni nchi ya visiwa, hivyo yaweza kupata maendeleo ya haraka kupitia miradi mbali mbali.Aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutatua baadhi ya changamoto, ikiwemo ya kuongeza fedha za bajeti an hivyo kuijengea uwezo wa kufanya kazi Tume hiyo.

Vile vile, aliziomba Serikali zote mbili (SMT na SMZ) kubuni utaratibu utakaowezesha kuwepo uwiano wa nafasi za Ajira katika sekta za Muungano.