SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inathamini sana mchango wa fani za Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar kwenye utekelezaji wa mipango mikubwa ya Maendeleo hasa miradi ya ujenzi.Imesema itaendelea kuwahusisha kikamilifu kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa kuzingatia dhana ya ushirikishwaji wa wataalamu wa Kitanzania katika miradi endelevu ya kimkakati ya uwekezaji nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozindua taasisi ya wasanifu, wahandisi na wakadiriaji Zanzibar, kwenye ukumbi wa hoteli Verde, Mtoni Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.Amesema, kwa kiasi kikubwa Serikali ilijitahidi kuzitumia kampuni za ndani kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali hasa wakati wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya fedha za UVICO zilitumika kampuni za ndani (wazawa) kwa lengo la kuwajengea uwezo ili wapate miradi mikubwa zaidi.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza miradi yote ilikamilika kwa ufanisi hali ya juu zaidi.Alisema, Serikali zote mbili za (SMZ) na (SMT) zinafanya jitihada za makusudi kushirikisha taaluma hizo kwenye shughuli tofauti za maendeleo, ikiwemo kuweka mazingira yanayowawezesha kujiajiri, kuhamasisha utambuzi wa fursa mbalimbali kupitia rasilimali zilizopo nchini pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya kufanikisha utafiti na ubunifu mbalimbali.
“Tunajua tunahitaji kushirikiana ili kufanikisha dhamira ya Maendeleo Endelevu hususan fani hizi kutokana na umuhimu wake kwa ustawi wa nchi yetu”. Alieleza Rais Dk. Mwinyi.Vilevile Dk. Mwinyi alieleza hizo ni uti wa mgongo wa shughuli nyingi za uchumi wa nchi kwani zinabeba dhima ya shughuli-mama katika harakati za kujenga, kuimarisha na kuendeleza maendeleo ndio maana Serikali inazipa mazingatio makubwa.
Alisema Serikali pia imefungua njia kwa fani hizo kuwa na uthubutu na kujiamini sambamba na kuwasihi wahandisi hao kuendelea kuongeza juhudi ili kazi zao zizidi kuchangia kiasi kikubwa cha kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.Dk. Mwinyi alisema Tanzania ni nchi inayoendelea na inajivunia kufikia Uchumi wa Kati, kutokana na kuwa na miradi inayochangia zaidi pato la Taifa, nyuma yake wakiwepo wenye fani za usanifu, uhandisi na ukadiriaji wa ujenzi.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza, Serikali ya Zanzibar kupitia Uchumi wa Buluu imeendeleza Sera ya kuajiri wasanifu, wahandisi na wakadiriaji wazalendo ikiamini kuna wakandarasi wazuri na washauri elekezi mahiri (wazawa) wenye uwezo mkubwa wa kufanyakazi za uhandisi kwa weledi kupitia miradi mbalimbali waliyoitekeleza kwa ufanisi mkubwa ni kielelezo cha kuaminika kwao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salim Mohamed amesema Sekta ya majengo na ujenzi Zanzibar iko kwenye mageuzi makubwa kwa kasi kubwa ya ujenzi inayoendelea nchi nzima zikiwemo barabara za mijini na vijijini, ujenzi wa skuli za ghorofa maeneo yote ya visiwa vya Unguja na Pemba, ujenzi wa hospitali kwa wilaya zote nchini ujenzi wa nyumba za makaazi miundombinu ya maji safi na salama pamoja na umeme.
Alisema hatua hiyo inatokana na dhamira njema na maono ya Rais Dk. Mwinyi katika azma yake ya kuibadilisha Zanzibar na mandhari na haiba nzuri ya maendeleo endelevu.Alizipongeza juhudi za wahandisi wote kwa ushiriki wa wao mkubwa wa mageuzi yanayoendelea nchini chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi, kupitia sekta ya ujenzi na miundombinu.Alisema, maisha ya kila siku yanategemea mchango na ushiriki mkubwa wa wahandisi.
Dk. Khalid alifafanua makaazi ya watu wanayoishi, ofisi na mawasiliano yao, nishati za umeme, madaraja na barabara wanazozitumia, maji safi na salama na shughuli zote za jamii zina mnasaba mkubwa na kazi za wahandisi.Hivyo, alileleza kuundwa kwa taasii ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar ni kielelezo muhimu cha kukuza uwezo wao katika kuimarisha sekta ya ujenzi kwa maendelo ya nchi.
Naye, Rais wa Taasisi ya Wasanifu Wahandisi na Wakadiriaji Zanzibar, QS. Abduswamad Mohamed Mattar amesema taasisi hiyo ilimedhamiri kufanya makubwa zaidi kama mchango wao kwa taifa na kuadhimia kuwa na wanachama wengi ambapo kwa sasa kuna wanachama 192. Hivyo. Aliwashauri wataamu wa fani hizo kuendelea kushirikaina na kujiunga kwa wingi wao ili kushajihishana zaidi.
Aidha, alieleza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kushirikiana na taaasiisi mbalimbali za ujenzi ndani na nje ya nchi ikiwemo kutayarisha mafunzo nao kujifunza zaidi mageni wasiyoyajua sambamba na kusaini hati tofauti za makubaliano kwa taasisi mbalimbali za wahandizi bara na visiwani.