RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kazi ya Misikiti sio kufanywa ibada za sala pekee, bali ni sehemu bora ya kutoa elimu kwa jamii na kituo kizuri cha kuwafunza vijana mambo ya kheri.Al hajj Dk. Mwinyi, aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa Masjid Al-Abraar - Kijiji cha Tazari Mkoa wa Kaskazini Unguja, mara baada ya Ibada ya Sala ya Ijumaa aliyojumuika pamoja na waumini wa Kiislam wa Kijiji hicho na maeneo jirani.

Alisema, mbali ya misitiki kutumika kwa kazi kubwa ya kufanyiwa ibada pia inajukumu la kutatua changamoto zinazoikumba jamii wakiwemo wajane, watu wenye uhitaji baadhi yao wanaoishi kwenye mazingira magumu, watoto yatima na watu masikini sana kwa kupata usaidizi wa jamii ziliouzunguka msikini huo.

Alhajj Dk. Mwinyi pia aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza kukithirisha ibada wakati wote kwani Mwenyezi Mungu yupo kila siku, hivyo aliwataka waumini hao kuziendeleza wakati kama walivyojitahidi kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na siku za Ijumaa.

Akizungmzia kuhusu hifadhi ya kitabu kitukufu cha Quran, Al hajj Dk. Mwinyi alisema ufunguzi wa Masjid Al-Abraar – Kijijini Tazari utakua kituo kikubwa cha kuwafunza vijana Quran kwa njia ya takhfidh, alisema, Zanzibar imepiga hatua kubwa na yakusifiwa kwenye eneo hilo, ambalo lilijidhihirisha wazi wakati wa Mwezi mtukufu wa Ramadhan vijana wengi walihifadhi Quran kwa njia za Takhfidh na Tajuwiid.

Pia, Alhajj Dk. Mwinyi aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza umoja, mshikamano na upendo baina yao pamoja na kuwashukuru wafadhili waliojenga msikiti huo.Vilevile, aliwasihi waumini wa msikiti huo kuitunza na kuikarabati na kuipatia huduma zote kadri itakavyohitaji ili usichakae haraka.

Mapema, akizungumza kwenye ibada hiyo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume alisema, Masjid Al-Abraar wa Kijiji cha Tazari Mkoa wa Kaskazini Unguja unakuwa wa msikiti wa 30 kufunguliwa na Alhajj Dk. Mwinyi ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, pia Alhajj Dk. Mwinyi amejumuika na wananchi na waumini wa dini ya kiislamu kwa ibada ya pamoja na sala ya Ijuma kwenye misikiti 170 ya Unguja na Pemba sambamba na kusaidia kutatua matatizo mengi ya misikiti hiyo.

Sheikh Khalid aliongeza kuwa, Al hajj Dk. Mwinyi ameshishiriki ijitimai zisizopungua tano kwa maeneo tofauti pamoja na kuendelea kujumuika na waumini wa Kiislam na wananchi wa Zanzibar kwenye sala na mabaraza ya Eid kwa nyakati tofauti za uongozi wake.Hivyo, aliwasihi waumini hao na wananchi kuendelea kumuungamkono Rais Dk. Mwinyi pamoja na kuendelea kumuombea dua njema kwenye majukumu yake ya kila siku.

Wakisoma risala na historia fupi za msikiti huo, mmoja waumini msikitini hapo, Shheikh Mohamed Wadi alisema, ujenzi wa msikiti huo ulianza mwaka 2022 baada ya msikiti wa awali kuchakaa sana hadi walipopata mfadhili aliewajengea ambao unatarajiwa kuwa wa ghorofa tatu.

Alisema Msikiti huo unatarajiwa kuwa kituo kikubwa cha kuhifadhia na kufundishia Quran kwa wakaazi wote wa vijiji vya Tazari, Kidoti na jimbo lote la Nungwi,  Mkoa wa Kaskazini pamoja na kutumika kwa mahitaji mbambali ya jamii sambamba na kuahidi kuutunza vyema.

Naye, Khatibu wa sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Salum Hisani alihimiza umoja kuendeleza ukoo pamoja na jitihada za kuitunza na kuisafisha misikiti nyakati zote.