Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba Serikali anayoiongoza ina lengo la kuhakikisha inajenga uchumi imara utakaoleta maendeleo kwa wananchi wote.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar,waliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba siasa ni uchumi na siasa ikiwa nzuri na uchumi nao huimarika, hivyo juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha kunajengwa uchumi ulio imara na madhubuti.Aidha, Rais Dk. Miwnyi aliwaeleza wazee hao mipango na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta za maendeleo ili kuhakikisha uchumi unazidi kuimarika pamoja na vijana kupata ajira na Serikali nayo kupata mapato.Alisema kuwa jambo kubwa na la msingi katika kuhakikisha Zanzibar inaendelea kupata maendeleo na kuujenga uchumi wake kuwa imara ni kuwepo kwa amani na utulivu, juhudi ambazo zimechukuliwa katika kuhakikisha hilo linafanyika.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kulipongeza Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, kwa kuendeleza utamaduni wao wa kukutanan na kiongozi aliyoko madarakani kwa azma ile ile ya kuzungumza na kubadilishana mawazo.Alitoa shukurani kwa dua wanazozifanya wazee hao mara kwa mara kwa viongozi wao na kwa nchi yao na kuwasisitiza haja ya kuendelezwa kwa utaratibu huo.

Dk. Mwinyi pia, aliwaeleza wazee hao juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza za kuhakikisha jengo la kihistoria la Beit al Jaib linajengwa upya na kurudi katika hadhi yake ya asili ujenzi ambao unatarajiwa kuanza rasmi hapo Febuari mwakani.Pia, Rais alieleza hatua za Serikali katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma za Bima ya Afya ili iwe rahisi kupatikana kwa huduma za afya.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja na umuhimu wa kuijenga upya nyumba ya Kijangwani iliyokuwa Afisi ya ASP ambayo kwa sasa imebomoka kwa azma ya kuhakikisha historia haipotei.

Mapema akisoma Tamko la Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Mzee Haji Machano alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2020 pamoja na ushiriki kabambe wa kampeni alizozifanya za uchaguzi huo.Baraza hilo lilieleza kufarajika na kazi aliyoanza kuifanya wakati alipoingia madarakani kwani uongozi wake wameifurahia ikiwa ni pamoja na kuzunguka katika Wilaya zote za Unguja na Pemba na kukagua maendeleo pamoja na kukutana na wananchi ambao walipata fursa ya kueleza matatizo wanayoyakabili.

Pamoja na hayo, Baraza hilo lilimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa juhudi zake anazozichukua katika kuiongoza Zanzibar na kuiweka katika hali ya usalama, amani na utulivu.

“Umekemea rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, umerekebisha mfumo mzima wa elimu na kukarabati utawala, umekemea ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, umechukizwa sana na uingizaji na utumiaji dawa za kulevya nchini na umeunda chombo cha udhibiti na ufuatiliaji, umepanua uchumi wa buluu na kuiweka Wizara maalum ya shughuli hizo, umewaita wawekezaji”,alisema sehemu ya Tamko hilo.

Aidha, Baraza hilo lilitoa ushauri kwa Rais Dk. Mwinyi ikiwa ni pamoja na kushauri kwa kujengwa nyumba ya ASP, iliyopo kijangwani ambayo ina historia kubwa pia, walishauri kujengwa kwa jengo la Bait el Jaib, kuongeza kasi ya kupiga vita vitendo vya ukatili, ubakaji, udhalilishaji wa watoto na wanawake, uingizwaji wa dawa za kulevya pamoja na kupambana na maradhi ya miripuko.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Wawekezaji wa Kampuni ya Sukari Kilombero wakiongozwa na Balozi Ami Ramadhan Mpungwe ambapo ambao wapo hapa Zanzibar kwa ajili ya mkutano wa Kampuni hiyo wenye lengo la kupanua shughuli na uzalishaji wa Kampuni hiyo ambapo Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza kwa kuamua kufanya mkutano huo hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza waekezaji wa wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombera Dira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uchumi wake ambapo imelenga katika Uchumi wa Buluu na kueleza fursa zilizopo katika uchumi huo huku akiwakaribisha wawekezaji hao kuja kuekeza sambamba na kuwa Mabalozi wa kuitangaza Zanzibar kiuwekezaji.