Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Mwinyi, leo tarehe 5 Oktoba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria, Mhe. Balozi Hamisu Umar, Ikulu Zanzibar.

Mhe. Rais Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumweleza Balozi Hamisu Umar kuwa Zanzibar iko tayari na inawakaribisha wawekezaji wa Nigeria kuja kuwekeza visiwani Zanzibar katika sekta mbalimbali za Uchumi wa Buluu ikiwemo Gesi na Mafuta ya Baharini, Viwanda vya kuchakata Samaki, Miradi ya Bandari pamoja na Utalii wa Mahoteli.

Kwa upande wake, Balozi Hamisu Umar, amempongeza Mhe. Rais Dk. Mwinyi kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuitangaza na kuijenga Zanzibar hususani katika sekta ya Uchumi wa Buluu ambayo amesema ni ubunifu mzuri kwenye kujenga uchumi wa taifa lililozungukwa na bahari.

Wakati huo huo, Mhe. Rais amekutana na kuzungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Suleiman Jafo. Mhe. Rais Dk. Mwinyi ameelezwa kuridhishwa na kasi ya utatuzi wa kero na changamoto za Kimuungano ambapo amemuelekeza Waziri Jafo kuendelea kuhakikisha kero na hoja mbalimbali zinaendelea kufanyiwa kazi kwani changamoto huwa haziishi katika jambo lolote.

Naye Mhe. Jafo amemueleza Mhe. Rais juu ya hatua mbalimbali zinazoendelea za wizara yake ambayo inashughulikia masuala ya Muungano ambapo mpaka sasa kero na changamoto zipatazo kumi na nane(18) zimekwishapatiwa ufumbuzi kati ya 25.

Aidha, Mhe. Jafo ameongeza kuwa, hivi sasa Wizara za pande zote mbili za Muungano zipo katika hatua za mazungumzo ya kumalizia hoja 7 zilizosalia ambazo wanatarajia zitamalizika ndani ya kipindi kifupi kijacho