Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na uongozi wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) uliofika Ikulu, Zanzibar leo tarehe 30 Machi 2026. Ujumbe huo ulioongozwa na Rais wa chama hicho, Dkt. Mary Mwanyika Sando, umewasilisha dhamira ya kuandaa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Vyama vya Madaktari Wanawake Afrika, unaotarajiwa kufanyika Zanzibar tarehe 05 Mei 2027. Mkutano huo unatarajiwa kuwashirikisha madaktari takriban 400 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Akizungumza katika kikao hicho, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kufanyika kwa mikutano ya kimataifa nchini ni tija kubwa na fursa muhimu ya kuitangaza Zanzibar kimataifa pamoja na kuimarisha sekta ya utalii. Ameeleza kuwa washiriki wa mikutano hiyo huwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Zanzibar wanaporejea katika nchi zao.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza juhudi za MEWATA kwa kuamua kuandaa mkutano huo Zanzibar, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya na uchumi kwa ujumla. Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kushirikiana na MEWATA ili kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa mkutano huo unafanikiwa kwa kiwango cha juu.
