Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja katika futari ya pamoja aliyowaandalia.
Hafla hiyo ya futari imefanyika leo, tarehe 14 Machi 2026, katika viwanja vya Ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Rais Dkt. Mwinyi amewashukuru viongozi, waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi wote waliohudhuria futari hiyo, aliyoielezea kuwa ni jambo jema lenye heri linalowakutanisha na kuwaunganisha wananchi wa makundi mbalimbali.
Rais Dkt. Mwinyi amehitimisha utaratibu wake wa kufutari na wananchi katika mikoa yote mitano ya Zanzibar, utaratibu anaouendeleza kila mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhi sadaka ya futari kwa Jumuiya ya Watu Wasioona, iliyotolewa na Jumuiya ya Zanzibar International Development Organization (ZIDOM).