Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kilimo cha mwani kinaongezewa thamani na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Machi 2026, alipokutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya TSC Purple Limited ya India pamoja na ujumbe wake waliofika Ikulu, Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi ameueleza ujumbe huo kuwa Serikali imeliweka zao la mwani kuwa miongoni mwa mazao ya kipaumbele kutokana na kuwashirikisha wananchi wengi.Amesema lengo ni kuhakikisha wanapata manufaa ya kazi ngumu wanayoifanya kwa kuliongezea thamani zao hilo kupitia ongezeko la uzalishaji, upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Kampuni ya Mwani ya Zanzibar imekuwa ikinunua mwani kutoka kwa wakulima, lakini haijaweza kufikia malengo yake kutokana na kukosa soko la uhakika, hali inayosababisha wakulima wengi kubaki na mwani mwingi majumbani mwao bila soko. Dkt. Mwinyi ameihakikishia kampuni hiyo ya India kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na taasisi za ndani na za kimataifa kuijengea uwezo Kampuni ya Mwani ya Zanzibar (ZASCO), pamoja na kuwajengea uwezo wakulima wa mwani ili wazalishe mwani bora unaokubalika katika masoko na hivyo kuinua hali zao kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameishauri kampuni hiyo kuweka utaratibu wa kununua mwani ukiwa mbichi kutoka kwa wakulima, hatua itakayowapunguzia gharama za uzalishaji.
Naye Mwenyekiti wa TSC Purple Limited, Dkt. Stefan Kraan, amesema kampuni hiyo inaendelea na ufungaji wa mitambo katika kiwanda cha kusarifu mwani cha Chamanangwe, ambapo hatua hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2026 na kuanza uzalishaji mwezi Septemba 2026. Ameeleza kuwa hatua hiyo italeta mapinduzi makubwa katika kilimo cha mwani Zanzibar, ikiwemo uzalishaji wa mbolea, chakula cha wanyama na dawa.
Aidha, amemueleza Rais Dkt. Mwinyi kuwa kampuni hiyo inatarajia kuandaa mkutano mkubwa wa wadau wa kilimo cha mwani utakaofanyika Tanzania kuanzia tarehe 16 hadi 19 Juni 2026, na baadaye kufanya ziara maalum katika maeneo mbalimbali yanayolimwa mwani Zanzibar ili kubaini fursa mpya za kuendeleza kilimo hicho hapa nchini.
.jpeg)