Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaongoza viongozi wa kitaifa, wanafamilia na wananchi mbalimbali katika dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.Du a hiyo imefanyika leo, tarehe 07 Aprili 2026, katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo pia imehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba,  Mama Fatma Karume na familia yake, Viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali.

Baada ya kisomo hicho maalum, Rais Dkt. Mwinyi pamoja na viongozi na wanafamilia walizuru kaburi la Hayati Sheikh Abeid Amani Karume na kuweka mashada ya maua.Viongozi wengine waliohudhuria kisomo hicho ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah, Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji George Masaju, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda pamoja na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi.

Kumbukumbu hiyo imetimiza miaka 54 tangu Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, tangu kifo chake mwaka 1972. Aidha, dua hiyo imehitimisha Wiki ya Kuwaenzi na Kuwakumbuka Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar waliotangulia mbele ya haki, ambayo huadhimishwa kitaifa kila mwaka.