Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha na kuhifadhi maeneo ya kihistoria kutokana na mchango wake katika uchumi na utamaduni wa Zanzibar. Akizungumza Ikulu Zanzibar leo tarehe 01 Aprili,2026 alipokutana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Mhe. Marjo Crompvoets, Rais Dkt. Mwinyi amesema juhudi hizo ni pamoja na ukarabati wa jengo la kihistoria la Sinema ya Majestic, unaofanyika kwa ushirikiano na Serikali ya Japan, ili kulibakisha katika muonekano wake wa asili na kuongeza matumizi yake kiutamaduni.

Aidha, ameishukuru Uholanzi kwa ushirikiano unaoendelea na kuwataka wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kuwekeza Zanzibar, hususan katika sekta za utalii, uchumi wa buluu, viwanda, uvuvi na kilimo. Kwa upande wake, Mhe. Crompvoets ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na kuongeza uwekezaji, akieleza kuridhishwa na maendeleo ya kiuchumi yanayopatikana Zanzibar.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na Balozi wa Slovakia nchini, Mhe. Ivan Lančarič, na kueleza utayari wa Zanzibar kushirikiana na nchi hiyo katika sekta za uwekezaji, biashara na utalii.

Naye Mhe. Lančarič amesema Slovakia inapanga kufungua ofisi ya ubalozi nchini Tanzania pamoja na ofisi ndogo Zanzibar, ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji