RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHESHIMIWA AL HAJ DK. HUSSEIN ALI MWINYI YA KUUKARIBISHA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI KWA MWAKA 2026 MILADIA, SAWA NA MWAKA 1447 HIJRIA.

Ndugu Wananchi,

Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh

Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujaalia neema ya uhai na kwa kutuwezesha kuifikia siku hii tunapoukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu wa 1447 Hijria, sawa na mwaka 2026 Miladia.

Mwezi wa Ramadhani umetukuzwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mwezi mtukufu kwani amali za waja katika mwezi huu, huwa na fadhila na daraja kubwa. Kwa mnasaba huo,imefaradhishwa kufunga pamoja na kuongeza juhudi katika kutekeleza ibada nyingine za faradhi na sunna kwa wingi ili tunufaike na utukufu wa Mwezi wa Ramadhani. 

Ndugu Wananchi,

Ramadhani ni mwezi ulioteremshwa kitabu kitukufu cha Qurani katika usiku ulio bora zaidi wa Lailatul Qadir, kitabu ambacho ndio muongozo wa dini yetu. Tunafundishwa na kuhimizwa kuwa miongoni mwa ibada bora na muhimu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tunaoukaribisha ni kukithirisha kusoma Qurani na kuzingatia mafundisho yake ili tuweze kupata mafanikio hapa duniani na kesho mbele ya haki.

Natumia fursa hii kuwahimiza waislamu kuendeleza utaratibu wa kuwa na darsa mbalimbali za Qurani na mafunzo mengine katika mwezi wa Ramadhani ili kujiongezea maarifa na kukuza imani zetu pamoja na kutuwezesha kutekeleza ibada kwa usahihi zaidi. Aidha, tuendeleze utamaduni wa kuandaa mashindano ya kuhifadhi Qurani ambayo huchangia kuwawezesha watoto na vijana wetu kufuata mwenendo mwema wa kupenda kusoma na kuhifadhi Qurani na huongeza hamasa ya usomaji wa Qurani ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Nitoe wito kwetu sote tujitahidi kuhudhuria na kushiriki katika mashindano hayo.

Ndugu wananchi,

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa kuchuma fadhila ambazo Mwenyezi Mungu amewaahidi waja wake watakaofanya mema na kujiepusha na makatazo yake. Miongoni mwa mambo mema yanayohimizwa ni kutoa sadaka kwa ndugu zetu wenye uwezo mdogo ili nao waweze kupata mahitaji yao muhimu yakiwemo ya chakula.

Napenda kutumia fursa hii kuwaomba wafanyabishara kutopandisha bei za bidhaa muhimu hasa zile zinazotumika zaidi katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mwezi wa Ramadhani ni kipindi cha kuchuma mema kwa kusaidiana na kuhurumiana mambo ambayo huzidisha mapenzi na kuongeza baraka katika jamii. Ni wajibu wetu kuwafikiria na kuwasaidia wenzetu wasio na uwezo wakiwemo wajane na mayatima ili nao waweze kuupokea vema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Ndugu wananchi,

Serikali kupitia Tume ya Ushindani Halali wa Biashara imefanya ukaguzi kwenye maghala ya kuhifadhia bidhaa muhimu za chakula zikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari na mafuta ya kupikia pamoja na kukagua madukani. Tumejiridhisha kuwa kuna chakula cha kutosha kwa mwezi wa Ramadhani na hata baada ya hapo. Hivyo, nazitaka mamlaka husika kusimamia mwenendo wa bei za bidhaa za chakula na kuhakikisha hazipandishwi ovyo ili kufikia malengo ya dhamira njema ya Serikali ya kuondoa ushuru wa bidhaa hizo ili wananchi hasa wa kipato cha chini waweze kumudu kuzinunua.

Ndugu wananchi,

Suala la kutunza usafi ni moja ya majukumu muhimu katika kujiepusha na maradhi mbalimbali hasa ya kuambukiza na pia kuimarisha haiba na taswira ya miji yetu. Sote ni mashahidi kuwa uzalishaji wa taka huongezeka sana katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kutokana na shughuli mbali mbali katika Manispaa, Miji na Halmashauri zetu.

Napenda kutumia fursa hii kuzitaka Mamlaka zote zinazosimamia usafi wa mazingira katika Manispaa, Miji na Halmashauri zote Unguja na Pemba kuwa na mipango na mikakati maalum ya kushughulikia usafi katika maeneo yao.

Aidha, niwaombe wananchi kushirikiana na mamlaka husika kutunza usafi wa mazingira  katika maeneo yote hasa kwenye masoko, maeneo ya huduma za chakula na maeneo ya makaazi.

Ndugu wananchi,

Nahitimisha risala yangu kwa kuhimiza umuhimu wa kuendelea kuishi kwa amani, kuheshimiana na kujiepusha na mambo yote ambayo yanakwenda kinyume na mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kutii sheria, kuepuka mambo yote yanayoweza kusababisha maudhi au karaha kwa  waliofunga. Tuna wajibu wa kuendelea kuishi kwa kuvumiliana ili kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini.

Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie kuitekeleza ibada ya saumu na ibada nyengine kwa Ikhlasi ili tuweze kunufaika na fadhila za utukufu wa mwezi huu. Mwenyezi Mungu aizidishie nchi yetu amani, umoja na mshikamano. Atuzidishie Imani, uchamungu na atuwezeshe kupata riziki za halali kwa baraka na utukufu wa mwezi wa Ramadhani ili tuweze kupata mafanikio  hapa Duniani na kesho mbele ya haki. Amina! 

Ramadhan Mubarak.

Wassalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu

Ahsanteni kwa kunisikiliza