Media » Speeches and Statements

Kukaribishwa kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan

Ndugu Wananchi,
Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuhu.
Ni wajibu wetu kumshukuru Mola wetu (SW) kwa kutujaalia neema ya uhai hadi leo hii ambapo tunaukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.  Hii ni neema kubwa kwa kuzingatia kuwa ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu mwenyewe kutufikisha, kwani tulikuwa na wenzetu wengi tuliofunga nao Ramadhani iliyopita lakini sasa wameshatangulia mbele ya haki.  Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na sisi atuwezeshe kuukabili mwezi wa Ramadhani kwa salama na amani.  Atupe afya njema na ilhamu ya kuitekeleza nguzo hii ya nne ya kiislamu kwa ikhlasi ili tuweze kunufaika na malipo makubwa ya ibada katika mwezi huu na katika maisha yetu ya baadae.

Ndugu Wananchi,
Mwenyezi Mungu (SW) ametujaalia neema ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kila mwaka na kutufaridhishia kufunga kama alivyoeleza katika Kuran, kwenye aya ya 183 ya Surat Al Baqara yenye tafsiri isemayo:“Enyi mlioamini mmefaradhishiwa kufunga (saumu) kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”.
Maimamu na masheikh wetu huwa wanatumia aya hii kutukumbusha kuwa ibada ya saumu inatokana na Mola mwenyewe kuwataka waumini waitekeleze ili iwe ni sababu ya kupata uongofu na rehma za Mola wetu (SW). Saumu inamuongezea muumin daraja ya ucha Mungu, kuwa msafi kwa kujiepusha na maasi ya aina mbali mbali, kuongeza mapenzi mema baina ya wanaadamu, kuimarisha afya ya kiwiliwili na kubainisha dhana ya usawa miongoni mwa watu, kwani waumini wote humwelekea Mola mmoja kwa kutarajia malipo mema kutoka kwake hapa duniani na kesho akhera.

Ndugu Wananchi,
Mwenyezi Mungu (SW) ameujaalia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa ni mwezi wenye daraja kubwa ikiwa ni pamoja na kuteremshwa kitabu kitukufu cha Kurani katika usiku wenye hadhi wa ‘Lailatul Kadir’ ambao ni bora kuliko miezi elfu. Kwa hivyo, miongoni mwa ibada muhimu tunazopaswa kuziendeleza sana katika mwezi wa Ramadhan ni kufanya bidii ya kusoma Kurani, kuhudhuria darsa mbali mbali ili kufahamu mafundisho ya Mola wetu pamoja na jitihada katika sala za Faradhi na Sunna hasa kusali Tarawekh na sala nyengine za usiku.  Kwa namna hii tutakuwa ni wenye kunufaika na rehema na baraka ya malipo makubwa yanayotokana na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao hutufikia mara moja tu kwa mwaka. Imeelezwa katika mafundisho ya Hadith kwamba katika mojawapo ya hotuba alizozitoa kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Bwana Mtume (S.A.W) amesema,
“Enyi watu! Hakika umewaelekeeni nyinyi, mwezi wa Mwenyezi Mungu (mwezi wa Ramadhani) kwa baraka, rehema na msamaha. Mwezi ambao ni bora kuliko miezi yote, na masiku yake ni bora kuliko masiku mengine yote na saa yake ni bora na muhimu kuliko masaa yote”.Kwa hivyo, tuukaribishe Mwezi huu kwa matumaini, imani na matarajio ya kunufaika na fadhila kubwa za malipo ya kufanya ibada katika mwezi huu wa Saum.

Ndugu Wananchi,
Napenda kuwakumbusha wazazi wenzangu juu ya wajibu wetu wa kuwaongoza watoto wetu kuinukia katika misingi hii ya ibada.  Wahenga walisema “Udongo upate ulimaji”.  Ni dhahiri kuwa wazazi tuna wajibu muhimu wa kuwalea watoto wetu katika misingi ya maadili mema ili kuwaandaa kumcha Mwenyezi Mungu na kufanya ibada tangu wakiwa wadogo.  Hapana shaka kuwa elimu ya dini ina faida kubwa kwa watoto na ni yenye kudumu katika mioyo yao.
Kwa kupitia mafundisho ya dini, watoto hujifunza mambo ya ibada kama sala, funga, historia ya Uislamu vikiwemo visa vya Mitume kupitia Kurani na Hadithi ambazo huwajenga kiimani na kuwafanya wawe na tabia njema na kuwapa misingi bora ya ucha Mungu ili kuwawezesha kuwa raia wema wenye nidhamu na kuzingatia maadili mema.

Ndugu Wananchi,
Katika kuelezea umuhimu wa elimu ya dini kwa watoto, ulamaa mmoja mashuhuri Sayyid Qutb wa Misri katika mwaka 1323 AH aliwahi kusema kuwa watu wazima sio peke yao wanaopaswa kufunzwa uislamu kwa kufundishwa Kuran Tukufu na Hadithi za Bwana Mtume( SAW). Lakini elimu hiyo vilevile ni muhimu kwa watoto ili kuwakuza imani, maarifa na maadili mema ya dini ya Mwenyezi Mungu tangu wangali wadogo.
Sayyid Qutb alisisitiza umuhimu wa vijana wa vizazi vya sasa na vijavyo kupewa elimu (ya dini) kutokana na kukabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali. Kwa hivyo, elimu na malezi bora ndiyo misingi bora ya kuwafanya watoto wetu wawe na hatma njema katika maisha yao na hatma njema ya jamii yetu kwa jumla. 

Kauli hii ya mwanazuoni wa Misri inatukumbusha wajibu tulionao sisi wazazi kwa watoto wetu. Jambo hili ni muhimu kuliimarisha katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuyatumia mafunzo yake katika miezi mingine. Katika mwezi wa Ramadhan, wazazi watumie vizuri fursa hii kuwahimiza watoto wetu wasome Kurani iwe katika madrasa, misikitini na hata majumbani kwani katika kipindi hiki skuli huwa zimefungwa. Kwa hivyo, ni vyema kuliendeleza jambo hilo ili kuwaandaa vyema watoto wetu kupenda kufanya ibada na kuwa na maadili mema. 

Ndugu Wananchi,
Napenda niitumie fursa hii ili niupongeze na niushajiishe zaidi utamaduni wa kuendesha mashindano ya usomaji wa Kurani miongoni mwa vijana wa madrasa zetu nchini katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Ni dhahiri kuwa,  kuisoma na kuihifadhi Kurani ni njia moja iliyo bora ya kukitukuza kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa kukisoma zaidi katika mwezi huu ili tupate fadhila nyingi. Utaratibu wa mashindano ya kuhifadhi Kurani una mchango mkubwa katika kuwaelekeza vijana wetu katika mambo ya kheri. Kadhalika, utaratibu huu unasaidia katika kukuza uhusiano miongoni mwa vijana wa madrasa zetu, kuwapa moyo zaidi wale vijana wanaofaulu na kuwapa ari ya kujitayarisha zaidi kwa wakati ujao wale ambao hawakufanikiwa wakati huu. Hata hivyo, wote hawa huwa wameshinda mbele ya Mwenyezi Mungu na wana fadhila kubwa kesho mbele ya haki kwa kuisoma Kurani hasa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani.  Niwanasihi wazazi wenzangu tuziunge mkono jitihada hizi za walimu, masheikh na maulamaa wetu kwa namna mbali mbali ili kuliendeleza jambo hili lenye manufaa kwetu sote hapa duniani na huko tunakokwenda.

Ndugu Wananchi,
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani huwa na nafasi na haiba maalum katika maisha na utamaduni wetu ambao hudhihirika katika mambo mbali mbali ikiwemo mavazi, vyakula, biashara, mashirikiano baina ya watu na mambo mengine.  Katika baadhi ya maeneo na hasa mashamba, watu wanaendeleza utamaduni wa kula pamoja nje ya nyumba zao na wengine kupelekeana vyakula hasa vile vya tunu. Mambo haya yana umuhimu mkubwa kwa jamii yetu kwani huongeza mapenzi, ukarimu, mashirikiano, udugu na kusaidiana katika mambo ya heri. Kadhalika, katika mwezi huu watu wengi huzingatia umuhimu wa kuvaa mavazi ya stara na kujiepusha na vitendo vyote vitakavyosababisha kuleta maudhi, ugomvi au kuondoa hali ya amani na utulivu tuliyonayo mambo ambayo yangepaswa yaendelezwe siku zote.
Shughuli za biashara nazo huzidi kushamiri katika Mwezi wa Ramadhani.  Ni vyema wafanyabiashara wakaitumia neema hii kwa kufanya biashara zao kwa njia ya uadilifu na kutilia maanani uwezo mdogo wa baadhi ya wanunuzi wao.  Kwa hivyo, kama kawaida nawanasihi wafanyabiashara wote kuwasaidia wananchi wenzao kupata unafuu wa mahitaji ya bidhaa mbali mbali za chakula, mavazi na nyenginezo. Mafunzo ya Uislamu yanatufundisha kwamba Mwenyezi Mungu (SW) huiongezea baraka biashara inayofanywa kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na kuridhiana. 

Katika kuonesha umuhimu wa uaminifu katika biashara, imepokelewa kutoka kwa Al-Tirmidhiy na Al-Haakim kwamba Bwana Mtume(SAW) amesema, “Mfanyabiashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, Wakweli na Mashahidi siku ya Kiyama” .
Kwa hakika hii ni daraja kubwa kuifikia na hapana shaka malipo yake huongezeka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwa hivyo, ni vyema fursa hiyo tukaitumia katika kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Kwa upande mwengine, napenda kuwakumbusha wafanyabiashara wote wafahamu kuwa fursa inayotolewa na Serikali ya kupunguza kodi kwa baadhi ya bidhaa muhimu ikiwemo mchele, unga wa ngano na tende ina lengo la kuwanufaisha wananchi. Si sahihi kuwauzia wananchi bidhaa zilizopita muda wake, zilizo chini ya kiwango au kuuza katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuleta usumbufu kwa wananchi. Naziagiza taasisi zinazohusika kusimamia sheria ya uendeshaji wa biashara ikiwa ni pamoja na kuzikagua vyema bidhaa wanazouziwa wananchi juu ya ubora wake na kuzingatia usafi ili kuzilinda afya zao.

Ndugu Wananchi,
Hali ya upatikanaji wa chakula muhimu kwa kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani tunategemea kwamba itakuwa nzuri. Taarifa tuliyoletewa Serikalini ni kwamba tayari ghala za ndugu zetu wafanyabiashara zina shehena ya kutosha ya bidhaa muhimu ikiwemo mchele, unga na sukari.  Aidha, kutokana na baraka ya mvua tuliyoipata katika kipindi hiki pamoja na hali ya mazao katika masoko yetu ilivyo hivi sasa, ni wazi kwamba hali ya vyakula vinavyotumika sana katika futari zetu vikiwemo ndizi, muhogo na viazi itakuwa ni ya kuridhisha. Kwa jumla hali hii itatusaidia waumini kupata unafuu wa chakula na kuendeleza shughuli mbali mbali za ibada kwa utulivu.
Nasaha zangu ni kuzitumia neema hizi za kuwepo kwaa hali nzuri ya upatikanaji wa chakula kwa manufaa ya kila mmoja wetu lakini nataka nizidi kuwasisitiza wafanyabiashara wetu waepuke kupandisha bei ya bidhaa na mahitaji muhimu bila ya sababu za msingi.

Ndugu Wananchi,
Kwa neema za Mwenyezi Mungu, mwezi wa Ramadhan umekuja wakati nchi yetu inaingia katika msimu mkubwa wa utalii.  Tunatarajia kupokea wageni wengi wakiwemo wale ambao si waislamu. Uislamu unatufundisha namna ya kuwatendea wema wasafiri bila ya kuwabagua.  Ni dhahiri kuwa wao watategemea sana mchango wa kila mmoja wetu katika kuwaelekeza taratibu ambazo wanapaswa wazifuate wakati huu, ambao jamii yetu ipo katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani bila ya kuwabughudhi. Naamini kuwa hata wale ambao hawatoshiriki katika saumu, wataendelea kuuheshimu na kuustahi Mwezi huu Mtukufu kwa kujiepusha na vitendo vya karaha na vitendo vyengine vitakavyosababisha mapenzi baina yetu, umoja wetu na mshikamano wetu, kuanza kutetereka. 
Kila mmoja azingatie umuhimu wa kuishi kwa amani na kustahamiliana ili nchi yetu iendelee kupata ustawi mzuri na mafanikio kwa wananchi na wageni wanaokuja kututembelea. Katika baadhi ya nchi kama vile Misri, watalii na wageni wengine huhusishwa na tabia na shughuli mbali mbali zinazofanywa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwa mfano, kufuturu na wenyeji kwa pamoja ili waone utamaduni wa Kiislamu.  Hili ni jambo zuri kwani linaimarisha urafiki na udugu na kujenga imani miongoni mwa waja.

Ndugu Wananchi,
Napenda nimalizie risala yangu kwa kusisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika masuala yote yanayohusu ustawi wa jamii yetu. Sote tuwe walinzi wa amani kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama. Askari wa usalama barabarani wasaidie kuwadhibiti madereva ili waache kwenda mwendo wa kasi kwa kisingizio cha kuwafikisha watu wanakotaka kwenda kwa haraka.
Namuomba Mola wetu Mtukufu atuafikishe kuikabili Saumu ya Ramadhan kwa mafanikio.  Atujaalie baraka, afya njema na uwezo wa kufanya ibada kwa wingi ili tufanikiwe kupata fadhila zake zikiwemo rizki, maghfira na kuachwa huru na moto.
Ramadhan Karim
Assalamu Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuhu
Ahsanteni kwa kunisikiliza

RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHESHIMIWA ALHAJ DK. ALI MOHAMED SHEIN YA KUUKARIBISHA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI MWAKA 1435 A.H. SAWA NA MWAKA,2014 BISMILLAHI RAHMAN RAHIM Naanza kwa jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muumba wa dunia na vyote viliyomo ndani yake.  Ni yeye pekee ndiye anayestahiki shukurani za waja na viumbe wote.  Na kwake yeye ndiyo marejeo yetu sote.