Alimueleza balozi huyo kuwa Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii na ndo maana juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na serikali anayoiongoza katika kuiimarisha sekta hiyo muhimu katika kuchangia pato la taifa.
Kwa upande wa sekta ya kilimo Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekusudia kuimarisha Mapinduzi ya Kilimo kwa kutekeleza Sera na programu mbali mbali za kilimo.Alimueleza kuwa lengo kuu la kuchukua hatua hiyo ni kuhakikisha wananchi wa Zanzibar pamoja na Taifa kwa jumla wanakuwa na uhakika wa chakula wakati wote.Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo hatua zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuimarisha sekta ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa kutokana na tija yake kwa wavuvi na Taifa kwa ujumla.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na kuimarisha sekta nyengine za maendeleo pia, imeelekeza zaidi nguvu zake katika kuimarisha sekta ya uvuvi huku akimueleza jinsi uchumi wa Zanzibar unavyoimarika siku hadi siku sanjari na kuimarika kwa ukusanyaji wa mapato yake.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake ulionao kati yake na Ireland na kusisitiza kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano huo.Dk. Shein hakuchelea kutoa pongezi kwa balozi huyo kutokana na nchi yake kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo.Kwa upande wa utamaduni, Dk. Shein alieleza kuwa ipo haja ya kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika kushirikiana kiutamaduni hasa ikizinagtiwa kuwa bado tamaduni na nchi hiyo hasa katika masuala ya ujenzi historia yake ipo hapa Zanzibar.
Nae, Balozi Gilsenan alimueleza Dk. Shein kuwa mafanikio makubwa yamepatikana Zanzibar kwani Zanzibar imeweza kuwa na badaliko kadhaa ya kimaendeleo kila kukicha.Katika maelezo yake balozi huyo ambaye aliwahi kuitembelea Zanzibar katika miaka ya tisini, alisema kuwa amejionea mabadiliko makubwa ya kimaendeleo hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua hiyo imetokana na juhudi za Serikali pamoja na wananchi wake katika kujiletea maendeleo.Akieleza kuhusu utamaduni wa Zanzibar, Balozi huyo wa Ireland alisema kuwa anavutiwa sana na maonyesho na matamasha mbali mbali yanayofanyika hapa Zanzibar ambayo yana lengo la kuuimarisha na kuutangaza utamaduni wa Zanzibar ndani na nje ya nchi.
Kutokana na hatua hiyo, Balozi Gilsenan alimueleza Dk. Shein kuwa ni vyema matamasha hayo yakaendelezwa ambayo sio tu ni muhimu katika kukuza utamaduni bali pia, ni muhimu katika kuendeleza sekta ya utalii nchini.
Katika maelezo hayo, Balozi Gilsenan alimuahidi Dk. Shein kuwa yeye mwenyewe binafsi ataendelea kuwa balozi katika kuitangaza Zanzibar kiutalii nchi mwake hasa akizingatia mafanikio yaliopatikana katika sekta hiyo hapa nchini. Akieleza kuhusu mazingira, balozi huyo alisisitiza haja ya kutunzwa na kuenziwa mazingira ya bahari hasa ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii kutoka nchi mbali mbali duniani.Balozi huyo alieleza kuwa Ireland itaendelea kuiunga mkono Zanzibar sambamba na kuzidisha uhusiano na ushirikiano wake katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo sekta ya elimu, afya na huduma nyengine za kijamii.