Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee walishiriki kikamilifu, Wizara hiyo ilieleza kuwa hatua hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro kadhaa katika sehemu za kazi nchini. Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Bi Zainab Omar alisema Sera hii itahusisha program mbali mbali za pencheni kwa wazee wote wakiwemo wakulima na wafanyakazi, afya kwa wazee na watoto, ulipaji wa fedha kwa familia zisizo na uwezo na kazi za malipo za kijamii.Wizara hiyo ilieleza kuwa kukamilika kwa Sera hii kutasaidia sana kujenga ustawi wa jamii kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na utekelezaji wake.
Waziri Bi Zainab, alieleza kuwa Wizara imo mbioni kukamilisha Sera ya Jinsia ambayo kukamilika kwake kutasaidia sana kuelimisha jamii juu ya maana ya jinsia na umuhimu wake katika mazingira ya utekelezaji wa kazi pamoja na maisha ya kijamii.Alieleza kuwa wazee wa Sebleni na Welezo Wizara imeendelea kuwatunza na kuwahudumia vizuri kadri ya uwezo wao na tayari imeshaanzisha suala la kuwapatia milo mitatu kwa siku na kuendelea kuwapatia posho lao kama kawaida. Pia, Wizara hiyo ilieleza jinsi ilivyolitafutia ufumbuzi suala la watoto wenye mazingira magumu nchini hasa kutokana na utafiti walioufanya huku ikieleza namna ilivyoendelea kuwa karibu na wanawake katika vikundi vyao vya kilimo, ujasiriamali, SACCOSS na Ushirika na kueleza ilivyofanya utafiti wa awali wa uanzishwaji wa Benki ya wanawake.Wizara pia, ilieleza haja ya upatikanaji wa mashine ya DNA, ili mapambano mdhidi ya udhalilishaji yaweze kufanikiwa kwani ilieleza kuwa pamoja na juhudi zote zinazofanywa na Wizara bado suala la udhalilishaji wa Wanawake na Watoto limeendelea kushika kasi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia, alikutana na uongozi pamoja na watendaji wa Wizara ya Kilimo na Malisili chini ya Waziri wake Mhe. Suleiman Othman Nyanga na kueleza nia ya Wizara hiyo ya kutekeleza kwa vitendo katika kumkomboa mkulima wa Zanzibar kutoka katika
kilimo duni kisicho na tija. Wizara hiyo ilieleza kuwa imo katika kutekeleza dhima ya Mapinduzi ya
Kilimo katika kuimarisha uchumi wa Taifa na kuondokana na umasikini.Aidha, Wizara hiyo ya kilimo na Maliasili ilieleza mikakati yake ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji maji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua ili yaweze kusaidia katika kilimo.Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza jinsi ilivyopania katika suala zima la utafiti na kueleza jinsi ilivyoamua kuwashirikisha wakulima pamoja na washirika wengine sanjari na kuwashajiisha wakulima katika matumizi ya pembejeo na mbinu bora za kilimo.Waziri Nyanga alieleza kuwa Wizara hiyo imo katika mikakati ya kuwajengea uwezo wakulima katika kusarifu mazao ya wakulima pamoja na kuhifadhi kilimo na maliasili ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko.Pia, Wizara imo katika juhudi za kupunguza uharibifu wa mimea na mazao utokanao na maradhi, wadudu, ndege na nzi na kueleza haja ya kuimarisha soko la ndani na kupunguza kusafirisha mazao nje ya nchi. Sambamba na hayo, Wizara hiyo ilieleza juhudi inazozichukua katika kuimarisha zao la Karufuu nchini.
Akitoa pongezi kwa nyakati tofauti alizokutana na Wizara hizo, Dk. Shein aliipongeza Wizara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto kwa juhudi zake inazozichukua katika kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea.
Kwa upande wa Wizara ya Kilimo na Maliasili, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mikakati maalum ya kuimarisha sekta hiyo ili kuleta tija na mafanikio nchini huku akieleza azma ya serikali katika kuendelea kuwaunga mkono wakulima nchini.