Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza viongozi wa dini, wanasiasa, waandishi wa habari na wananchi kupaza sauti kukemea matamko yote yanayoashiria uvunjifu wa amani.Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Baraza la Maulid lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Polisi Ziwani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kuhubiri na kulinda amani, sambamba na kujiepusha na matamko yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani hususan wakati huu ambapo nchi inakaribia uchaguzi mkuu.Ameeleza kuwa hakuna taifa lolote linaloweza kuendelea bila amani ya kudumu.

Aidha, amewasisitiza wanasiasa kuepuka siasa za chuki na mifarakano kwani hazina tija kwa jamii inayohitaji maendeleo na ustawi.Vilevile, Dkt. Mwinyi amewanasihi waumini wa dini ya Kiislamu kufuata mwenendo na mafunzo ya dini yao ili kudumisha amani.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika Baraza hilo la Maulid ambalo kauli mbiu yake ilikuwa: “Amani na Utulivu Tunu.”