Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaongoza viongozi na wananchi mbalimbali katika maziko ya marehemu Joseph Abdallah Meza.

Maziko hayo yamefanyika leo tarehe 31 Januari 2026, Kisauni, Mkoa wa Mjini Magharibi, majira ya alasiri. Marehemu Joseph Abdallah Meza amefariki dunia tarehe 29 Januari 2026 alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Katika uhai wake, marehemu Joseph Abdallah Meza aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi, zikiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Kamishina wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kabla ya kuwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC).

Marehemu Joseph Abdallah Meza alizaliwa tarehe 8 Agosti 1959 na kufariki tarehe 29 Januari 2026, akiwa ameacha mjane na watoto saba.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya familia, mtoto wa marehemu, Paulina Joseph Meza, amemshukuru Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa upendo na msaada mkubwa wa matibabu aliyoutoa kwa marehemu alipokuwa akitibiwa, pamoja na kumuelezea marehemu kuwa alikuwa mtu wa watu na mwenye upendo.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.