Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka viongozi wa siasa, viongozi wa dini pamoja na waandishi wa habari kuhakikisha wanahimiza amani na utulivu wakati Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu.Akizungumza katika Sala ya Ijumaa na Dua Maalum ya kumuombea pamoja na kuliombea Taifa, iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Al-Abrar, Tazari, Mkoa wa Kaskazini Unguja leo tarehe 3 Oktoba 2025.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo Taifa haliwezi kuendelea bila utulivu.Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa si sahihi kwa baadhi ya wanasiasa kuhamasisha wananchi “kulinda kura”, kwani jukumu hilo kwa mujibu wa sheria linatekelezwa na mawakala wa uchaguzi, na si wananchi binafsi. Alionya kuwa kauli hizo huweza kuchochea uvunjifu wa amani, jambo ambalo halikubaliki wakati huu ambao Zanzibar imeendelea kufurahia utulivu na maelewano.

Halikadhalika, Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Zanzibar bado inahitaji maendeleo zaidi, hivyo amani ni sharti la msingi kwa Serikali kuendelea kutekeleza mipango yake ya maendeleo kwa ufanisi.Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amewataka Waislamu kuzingatia mafunzo ya Mtume Muhammad (SAW) ili kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani.

Naye Khatibu wa Msikiti wa Al-Abrar, Sheikh Omar, amemshukuru Rais kwa miradi mikubwa ya maendeleo katika Mkoa wa Kaskazini hususan sekta za elimu, afya na miundombinu ya barabara. Ameahidi kuendelea kumuombea dua Rais pamoja na viongozi wengine wa Serikali.