RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuhakikishia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo kuwa ataendelea kushirikiana nae katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezwa ipasavyo.

Rais Dk. Mwinyi ambaye pia, ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, aliyasema hayo leo wakati alipokutana na ujumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ulioongozwa na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fusra hiyo kuwapongeza viongozi hao wakiwemo wapya pamoja na wale wa zamani kwa kuendelea kubaki katika nafasi zao na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kutekekeza majukumu ya chama na Serikali.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeshaanza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambapo hivi karibuni imepitisha Bajeti ya Kwanza ya Serikali hiyo na lililobaki hivi sasa ni kuhakikisha yale yote yaliyoahidiwa kwa wananchi yanatekelezwa.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwashukuru viongozi hao kwa kuja kumuona na kujitambulisha kwake na kuwaahidi kufanya kazi nao huku akiwahakikishia kwamba milango yake iko wazi na yuko tayari kukutana nao wakati wowote kwa madhumuni ya kujenga nchi sanjari na kuhakikisha CCM inaendelea kufanya vizuri zaidi.

Rais Dk. Mwinyi aliwashukuru viongozi hao kwa kuwa karibu na Serikali zote mbili na kuahidi kufanya kazi nao ili maendeleo zaidi yaweze kupatikana.

Pia, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba pale watakapokuwa tayari kuuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Serikali zote mbili wawe huru kueleza yale yote yanayopaswa kufanywa vizuri zaidi kwa lengo la kuitakia mema CCM na Serikali zake mbili.

Mapema Katibu Mkuu huyo wa CCM Taifa Daniel Chongolo alisema kuwa ujio wake wa kukutana na Rais Dk. Mwinyi pamoja na ujumbe wake huo ni kuja kujitambulisha kwake ambapo pia, tayari ameshajitambulisha kwa wazee, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar pamoja na kuzungumza na baadhi ya wanaCCM wa Zanzibar.

Pia, Katibu Mkuu huyo alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa niaba ya Sekretarieti kwa kazi kubwa anayoifanya kwa wananchi wa Zanzibar huku akitumia fursa hiyo kumkabidhi Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa la kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Sambamba na hayo, Katibu Mkuu huyo alieleza kwamba ziara yake ya hapa Zanzibar imempa mwanga mkubwa wa jinsi Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi inavyofanya juhudi za kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar.

Pia, Katibu Chongolo alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba wazee wa CCM Zanzibar wametoa azimio la kumpongeza yeye pamoja na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Taasisi inayoshughulikia misaada ya Kibinaadamu kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) Sheikh Ahmad Al Nazir Al Falasi na ujumbe wake.

Katika mazungumzo yake ya Taasisi hiyo, Rais Dk. Mwinyi ameihakikishia Taasisi hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Taasisi hiyo katika kuimarisha huduma za kijamii pamoja na zile za kimaendeleo.

Rais Dk. Mwinyi ameipongeza Taasisi hiyo kwa utayari wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kusaidia vifaa tiba katika Hospitali kuu za Unguja na Pemba ikiwemo Hospitali ya Mnazi Mmoja na Vitongoji Pemba.

Mapema Sheikh Ahmad Al Nazir Al Falasi alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya Taasisi anayoingoza ya kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

Aidha, Al Falasi alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba mbali ya kuunga mkono juhudi hizo pia, amevutiwa na mazingira ya uwekezaji katika sekta ya kilimo hapa Zanzibar na kuahidi kutekeleza azma yake hiyo. 

Ujumbe huo ambao umefuatana na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui pia, unatarajia kutembelea kisiwani Pemba katika hospiitali ya Vitongoji, Chake Chake na Wete.