Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Oman na kupongeza uhusiano mwema wa kindugu na kihistoria uliopo baina ya Zanzibar na Oman. Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 09 Oktoba 2025, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Kale na Utalii wa Oman, Mhe. Sheikh Salim bin Mohammed Al Mahrouqi, aliyefuatana na Balozi Mdogo wa Oman anayefanya shughuli zake Zanzibar, Mhe. Said Salim Al Sinawi, pamoja na ujumbe kutoka Wizara hiyo ya Oman.
Waziri Mahrouqi amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa kumkaribisha Ikulu, na ameahidi kuendeleza ushirikiano katika programu ya ukarabati wa majengo mbalimbali ya kihistoria yanayofadhiliwa na Serikali ya Oman.
Akiwa na mwenyeji wake, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga, Waziri Mahrouqi alipata fursa ya kutembelea majengo mbalimbali yanayofadhiliwa na Serikali ya Oman, ikiwemo Beit al Ajaib, Jengo la Mtoni Palace, Jengo la Kibweni Palace, na majengo mengine yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
