Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alieleza kuwa ni vyema kila mmoja akaitumia fursa hiyo ya kidemokrasia na kuwataka wananchi kuwa makini na subira kusubiri siku itakapofika kwani hatopuuzwa wala hatobezwa mtu na kusisitiza kuwa wasije wakatokea mahodari wakawakataza wenziwao kwani nchi hii ina uhuru wa kutoa maoni.
Dk. Shein alisema kuwa ndio maana Serikali imeweka Tume hiyo ili watu waseme na watoe maoni yao kwa lengo la hapo baadae kupata Katiba iliyo nzuri. Kwani Tume hiyo imesheheni wajumbe wazuri ambao watapita kila Mkoa hapa nchini.
“Hakuna haja ya pupa, hata ukisema sasa hivi atakusikiliza nani, Tume haipo”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein katika hotuba yake hiyo ya majumuisho alitoa wito kwa viongozi wote wa kidini a kisiasa kutumia mawaidha na nasaha zao kwa watu kuelimisha juu ya ubaya wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika Mkoa huo.
Dk. Shein pia, aliitaka Wizara ya Kilimo na Maliasili kuchukua hatua za haraka za kuwafikishia wakulima matrekta na pembejeo zinazohitajika kwa lengo la kuuwahi msimu wa kilimo unaoendelea.
Katika maelezo yake, Dk. Shein pia alisisitiza umuhimu wa sensa ya kuhesabu watu na aliwasihi wananchi wa Mkoa huo kuyaendeleza mafanikio ya zoezi la sensa ya majaribio yaliofayika mwezi Oktoba mwaka jana na kutaka kuyatumia mafaikio hayo mwezi Agosti mwaka huu wakati wa zoezi hilo utakapofika.
Kwa dhati kabisa Dk. Shein alimpongeza Dk. Maua Daftari kwa mchango wake mkubwa katika uhamasishaji na ushiriki wake katika kuanzishwa na kuendelezwa kwa SACCOS ya “Muungano wa Wajasiriamali Pemba” MUWAPE, sanjari na uungaji mkono wake yeye na wahisani kutoka Marekani na wengineo waliowasaidia vijana walioanzisha kiwanda cha utengenezaji sababuni kwenye ushirika wa MPIKI MILIKI.
Dk. Shein alitoa ushauri kwa ushirika huo kutafuta mbinu za kuendeleza shughuli zao kwa kuongeza ubora wa sababuni wanazozizlisha na wajitangaze kwa kutumia fursa mbali mbali zilizopo.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Awamu ya Saba ina dhima ya kupambana na umasikini wa kipato kwa wananchi wa makundi mbali mbali wakiwemo vijana na akina mama, ambapo tayari pia serikali imeshaandaa programu kadhaa kwa ajili ya kufikia malengo yaliokusudiwa.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa hatua ya Serikali ya kujenga tuta la kuzuia maji ya chumvi katika bonde ka Ukele-Mizingani zina lengo la kuyaimarisha mazingira ya eneo hilo ili liweze kutumika tena kwa shughuli za kilimo.
Kutokana na hali hiyo Dk. Shein alisisitiza upandaji wa mikandaa ziendelezwe kwa juhudi zote kwani ndio suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo na kuelez kufarajika kwake kutokana na Wzara ya Kilimo na Maliasili kuanza kupanda miti hiyo.
Aliipongeza Wizara ya Kilimo kwa juhudi zake za kuwapatia wakulima miche ya mikarafuu ambapo jumla ya miche 327,000 ya imeshagawiwa na kupandwa ikiwa ni lengo la Serikali la kupanda miche 500,000 kwa msimu huu ambapo miche hiyo itagawiwa bure kama ilivyoahidiwa na seriali kwa kipindi kisichopungua miaka kumi kwa lengo la kupanda miche 5,000,000.
Akielezea juu ya zoezi lauchumaji wa karafuu, Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na ushirikiano wa wananchi pamoja na vikosi vya ulinzi katika kufanikisha zoezi la msimu huu ambapo lengo limevukwa huu akilitaka Sirika la ZSTC kufanya sensa ya mikarafuu yote ya Unguja na Pemba ili iwe rahisi kufanya makisio ya mavuno katika msimu.
“Narudia nasaha zangu kuwa vita dhidi ya magendo ya karafuu viendelee kwani ndio mkombozi wa uchumi wa wananchi na Taifa kwa jumla”,alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa wananchi wa Chimba kwa juhudi zao za kuanzisha kituo cha afya na kueleza kuwa serikali ina wajibu wa kuziunga mkoo juhudi hizo kwa kusaidia katika hatua inayoendelea.
Mapema kabla ya majumuisho hayo, Dk. Shein alishirikiana na wananchi katika kupanda miche ya mikarafuu huko katika shamba la Mikindani Tungamaa ambapo jumla ya miche 1200 imepadwa katika hekta 12 na nusu.
Dk. Shein pia, aliwapongeza wananchi wote wa Pemba kwa mapokezi yao mazuri na kuisifu ripoti ya Mkoa huo na kueleza kuwa ni dhahiri kuwa watendaji wa Mkoa huo wameanza kubadilika.
Nao wananchi wa Mkoa huo walitoa shukurani zao kwa Dk. Shein na kueleza jinsi walivyofarajika na ziara yake hiyo ambayo ni ya pili tokea kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kueleza kuwa wamepata kujifunza mambo mengi huku wakiahidi kuendelea kuiunga mkono serikali anayoiongoza pamoja na viongozi wake wote.