BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa imani yao wanayotoa kwa taasisi za fedha na hasa benki hiyo ya (NBC) hatua ambayo imechangia kuendelea kukua kwa uchumi wa Zanzibar. Hafla hiyo ya futari ilifanyika katika ukumbi wa Hoteli ya ‘Zanzibar Beach Resort’, Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar ambayo ilihudhuri na viongozi mbali mbali wa dini, siasa na Serikali, wateja na wanahisa wa Benki hiyo pamoja na wananchi.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Benki hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa (NBC) Dk. Kassim Hussein alisema kuwa imani ya wao kufanya kazi inatokana na amani, utulivu na upendo uliopo kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika nafasi zao mbali mbali walizonazo. Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa tofauti za dini, imani na mahali watu wanapotoka lakini tofauti hizo zinajumuishwa na harakati mbali mbali za kiuchumi ambazo kwa kiasi kikubwa zimeweza kuimarisha uchumi wa Zanzibar.  Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuweka Mazingira mazuri ambayo yanaiwezesha Benki hiyo kufanya shughuli zao vizuri pamoja na kuwepo kwa Sera na miongozo.

“Leo ukiona meli zinatoka Dar-es Salaam mara nne kuja Zanzibar pamoja na ndege zinazokuja Zanzibar kutoka maeneo mbali mbali duniani utaona wazi kuwa hiyo yote ni dalili ya kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar”,alisema Dk. Kassim.  Mwenyekiti huyo wa Benki ya (NBC) alieleza kuwa hatua ya kufutarisha ni utamaduni waliouweka ambao wamekuwa wakiuendeleza kwa muda mrefu na kupata fursa ya kuwaalika viongozi mbali mbali, wateja, wanahisa na wananchi kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara. Mwenyekiti huyo alisema kuwa (NBC) haifanyi Miamala yoyote na taasisi zozote za Serikali na kueleza kuwa asilimia 30 ni hisa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hatua ambayo inawapa kujiona kuwa wako pamoja na taasisi za Kitaifa.

Alieleza kuwa kuanzia mwaka 1967 tokea kuanzishwa kwa Benki hiyo ambayo ni ya kizalendo imekuwa ikitoa huduma pamoja na kuwa na mashirikiano mazuri na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), na wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na kuahidi ushirikiano huo kuendelezwa. Alieleza kuwa Benki hiyo pia, imekuwa ikitoa huduma ya Benki ya Kiislamu ambapo hutengwa huduma za riba na zisizo na riba hatua ambayo imewapelekea kuwa na watenja wengi kutokana na kufuata sheria katika masuala ya fedha na kutoa shukurani kwa wale wote wanaotumia huduma za benki ya Kiislamu. Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo alisema kuwa Benki hiyo imekuwa ikitoa miamala ya mikopo mbali mbali kwa kufuata sheria na kueleza kuwa wako tayari kufanya biashara kupitia Benki hiyo ya Kiislamu na wafanya biashara mbali mbali hapa nchini.

Aidha, alieleza kuwa kukua kwa sekta ya fedha hapa Zanzibar pia,  kunatokana na kuwepo kwa huduma za Benki hiyo ikiwa ni pamoja na kutumiwa na wafanyabiashara wakiwemo wa meli, wanaojenga mahoteli na wakandarasi kadhaa na watoa huduma mbali mbali na kuwa mkusanyaji mzuri wa kodi za Serikali kupitia (TRA) na (ZRB). Alisisitiza kuwa Benki hiyo imekuwa mkusanyaji mzuri wa mapato ya Serikali kwa Zanzibar na Tanzania Bara kupitia (TRA) na (ZRB) ambapo pia, haijawahi kupata shutuma za ubadhirifu hata mara moja ambayo pia, ni benki safi na kuwataka wananchi kuitumia Benki hiyo yenye uadilifu ili waweze kupata manufaa zaidi.

Nae Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein alitoa shukurani kwa Bodi ya Wakurugenzi na viongozi wa (NBC) kwa kumpa heshima ya kumualika Rais wa Zanzibar katika futari hiyo. Aidha, alitoa shukurani kwa utamaduni mzuri wa kurejesha sehemu ya faida yao kwa kila mwaka kwa wananchi wa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwatayarishia futari ambapo mbali ya kufutarisha kila mwaka pia, Benki hiyo imekuwa ikitoa misaada mbali mbali kwa wananchi. Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki hiyo kwa jinsi ilivyokuwa mstari wa mbele kuongeza kasi ya uchumi wa Zanzibar ambapo miradi mbali mbali imekuwa ikifanywa Zanzibar kwa kupitia Miamala ya (NBC). Pato la Taifa limekuwa likikua mwaka hadi mwaka ambapo moja ya wachangiaji ni Benki ya (NBC) na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar wataendelea kuiunga mkono Benki hiyo pamoja na taasisi nyengine za fedha.