RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza haja kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Canada ambao pia, unaiwakilisha Tanzania nchini Cuba kuitilia mkazo Sera ya Diplomasia ya Uchumi hasa katika sekta ya viwanda ambayo ndio kiu ya Tanzania.Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Canada ambaye pia, anaiwakilisha Tanzania nchini Cuba Alphayo Kidata aliefika Ikulu kumuaga Rais pamoja na kujitambulisha ikiwa tayari kuelekea katika kituo chake cha kazi alichopangiwa.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali zote mbili , Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeweka kipaumbele na mikakati maalum katika kuimarisha sekta ya viwanda katika kukuza uchumi wake.Dk. Shein alieleza kuwa Serikali zote mbili zimedhamiria kwa makusudi kuimarisha uchumi wake kupitia sekta ya viwanda na tayari mwanzo mzuri umeweza kuonekana huku akisisitiza kuwa sekta ya viwanda ni sekta ambayo ina msaada mkubwa katika kuimarisha sekta nyengine zikiwemo sekta ya kilimo na biashara.
Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa Ubalozi huo kuitangaza vyema Tanzania katika sekta ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwakaribisha wawekezaji kuja kuekeza Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vya uvuvi kwa upande wa Zanzibar kutokana na mazingira yake.Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya Ubalozi wa Tanzania nchini Canada kuongeza kasi katika kuutangaza Utalii wa Tanzania kutokana na kuwepo utajiri mkubwa wa vivutio vya kitalii vikiwemo mbuga za wanyama, mlima wa kilimanjaro, fukwe za bahari na viungo vya vyakula na Mji Mkongwe kwa upande wa visiwa vya Zanzibar.
Alieleza kuwa sekta ya utalii ni sekta muhimu katika kuchangia uchumi wa Zanzibar na hivi sasa imekuwa ikiimarika kwa kasi kubwa kutokana na ongezeko la watalii.Hata hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa nchi ya Canada kuendeleza dhamira ya dhati katika kuimarisha sekta ya elimu kwani Canada imekuwa ikiiunga mkono Tanzania kwa muda mrefu katika sekta hiyo.
Kwa upande wa nchi ya Cuba, Rais Dk. Shein alieleza kuwa nchi hiyo imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Zanzibar na imekuwa ikifaidika katika uhusiano huo hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ndiyo ya mwanzo kuyatambua Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imekuwa ikishirikiana vyema na nchi ya Cuba hasa katika sekta ya afya, ambapo nchi hiyo imeweza kutoa wataalamu wake kuja kutoa huduma za afya hapa Zanzibar pamoja na kutoa mafunzo kwa madaktari wa wazalendo.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba pia, umewezesha Zanzibar kuendelea kuungwa mkono na nchi hiyo katika sekta ya elimu hasa elimu ya juu.Alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya Cuba na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa siku nyingi ambao uliasisiwa na viongozi wa Taifa hilo akiwemi Marehemu Fidel Castro na Marehemu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Nae Balozi wa Tanzania nchini Canada ambaye pia, anaiwakilisha Tanzania nchini Cuba Alphayo Kidata alimueleza namna ya nchi ya Canada na Cuba jinsi zilivyokuwa na uhusiano na ushirikiano madhubuti na Tanzania ambao unapaswa kuimarishwa.Balozi Kidata alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa atafanya juhudi za makusudi katika kuhakikisha mashirikiano kati ya nchi hizo na Tanzania yanaimarika ikiwa ni pamoja na kuitangaza azma ya Tanzania katika kuimarisha uchumi wa viwanda pamoja na kutafuta wawekezaji katika sekta hiyo.
Sambamba na hayo, Balozi Kidata alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa ataitangaza vyema Tanzania katika sekta ya utalii.