RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema kuwa Kenya na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla zina uhusiano wa kihistoria na kindugu ambao ni lazima uimarishwe na uendelezwe kwa faida ya pande zote mbili.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati akizungumza na Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta mjini Nairobi . Katika mazungumzo hayo,Dk. Shein alisisitiza juu ya ushirikiano katika kuendeleza uchumi wa bahari kuu baina Kenya na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.

Dk. Shein alisema kwamba watu wa Tanzania ni ndugu na wamoja kwa hivyo ni muhimu pande mbili hizo kuzidisha ushirikiano huo uliopo katika masuala mbali mbali ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumzia suala la kuendeleza uchumi wa bahari kuu, Dk. Shein alishauri kwamba ni muhimu kuandaliwe programu ya pamoja ya kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, hatua ambayo ni muhimu katika jitihada zinazoendelea za kukuza ajira kwa vijana na kuwa na matumizi bora ya rasilimali za bahari.

Vile vile, katika kufanikisha mikakati na mipango iliyopo ya kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za bahari, mito na maziwa alisema kwamba ni vyema nchi hizo zikahakikisha kwamba sekta binafsi zinashirikishwa kikamilifu.

Aidha, Dk. Shein alipendekeza kwamba itakuwa ni vyema kuanzisha utaratibu ambao utaziwezesha timu za viongozi na wataalamu kutoka pande mbili hizo kukutana mara kwa mara, ikiwa ni hatua muhimu ya kujadili mafanikio na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika sekta hiyo. Aliongeza kusema kwamba hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uhusiano uliopo.

Kwa upande wake, Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na ujumbe aliofuatana nao kwa kwa kukubali mwaliko wa kuhudhuria katika mkutano wa Kimataifa wa Uchumi Endelevu wa bahari unaoendelea nchini humo.

Rais Kenyatta alipongeza uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuanzisha safari za meli baina ya Zanzibar na Mombasa kwa ajili ya kuimarisha huduma za usafiri, biashara na kuendeleza uhusiano wa kidugu na kihistoria uliopo baina ya wananchi wa pande mbili hizo.

Vile vile, alishauri kwamba itakuwa ni vyema hivi sasa kuimarisha huduma za usafiri kwa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja baina ya Zanzibar na Mombasa, ili kufanikisha utekelezaji wa mipango na mikakati ya kuimarisha sekta ya utalii, hasa ikizingatiwa kwamba sekta hiyo ni muhimu kwa uchumi wa pande zote mbili.

Alisema kwamba hivi sasa wapo watalii wengi wanaotembelea Mombasa ambao wangependa kusafiri moja kwa moja kwenda Zanzibar lakini hushindwa kufanya hivyo kutokana na kukosekana kwa usafiri wa aina hiyo.

Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, alihimiza haja ya kuimarsiha mikakati iliyopo ya kudhibiti uvuvi haramu katika mwambao wa Afrika Mashariki, sambamba na kuimarisha hali ya usalama katika ukanda huo.

Katika kikao hicho viongozi hao walikubaliana ziwepo ziara za mara kwa mara za viongozi wa ngazi mbali mbali la kuongeza maelewano na kuhakikisha utekelezaji wa mambo wanayokubaliana .