RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Waumini wa dini ya Kiislamu kufanya mambo mema kwa ajili ya kujiaandaa na mauti.Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa akiwasalimia waumini wa dini ya Kiislamu mara baada ya sala ya Ijumaa huko katika msikiti Nunge, mjini Dodoma.Katika salamu zake kwa Waislamu, Alhaj Dk. Shein aliwasisitiza haja ya kufanya mambo mema ili kujiandaa na mauti kwani kila mmoja atayaonja.
Alhaj Dk. Shein aliwaeleza Waumini hao wa dini ya Kiislamu kufanya mambo yatakayompwekesha MwenyeziMungu hapa duniani ili iwe faraja kwao huko akhera wendako.Aidha, Alhaj Dk. Shein alisisitiza haja kwa wauminiwa dini ya Kiislamu kuzidisha ushirikiano wao na umoja wao walionao katika kutekeleza mambo mema yatakayowasaidia katika maisha yao hapa duniani na kesho akhera.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwataka waumini hao wa dini ya Kislamu, kuifanyia kazi hotuba ya sala ya Ijumaa iliyotolewa na Khatibu wa Msikiti huo ambayo ilisisitiza haja ya waislamu kuwalea watoto wao kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (S.AW) juu ya malezi kwa watoto.
Khatibu huyo alisisitiza haja kwa waislamu kuwalea watoto wao katika maadili mema ambayo yatawasaidia katika maisha yao ya duniani na akhera.Katika hotuba yake pia, Khatibu huyo alieleza kuwa watoto wengi hivi sasa wamekuwa hawana malezi na badala yake wanajengeka katika mazingira ya kuwa waongo jambo ambalo limekuwa tatizo kubwa katika maisha ya wanaadamu hivi sasa.
Alieleza kuwa uongo umewapelekea hata wenye haki zao kuzikosa kwani wapo waislamu ambao hudiriki kusema uongo na kusimama Mahakamani na hupelekea mwenye haki yake kuikosa na huipata ambaye hana haki kutokana na uongo.
Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar yuko Dodoma ambapo leo anatarajia kuhudhuria katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM .kinachofanyika huko katika ukumbi wa Ikulu ya Chamwino, nje kidogo ya mji wa Dodoma.