RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesistiza haja kwa Wizara ya Katiba na Sheria kuandaa taratibu maalum za kuwaelimisha wananchi kuhusiana na sheria mbalimbali zilizopo nchini.
Dk. Shein amesema hayo Ikulu ndogo Kibweni mini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Wizara Katiba na Sheria, wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha Julai 2018 hadimweziMachi 2019.
Alisema utowaji wa elimu hiyo utawasaidia wananchi kufahamu kwa kina uwepo wa sheria mbalimbali na hivyo kuondokana na mkanganyiko katika masuala mbalimbali yahusuyo sheria.
Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na kazi nzuri iliyofanywa na Wizara hiyo katika utekelezaji wake wa majukumu, ikiwa pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutendaji.
Aidha, alisitiza haja ya viongozi wa Wizara hiyo kuwa wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ili waweze kupata ufanisi zaidi.
Dk. Shein alisema anamatumaini makubwa na Wizara hiyo iliyoanzishwa hivi karibuni ikiwa ni nguzo muhimu katika upatikanaji wa haki katika jamii, sambamba na uimarishaji wa dhana ya utawala bora hapa nchini.
Katika hatua nyengine Dk. Shein aliipongeza Wizara hiyo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake, ikizingatiwa Wizara hiyo inagusa masuala mbalimbali muhimu yanayoihusu jamii.
Nae, Waziri wa Katiba na Sheria Khamis Juma Mwalimu alisema uendeshaji na usikilizaji wa kesi za jinai na madai, unaozihusisha Ofis ya Mwanasheria mkuu, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na mahakama umeimarishwa na umekuwa ukiendelea katika mahakama zote nchini, wakati ambapo kwa mwaka wa 2018/2019, jumla ya kesi 8,485 zilisajiliwa na kesi 6,054 ikiwa sawa na asilimia 71 zikishughulikiwa.
Alisema katika kipindi hicho, Wizara iliendelea kuimarisha hali ya majengo ya mahakama Unguja na Pemba, wakati ambapo majengo manane kati ya 15 yakiwa katika hali nzuri hivi sasa baada ya kufanyiwa matengenezo.
Aidha ,alisema taratibu za ujenzi wa Mahakama Kuu Tunguu zimeanza kwa kupokea nyaraka zote kutoka kampuni zilizoomba tenda ya ujenzi huo, huku tathmini ya kumpata mkanadarasi ikiendelea kufanyika.
Waziri Khamis alisema katika kipindi hicho, Wizara hiyo ilikabiliwa na kazi ya kukamilisha mapitio na matayarisho ya sheria mbalimbali za kitaifa, ikwemo sheria ya mwenendo wa madai, sheria ya usimamizi wa mirathi, sheria ya mahakama kuu, sheria ya mawakili na sheria ya chama cha Mawakili na kubainisha haja ya upatikanaji wa fedha na rasilimali watu ilikuimarisha mfumo wa kisheria Zanzibar.
Alisema kukosekana kwa Ofisi ya Muendesha Mashtaka katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba, kumeisababishia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka gharama kubwa za mafuta kwa ajili ya kuwasafirisha watendaji kuelekea mahakama zilizomo katika Mikoa hiyo na kueleza umuhimu wa ujenzi wa ofisi ilikuondokana na tatizo hilo.
Wakati huo huo,Waziri wa Wizara ya kazi, Uwezeshaji, Wazee,wanawake na watoto,Moudline Castico akiwasilisha utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo alisema katika kipindi hicho Wizara iliratibu na kusimamia utekelezaji mpango wa pensheni jamii kwa wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, ambapo jumla ya wazee 27,783 wanaopokea pensheni hiyo Unguja na Pemba hadi kufikia mwezi Machi, 2019.
Alisema imeratibu upatikanaji wa ajira kwa wananchi 1,555 Unguja na Pemba, kupitia sekta binafs iikiwemo hoteli ,skuli binafsi na taasisi nyengine, sambamba na kuratibu ajira za nje ya nchi kwa vijana 1,033.
Aidha, Waziri Castico alibainisha kuwa Wizara hiyo imefanya ukaguzi maalum kwa taasisi 376 kuangalia utekelezaji wa agizo la kima cha chini cha mishahara huku taasisi 460 zikiwa tayari zimetekelez aagizo hilo.
Akigusia changamoto zilizoikabili Wizara hiyo, alisema ni pamoja na kuwepo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya fidia kwa wafanyakazi waliopata ajali wakiwa kazini ambapo zaidi ya shilingi Milioni 30.9 zinahitajika, pamoja na fidia ya zaidi ya shilingi Milioni 50.5 kwa ajili ya wananachi 248 walioanguka kutoka juu ya mikarafuu.