Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Awamu ijayo imepanga kujenga barabara mpya katika Kisiwa cha Tumbatu ili kuondoa changamoto ya muda mrefu ya miundombinu duni ya usafiri.

Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa mkandarasi tayari amekabidhiwa kazi hiyo na ameanza kuagiza vifaa kwa ajili ya kuanza ujenzi huo katika kipindi kifupi kijacho.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itajenga gati jipya katika Kisiwa cha Tumbatu ili kurahisisha safari za kuingia na kutoka kisiwani humo, hatua itakayochochea maendeleo ya huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Kuhusu upatikanaji wa maji safi, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali inaendelea na mradi wa kulaza bomba kuu baharini kwa ajili ya kusambaza maji salama kwa wakazi wa Tumbatu.

Ameongeza kuwa katika Awamu ijayo, Serikali itaendeleza uwezeshaji wa wavuvi kwa kuwapatia boti na vifaa vya kisasa ili waweze kufanya uvuvi wa bahari kuu.

Vilevile, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya elimu na afya, ikiwemo kuajiri walimu, madaktari na wauguzi wapya, pamoja na kuimarisha hospitali ya wilaya inayojengwa ili kutoa huduma za kibingwa kama upasuaji na uzazi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Muhammed Said Dimwa, ameeleza kuwa miaka mitano ya uongozi wa Dkt. Mwinyi imeleta mageuzi makubwa ya maendeleo Zanzibar, hususan Tumbatu, na amewataka wananchi kumchagua tena Dkt. Mwinyi na wagombea wote wa CCM ili maendeleo yaendelee.