Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeendesha kampeni za kistaarabu na kufanikiwa kuyafikia makundi yote ya kijamii nchini, hivyo kina kila sababu ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 24 Oktoba 2025, alipohutubia katika Mkutano Mkubwa wa Kampeni wa Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema kampeni za CCM zimekuwa za amani, umoja na zenye kuzingatia misingi ya kuheshimiana, jambo linalodhihirisha uadilifu na ukomavu wa kisiasa wa chama hicho.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa Wana-CCM na wananchi wote kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kukipatia ushindi mkubwa Chama Cha Mapinduzi, ambacho kimeendelea kuaminiwa na Watanzania kutokana na utekelezaji wa sera bora za maendeleo.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein, amesema vuguvugu la kampeni lililofanywa na Wana-CCM linaonesha wazi kuwa chama hicho kina kila sababu ya kushinda kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.
Ameongeza kuwa ushindi wa CCM utaleta maana kubwa kwa taifa, ikiwemo kulindwa kwa Muungano wa Tanzania, Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na kudumishwa kwa umoja, amani na mshikamano wa Watanzania.