Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inalenga kuviimarisha viwanja vya michezo nchini ili viwe bora na kukidhi viwango vya kimataifa.Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha inajenga viwanja zaidi vya kisasa vitakavyotoa nafasi kwa vijana kushiriki michezo na kukuza vipaji vyao.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo , tarehe 1 Oktoba 2025, katika fainali ya Michuano ya Yamle Yamle iliyozikutanisha timu ya Mazombi FC na Muembe Makumbi Combine, fainali iliyochezwa katika Uwanja wa New Amani Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kujenga viwanja vya kisasa katika kila wilaya ili michezo iwe sehemu ya ajira na maendeleo ya vijana.

Aidha, Rais amelitaja Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kama kinara katika kuendeleza michuano hiyo kwa msimu wa saba mfululizo, huku akilipongeza pia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kwa udhamini wake kama mdhamini mkuu.Katika mchezo huo wa fainali uliokuwa wa kusisimua, Muembe Makumbi ilitwaa ubingwa baada ya kuilaza Mazombi FC mabao 3–0, yote yakipatikana katika kipindi cha pili cha mchezo.

Rais Dkt. Mwinyi aliikabidhi Muembe Makumbi kitita cha shilingi milioni 20 pamoja na kombe la ubingwa wa msimu wa 2025/2026, huku Mazombi FC ikipokea shilingi milioni 10.Michuano hiyo ilibeba kaulimbiu: “AMANI AMANA.”