Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha miundombinu na ustawi wa wananchi wa Unguja na Pemba, kwa misingi ya umoja, mshikamano na maendeleo endelevu.

Amesema kuwa katika kufanikisha malengo hayo, Serikali itaendelea kuwawezesha wananchi kupitia mikopo isiyo na riba, mafunzo ya ujasiriamali, na kuendeleza maeneo ya michezo ili kuongeza fursa za ajira na kuinua kipato cha wananchi.Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo (06 Oktoba 2025) alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kwale, Mkoa wa Kaskazini Pemba, katika mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni kisiwani humo.

Amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kulipa kipaumbele eneo la Kwale kama ngome muhimu ya kihistoria ya chama, huku akiwataka wananchi kuendelea kukiamini na kukichagua CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao ili kuendeleza ajenda ya amani, umoja na maendeleo.Kwa niaba ya wananchi wa Kwale, Mzee Shaame Khatibu Hamadi amempongeza Dkt. Mwinyi kwa juhudi zake za kuimarisha umoja na maendeleo ya Wazanzibari, akimhimiza kuendeleza kasi ya mafanikio katika uongozi wake.

Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi ameshiriki mahojiano ya moja kwa moja kupitia Redio Jamii Micheweni, ambapo alielezea mwelekeo wa kampeni zake na malengo ya Serikali atakayoiongoza endapo ataaminiwa tena na wananchi katika Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na kuwaomba wananchi wa Zanzibar kumpa ridhaa ya kuendelea kuwatumikia.