Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wasiohubiri amani, akisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumza leo, tarehe 07 Oktoba 2025, katika Uwanja wa Michezo wa Likoni, Kojani, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Dkt. Mwinyi amesema viongozi wasioweka mbele amani hawana nia njema na ustawi wa nchi, hivyo akawahimiza wananchi kuendelea kuiunga mkono CCM ambayo imejidhatiti kudumisha umoja na utulivu wa Zanzibar.
Katika hotuba yake, Dkt. Mwinyi pia ametangaza kuwa Serikali inatarajia kujenga skuli 29 mpya Unguja na Pemba, hatua itakayowezesha wanafunzi wote kusoma kwa mkondo mmoja badala ya mfumo wa zamu mbili.
Akijibu ombi la wananchi wa Kojani, Dkt. Mwinyi ameahidi kujenga uwanja wa michezo kisiwani humo ili kukuza vipaji vya vijana. Pia ameweka bayana kuwa hospitali ya wilaya ya Kojani inaendelea kujengwa, sambamba na marekebisho ya gati ili kurahisisha matumizi ya boti ya wagonjwa (ambulance boat) aliyokabidhi rasmi leo kama sehemu ya ahadi zake.
Aidha, amesema Serikali imeagiza boti mbili za kisasa kwa ajili ya kuimarisha usafiri wa baharini baina ya Tanga, Pemba na Unguja, huku meli ya MV Mapinduzi ikitarajiwa kuanza safari zake hivi karibuni.Katika sekta ya uwezeshaji wananchi, Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa mikopo isiyo na riba kwa vijana na wajasiriamali ili kuongeza ajira na kipato.
Wananchi na wanachama wa CCM waliomsikiliza wamepongeza juhudi za Rais Dkt. Mwinyi za kuwaunganisha Wazanzibari na kufanikisha maendeleo makubwa kisiwani humo.Katika mkutano huo, wanachama 400 wa ACT Wazalendo wamejiunga na CCM, wakiahidi kumpa Dkt. Mwinyi kura za “ndiyo” katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29