Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kujenga masoko makubwa mapya matano ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika mazingira bora zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na wafanyabiashara wa Soko la Mwanakwerekwe akiwa katika muendelezo wa kampeni za uchaguzi.Ameyataja maeneo yatakayojengwa masoko hayo mapya kuwa ni Kinyasini, Mwera, Kibandamaiti, Kisauni na Kwahajitumbo.

Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa kukamilika kwa masoko hayo kutapunguza msongamano unaosababishwa na uhaba wa nafasi pamoja na kupunguza kodi wanazotozwa wafanyabiashara kwa sasa.

Rais Dkt. Mwinyi amewaomba wafanyabiashara na wananchi kumchagua tena pamoja na wabunge, wawakilishi na madiwani wa CCM ili kuiongoza Zanzibar na kutimiza dhamira ya ujenzi wa masoko hayo chini ya kaulimbiu yake ya Yajayo ni Neema Zaidi.

Aidha, amewasisitiza wananchi kudumisha amani ya nchi na kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi.