Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ina mpango maalum wa ujenzi wa majengo ya Afisi za Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahakama ili kuimarisha uwajibikaji, mazingira wezeshi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua majengo mapya ya Mahakama za Mikoa na Wilaya katika hafla iliyofanyika Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Mazizini.Amesema Mahakama ni miongoni mwa mihimili ya Serikali iliyokuwa ikikabiliwa na ufinyu na uchakavu wa majengo kwa muda mrefu, hali iliyozorotesha utendaji wake.
Ameeleza kuwa kuwa na majengo ya kisasa ya Mahakama yanayoendeshwa kidigitali ni hatua muhimu ya kuvutia ukuaji wa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi unaoendelea kuongezeka, kwani mahakama zenye miundombinu na utendaji bora huongeza imani kwa wadau.
Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Mahakama ya Mkoa Tunguu, Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliyopo Kiongele pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Magharibi iliyoko Kisakasaka, kunaashiria kuanza kwa mradi mwingine wa ujenzi wa Mahakama tano zitakazojengwa chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia.
Amesema mradi huo utatekelezwa mwaka wa fedha 2025–2026 na utajumuisha ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, Mahakama za Wilaya nne pamoja na matengenezo makubwa ya Mahakama ya Watoto Mahonda na jengo la Mahakama lililopo Wete, Pemba.
Aidha, ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji wa Haki kinachoendelea Chakechake, Pemba chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, ambapo kukamilika kwake kutawezesha Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mahakama ya Zanzibar na Mahakama za Wilaya kufanya kazi katika jengo moja.
Dkt. Mwinyi amepongeza pia hatua ya ujenzi huo wa Mahakama kutoa nafasi kwa taasisi na wadau wengine kufanya kazi zao ndani ya Mahakama ikiwemo Dawati la Jinsia, mawakili wa Serikali na wa kujitegemea, Polisi, Chuo cha Mafunzo, Ustawi wa Jamii, wasaidizi wa sheria,wazee wa baraza, Bodi ya Rufaa za Kodi, chumba cha akina mama kunyonyeshea watoto na chumba cha watu mashuhuri.
Ametoa wito kwa watendaji wa Mahakama kuitunza miundombinu hiyo ili ibaki na haiba yake kwa miaka mingi ijayo.Aidha, ameipongeza Mahakama na Kampuni ya CRJE–East Africa kwa kazi nzuri ya usanifu na ujenzi wa majengo hayo ya kisasa yenye hadhi ya Mahakama.