RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja kwa Mabalozi wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Urusi na Rwanda kutekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi kwani ndio silaha madhubuti ya kukuza uchumi wa Tanzania sambamba na kuimarisha uhusiano na nchi rafiki. Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipofanya mazungumzo na Mabalozi Wateule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliofika Ikulu kumuaga Rais pamoja na kufanya nae mazungumzo ambapo Rais alieleza kuwa Diplomasia ya Uchumi ndio kiu kubwa ya uchumi wa Tanzania hivi sasa. Mabalozi waliofika Ikulu kwa mazungumzo na hatimae kumuaga Rais Dk. Shein ni Balozi wa Tanzania nchini Rwanda IGP Mstaafu Enerst Jumbe Mangu na Balozi wa Tanzania nchini Urusi Meja Jenerali Mstaafu Simon Marco Mumwi.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa shabaha kuu ya Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuimarisha sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vikubwa, vidogo na vya kati hivyo ni vyema Mabalozi hao wakatumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchi hizo kuja kuinga mkono Tanzania katika mikakati yake hiyo iliyojiwekea. Akieleza uhusiano na uhusiano uliopo ambao ni kihistoria kati ya Tanzania na Urusi, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarishwa zaidi kama ilivyokuwa siku za nyuma hasa ikizingatiwa kuwa nchi hiyo imepata maendeleo makubwa katika sekta mbali mbali za kiuchumi na maendeleo vikiwemo viwanda vya aina zote.

Kwa upande wa Zanzibar, Rais Dk. Shein alisema kuwa Urusi ilikuwa na mashirikiano na mahusiano mema na hata kuweka ubalozi wake mdogo sambamba na kutoa nafasi nyingi za masomo, hivyo kuna kila sababu ya mahusiano hayo kuimarishwa zaidi kati ya pande mbili hizo. Dk. Shein alisema kuwa fursa kubwa ipo katika nchi ya Urusi hasa katika sekta ya utalii, uvuvi, wataalamu wa fani mbali mbali, viwanda, kilimo na nyenginezo ambazo nchi hiyo imezipigia hatua. Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano wa vyuo vikuu vya nchini Urusi na vyuo vikuu vya Zanzibar kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) nao ni muhimu sana hasa ikizingatiwa kuwa Urusi ina vyuo vikuu vingi hivyo, suala la kubadilishana uzoefu na utaalamu litaleta tija zaidi.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo uhusiano na ushurikiano katika kuwakaribisha wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar hasa katika sekta ya uvuvi na viwanda kwani nchi hiyo wana uzoefu mkubwa wa utengenezaji wa meli kubwa hasa ikizingatiwa katika historia kuwa meli kubwa ya kwanza duniani ilitengenezwa nchini Urusi. Akieleza mashirikiano na mahusiano mema yaliopo kati ya Tanzania na Rwandwa, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina uhusiano mzuri na Rwanda kwani wapo wananachi wa nchi hiyo ambao wanaishi Zanzibar huku akieleza jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika kusimamia amani na utulivu katika nchi hiyo. Kwa upande wa kuanzisha biashara ya samaki kati ya Zanzibar na Rwanda, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar italifanyia kazi wazo hilo lililotolewa na Balozi Mangu la Zanzibar kuanzisha biashara hiyo nchini Rwanda.

Pia, Dk. Shein alieleza kuwa tayari Zanzibar ilishawafikiana na Rwanda kuwa ndege zake la Shirika la ‘Air Rwanda’ kufanya safari kati ya Rwanda na Zanzibar ikiwa ni njia moja wapo ya kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar jambo ambalo linapaswa kutiliwa mkazo ili liweze kutekelezeka na kupata manufaa kwa pande zote mbili. Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwaeleza Mabalozi hayo umuhimu wa kuwa karibu na wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vya nchi wanazokwenda kuzifanyia kazi ili waweze kufarajika na kupata mashirikiano kutoka katika ofisi hizo za Ubalozi jambo ambalo pia, litasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.

Nao Mabalozi hao kwa nyakati tofauti walieleza kufarajika kwa kupata maelekezo na maoni sambamba na ushauri wa Rais Dk. Shein katika kutimiza majukumu yao wanayokwenda kuyafanya na kumuhakikishia Rais kuwa watatekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa ili Tanzania ikiwemo Zanzibar iweze kufikia malengo iliyojiwekea hasa katika azma yake ya Uchumi wa viwanda. Mabalozi hao walitoa pongezi na shukurani kwa Rais Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kwa kuteuliwa kwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi hizo. Aidha, Mabalozi hao walimuhakikishia Dk. Shein kuwa katika wadhifa wao huo juhudi za makusudi watazichukua kwa mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo na Tanzania unaimarishwa zaidi sambamba na kuimarisha maslahi kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabalozi hao walisisitiza kuwa Zanzibar ina fursa na maslahi ya pekee kwa nchi zote mbili wanazokwenda kufanya kazi hasa katika sekta ya utalii ambayo kwa upande wa Zanzibar sekta hiyo imeanza kupata mafanikio makubwa na kuahidi kwenda kuitangaza zaidi Zanzibar katika nchi hizo.