Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema madhehebu ya dini yana mchango mkubwa kwa Serikali katika juhudi za kudumisha amani na utulivu wa Taifa.Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 11 Septemba 2025 katika Kongamano la Kuiombea Nchi Amani lililoandaliwa na Umoja wa Akina Mama wa Kikristo na Maendeleo Zanzibar, lililofanyika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amefahamisha kuwa amani ni neema kwa maendeleo ya binadamu, inayopaswa kuenziwa na kudumishwa na kila mmoja kwa mustakabali wa Taifa.Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kutumia nafasi zao kuwaelimisha waumini umuhimu wa amani pamoja na kuwaandaa kuwa raia wema.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia akina mama hao wa Kikristo kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto zinazozikabili taasisi za dini ili ziweze kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi na amani.
Ameupongeza umoja huo kwa kuandaa kongamano hilo, alilolielezea kuwa ni la umuhimu mkubwa hasa katika kipindi hiki nchi ikielekea katika Uchaguzi Mkuu.